Kigwangala - Mtu wa Watu!

Wednesday, December 22, 2010
Mgombea Ubunge wa Nzega kupitia Chama Cha Mapinduzi ni mtu mcheshi, mwenye bashasha na anakubalika kwa watu wa makundi yote. Hapa anaonekana amekaa akiongea na bibi kizee wa Kijiji cha Ijanija, Kata ya Ijanija, kabla ya hapo alikuwa akielekea kuhutubia mkutano wa kampeni ambapo alisimamisha gari yake mara moja na kushuka kwenda kumsalimia kikongwe huyu ambaye alifurahi sana kumuona Kigwangalla kwa macho yake!

Watoto Wengi Wamepewa Jina la 'Kigwangalla' Jimboni Nzega!

 
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, jimboni Nzega ambako mgombea Ubunge wa CCM Dk. Hamisi Kigwangalla, ambaye alipewa Utemi wa Makaranga Ng'wana Ng'washi walizaliwa watoto wengi na kupewa jina la 'Kigwangalla' kwa mapenzi na mvuto wa mgombea huyu wa CCM, ambaye mwisho wa siku aliibuka mshindi wa uchaguzi huo! Mpaka leo hii takriban watoto 32 wamezaliwa kila pande ya Nzega na kupewa jina la Mbunge huyo...Huyu anayeonekana pichani ni mtoto Kigwangalla ambaye alizaliwa katika kijiji cha Ijanija, kilichopo kata ya Ijanija, Wilayani Nzega. Pembeni yake ni Bibi wa mtoto huyo akiwa amemshika kichwani kaka mkubwa wa 'Kigwangalla'.

Dk Kigwangala awakaba Resolute

Thursday, December 9, 2010
Dk Kigwangala awakaba Resolute
Mwananchi, Jumatano Desemba 1, 2010

Na Mustapha Kapalata, Nzega

   MBUNGE wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangala, amesema mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Nzega Golden Pride Mine Ltd, hauna manufaa na wananchi wa jimbo hilo.
    Kauli ya mbunge huyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kuanza kutumikia wananchi, akianzia ziara yake kwenye mgodi huo.
    Dk Kigwangala alifanya ziara ya kushtukiza mgodini hapo jana na kukutana na Meneja Mwendeshaji, Les Taylor, akimtaka kueleza jinsi wananchi wanavyonufaika na mgodi huo.
    Hatua ya Mbunge inatokana na kero kubwa ya maji inayowakumba wananchi wa Nzega. Hivi sasa plastiki la lita 20 za ujazo linanunuliwa kwa sh 1,500.
    Mbunge huyo alisema mgodi huo hauna msaada kwa wananchi wa jimbo hilo kwani, uongozi wa mgodi huo hautoi huduma muhimu kama maji kwa wananchi, ilhali wanaendelea kukausha vyanzo vya maji.
    Dk Kigwangala alisema uhusiano wa wawekezaji hao na wananchi wanaozunguka eneo hilo, ni sawa na chui na paka, hawaelewani kutokana na utawala wa mgodi huo unaodharau raia kwenye nchi yao.
     Alisema mikataba iliyofungwa enzi hizo siyo yakinifu ambayo itanufaisha wananchi wa Nzega na watanzania na kwamba, inalenga kunufaisha watu binafsi.
     Kuhusu mrahaba unaolipwa kwa halmashauri wa sh 200 milioni kwa mwaka, Dk Kigwangala alisema kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na rasilimali wanayovuna.
    "Kwa kweli kama mbunge, mikataba hii ni ya kihuni , siridhishwi nayo hata kidogo, kiwango wanachotoa ni bora wangechimba bure. Hawana msaada kwa watu wa taifa hili, wanachokifanya ni kuongeza umaskini, naheshimu sana mikataba lakini huu siridhiki nao," alisema Dk Kigwangala.
     Alisema muda wa uchimbaji kwa mgodi huo unakaribia kumalizika na wananchi wataachiwa mashimo, yenye madhara makubwa kwa afya zao, huku akimtaka meneja huyo kurekebisha haraka uhusiano wao na wananchi.
     Kwa upande wake, Taylor alimshutumu mbunge huyo kwa kufanya ziara isiyo rasmi na kwamba, alitakiwa kutoa taarifa kama mbunge kuingia mgodini.
     Taylor alisema malalamiko ya wananchi kuhusu uhusiano siyo kazi ya mgodi, bali serikali ambayo inatakiwa kutimiza ahadi zake.
     Alisema kampuni inatoa msaada pindi inapoguswa na tatizo, siyo lazima na halihusiani na mkataba wao.
Awali, Dk Kigwangala alitembelea vyanzo vya maji na Meneja wa maji wilaya ya Nzega, Samuel Buyigi, akimweleza kutokuwepo kwa uhusiano mzuri na mgodi huo ambao unakausha vyanzo vya maji.
     Buyigi alisema mgodi huo unachukua maji kutoka vyanzo vya maji na kwamba, vingine vimeanza kukauka, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi.
Makada wa CCM Nzega, Dr. Hamisi Kigwangalla (Kushoto) na Ndg. Hussein Bashe (Kulia) wakibadilishana mawazo wakimsubiri Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete atue viwanja vya Shule Bukene kabla ya kuhutubia mikutano miwili ya Kampeni Jimbo la Bukene na Jimbo la Nzega. 

Ka Obama Vile! Watu wangu wa Kata ya Lusu...

Sunday, August 8, 2010
Watu wangu wa Kata ya Lusu waliniita Obama...walishangilia kwa bashasha ya hali ya juu lilipotajwa jina langu Dr. Hamisi Kigwangalla a.k.a 'Shimba Ngosha'. Basi nami sikuwaangusha, hakika niliunguruma kama simba dume, nilitoa hotuba ya ukweli iliugusa kila moyo wa mwana Lusu aliyekuwepo pale. 

Nata ilikuwa balaa, mpaka nashindwa kusema neno lolote lile...walinipokeaje?

Isanzu, mh....

KURA ZA MAONI NZEGA!

Jamani, Uchaguzi si mchezo si lelemamaaa...

Hili ni baadhi tu ya mabango yaliyotumika kuuza sura, sera na jina la mbegu mpya, bora na ya kisasa inayoitwa "Kigwangalla"...pale Nzega kwa wanaCCM.

Tabasamu hili liliupamba mji wa Nzega...

Nikiliangalia napata fikra za kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa watu wangu wa Nzega...Mungu nipe uwezo.

Nimejifunza mengi sana ila moja ni la msingi na halitatoka kifuani mwangu mpaka kufa - wapende wapiga kura wako maana wao ndiyo mtaji na msingi mkuu wa kazi ya kisiasa!

Kuoa Uchagani kuna raha zake!

Friday, May 21, 2010
wikiendi iliyopita mke wangu Mama Sheila na Mimi tulitembelewa na wageni. Wageni hao, wakwe zangu na mashemeji walituletea supu (mbuzi wawili) ya mzazi (mama Sheila) kwa ajili ya kunywa na kuleta maziwa ya kutosha. Hii ni baada ya kufurahishwa na ujio wa Mtoto wetu wa pili tuliyempa jina la Hawwah Kigwangalla. Hawwah ni jina la mama mkwe wangu.

Dk. Hamisi Kigwangalla na Kilimo Kwanza Nzega: Kilimo cha Pamba Kinawezekana!

Jitihada za kufufua kilimo cha zao la biashara la pamba Nzega, Tabora zinaelekea kuzaa matunda baada ya mwanga wa mavuno mazuri kuonekana. Zifuatazo ni picha zilizopigwa na Mkurugenzi wa Mradi wa Kuendeleza Pamba Nzega - yaani Nzega Cotton Development Project (NZECODEP), Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa na wadau wengine wa wilayani Nzega wakati wa tathmini ya mradi inayoendelea kule wilayani Nzega. Mpaka sasa dalili zinaonyesha kuwa kilimo cha pamba kitaleta mapinduzi makubwa ya uchumi wa mkulima Nzega, baada ya mradi kuwawezesha wananzega kutegemea kupata wastani wa kilo 1200 kwa ekari moja; kiwango kikubwa kuliko wastani wa taifa wa kilogramu 400 tu kwa ekari. Hii ni kutokana na uhamasishaji mkubwa uliofanywa na wafanyakazi mahiri na waliojitoa wa kampuni ya MSK Solutions Ltd, ambaye ni mmiliki wa mradi huo. Mradi huu unahamasisha matumizi kidogo ya madawa ya kuua wadudu na matumizi ya samadi au mboji pekee (kwa ajili ya kutunza ardhi) badala ya mbolea za kisasa za chumvichumvi. Hii inaifanya pamba ya Nzega iwe na hadhi ya pamba hai (organic cotton). Matumizi madogo ya dawa yanawezeshwa na kutumika kwa mfumo wa zao mtego (Integrated Pest Management, IPM) na zao linalotumika Nzega ni alizeti, ambayo inawawezesha wakulima pia kuvuna na kujipatia mafuta kwa ajili ya kula na mashudu kwa ajili ya mifugo yao.

Mradi unaelekea katika ujenzi wa kiwanda cha kuchambua pamba (cotton ginnery) mjini Nzega, kilimo cha mkataba kwa mwaka wa kilimo wa 2010/2011 ambao ni mwaka wa pili wa mradi na pia kutanuka zaidi na kuunganisha wilaya jirani ya Uyui.

Hizi ni harakati za mashirika na watu binafsi kujitokeza kuunga mkono azimio la Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete la Kilimo Kwanza kwa vitendo. Na tayari mafanikio yameshaonekana. Ushirikiano huu utawaletea manufaa makubwa wakulima na taifa kwa ujumla. Wengine wengi zaidi tujitokeze. TUKISHIRIKIANA TUTAJENGA UCHUMI IMARA!

Dk. Hamisi Kigwangalla atangaza rasmi kwa waandishi wa habari nia ya kuwania ubunge Nzega

Wednesday, March 10, 2010
Tarehe 10 Machi 2010

Dk. Hamisi A. Kigwangalla (MD, MPH, MBA) ni kijana msomi mwenye umri wa miaka 35, mwenye digrii tatu na aliyebobea katika taaluma ya afya ya jamii na utawala wa biashara. Dk. Kigwangalla ni kijana wa kitanzania anayeamini kwenye fikra mbadala na za kisasa lakini anaamini katika misingi iliyowekwa na wazee waasisi wa TANU na ASP. Alihitimu masomo ya digrii ya udaktari wa tiba ya binadamu (yaani Doctor of Medicine, MD) kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam mnamo mwaka 2004. Pia ni muhitimu wa digrii mbili za uzamili; moja ambayo ni Masters in Public Health Sciences (major: Safety promotion) – kwa Kiswahili inatafsirika kama digrii ya uzamili katika sayansi ya afya ya jamii (amebobea kwenye kuhamasisha usalama), alihitimu mwaka 2007 kutoka chuo kikuu cha Karolinska Institutet, Stockholm, Sweden, na ya pili ni Masters in Business Administration (major: organization and leadership) – ambayo kwa Kiswahili inatafsirika kama digrii ya uzamili katika utawala wa biashara (amebobea kwenye mambo ya uongozi na miundo ya mashirika) aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Blekinge (Blekinge Institute of Technology), pia kilichopo Sweden, mjini Ronneby.

Dk. Kigwangalla anaamini katika kutoa mchango wake juu ya maendeleo ya jamii kuliko kusubiri atafanyiwa nini na Taifa lake. (kama alivyowahi kusema raisi wa zamani wa marekani Bw. Abraham Lincoln).

Dk. Kigwangalla ni mtu anayefanya kazi zake kwa umakini, spidi na maarifa, na kuzingatia misingi ya maendeleo na uwajibikaji. Ni mwanapinduzi anayeamini mapinduzi ya Uchumi wa Tanzania yako karibu, na kwamba tutaendelea tu kama tutabadilisha fikra zetu (change of mindset). Anaiona Tanzania kama ni nchi yenye fursa nyingi na kwamba ni nchi iliyokaa vizuri na tayari tayari kuyapokea mapinduzi ya kiuchumi (Tanzania ni miongoni mwa emerging economies in Africa). Anaamini kuna haja ya kuwapa nafasi watu ambao wanayaona maisha kwa macho tofauti, badala ya kuangalia matatizo tu wanaangalia fursa ziko wapi ndani ya hayo matatizo. Bila kubadilisha mtazamo wetu hatutoweza kusonga mbele, itakuwa ni sawa na kujaribu kukimbiza jahazi nchi kavu!

Yeye anasema “maadui wa Tanzania wanajulikana na njia za kupambana nao zinajulikana – maadui hawa wapo toka nchi hii ianze, sasa kama maadui tunawajua na silaha za kuwamaliza tunazo, tunangoja nini sasa?....” Hapa anaongelea Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Yeye anaona kuna ya haja ya viongozi mahiri na wenye nia thabiti ya kuwatumikia watu wajitokeze popote walipo na waje kuongeza nguvu kwa taifa letu ili tuweze kupambana na maadui hawa. Anasema, “tatizo kubwa ni kwamba watu wengi wanaogopa kuingia kwenye ‘mainstream politics’ kwa kuwa hawajiamini katika uwezo wao wa kukabili mikiki mikiki inayoendana na siasa, wengine wanafikiri siasa ina wenyewe, wengine wanasubiri wastaafu ndiyo waingie kwenye siasa (hivi utaweza kutawatumikia watu vizuri wakati ukiwa umechoka?). vijana wengi wasomi na wachapakazi wazuri kabisa wanasahau kwamba siasa na mfumo wa maisha yao ya kila siku na kwamba hadi majumbani mwao wanafanya siasa– wengine ni watu makini sana na wangeweza kuchangia mengi kwenye kuleta maendeleo ya taifa letu, ……tatizo kubwa ni kwamba watanzania ni wazuri sana wa kusema na kupanga lakini ni wavivu wa kutekeleza, hivyo tunahitaji viongozi watendaji kwenye kila sekta, popote walipo wafanye mabadiliko! Tuache kuongea na kupanga tu, sasa tuanze kuwa mabingwa wa utekelezaji!” “….pia viongozi wengi si wabunifu, wachovu wa kufikiri na hivyo hata utendaji na usimamizi wao wa sera nzuri zilizowekwa unakuwa mbovu”

Dk. Kigwangalla anasema kwa kuyaangalia yote haya na ametafakari kwa umakini na kujipima uwezo wake, ameonelea aanze kwa vitendo ili awe chachu ya mabadiliko kwa watu wa Nzega, ambako ndipo alipozaliwa. Anasema, “jamani Charity begins at home na ndo maana nimeamua kuwania ubunge wa Nzega ili nishiriki kikamilifu na kwa ukaribu zaidi pamoja na wana Nzega wenzangu katika kuzikabili changamoto za maendeleo katika jimbo la Nzega kwa spidi na kwa ubunifu wa hali ya juu…..maana mimi kila nikiiangalia Nzega sioni matatizo bali naona fursa tu za kuleta mabadiliko, nashindwa kuelewa kwa nini sasa watu wakose mahali pa kunyweshea mifugo yao wakati mungu ametujaalia mabonde na mito ya kumwaga kabisa? Siku moja nilipita kijiji cha Nata, ambacho kipo karibu kabisa na bonde la mto Manonga, nilishangaa na kusikitika sana kuwaona akinamama wakifuata maji mbali kabisa na miji yao, takriban kilomita tano au saba! Eti kijijini hakuna visima, kweli?” Nikafuatilia sana suala hili nikagundua kuwa tatizo haliishii hapo tu, wakazi wa vijiji vya sehemu moja huwa wanalazimika wakati wa kiangazi kupeleka mifugo yao kuwekeza kwenye vijiji vilivyo karibu na mto, kweli tumeshindwa hata kutega maji kwa ajili ya mifugo yetu?”

Japokuwa Nzega ina fursa nyingi, na ni mojawapo ya wilaya kongwe, kasi yake ya maendeleo haiendani na fursa zilizopo. Nzega ilikuwa ni wilaya ya mbele kimaendeleo tangu miaka ya 60, mzunguko wa hela ulikuwa mkubwa, miundo mbinu ilikuwa na hali nzuri zaidi ya sasa ukilinganisha na wilaya zingine, lakini kasi yake ya ukuaji hairidhishi na shughuli za uchumi na maendeleo zinazidi kuzorota siku hadi siku.

Dk. Kigwangalla anasema “kasi ya maendeleo ya Nzega hairidhishi na matatizo mengi ya msingi hayapatiwi ufumbuzi…kero zinazowakabili watu wa Nzega ni nyingi na zinahitaji mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kubuni miradi mbalimbali itakayoweza kuharakisha maendeleo ya Nzega. Wananchi wa Nzega wanahitaji kuwa na kiongozi mwenye kupenda maendeleo, mwenye fikra mbadala na mwenye uwezo wa kuanzisha msukumo mpya wa kasi ya maendeleo kulingana na kero zao na vipaumbele vya kisera na kimikakati vya kiwilaya na kitaifa.” “Kuna mambo mengi hayajakamilika na utekelezaji wake unalegalega – nyumba za walimu na baadhi ya vyumba vya madarasa kwenye mashule ya kata havijakamilika, waalimu hawatoshi kwenye shule zetu mpya; huduma duni za ugani kwa wakulima, hali ya miundo mbinu vijijini bado hairidhishi.”

Mke wangu siku moja aliniuliza swali, maana yeye huwa muoga sana na hapendi sana mikakati yangu ya kuingia kwenye siasa, “hivi kwa ni haswa unataka kugombea Ubunge? Si ufanye tu mambo yako?” Na mimi sikusita kumjibu kuwa: “Ninataka kugombea Ubunge kwa kuwa ni uwezo mkubwa wa kuwatumikia watu, nina wito na ni haki yangu ya msingi kikatiba”. Alivyo kin’gang’anizi akaendelea “kwa nini lazima wewe tu, si uwaache wengine wafanye?” Nikamwambia: “mimi naona kama mambo hayaendi inavyopaswa na ninajiona kama ninaweza kuyafanya kwa ubora zaidi, sasa kwa nini nisitoe mchango wangu kwa taifa? Nikamuuliza wewe ni daktari, umeshuhudia akinamama wangapi wakipoteza maisha kwa kukosa huduma, wengine wakizalia njiani bila msaada wowote wa huduma? Je haya mambo kama yakipata watu wenye nia ya kweli ya kubadili mambo hayatendeki?” akanyamaza. Kwisha kazi yake. “mimi nikiangalia mjane aliyeachwa na babu yangu mdogo pale Inagana, Magengati naona kama anahitaji msaada kidogo tu aweze kumudu kuendesha maisha yake. Ndugu zangu wanaolima vitunguu kule Milambo-Itobo hawahitaji vitu vikubwa sana, wanahitaji wapate mtu wa kuwatetea na kuwaongoza kidogo tu waweze kupata faida zaidi kwenye shughuli zao na waboreshe zaidi maisha yao. Ni watu kama hawa wanaonifanya nijisikie wito zaidi wa kwenda kushirikiana nao kuleta mabadiliko katika maisha yao na familia zao, naona kama wamewekwa pembezoni na hawana mtetezi!

Mzee wangu Mzee Masanilo ni mkulima stadi na mahiri sana, hahitaji vitu vikubwa wala vya kutisha, yeye anahitaji soko la uhakika tu la mazao yake ya pamba, alizeti na mpunga. Wadogo zangu, akina Fatu na Ibra wao wanahitaji uhakika wa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na au vyuo vya kati (vya kutoa Diploma na Vyeti) vya kuwapa ujuzi na maarifa, wanahitaji madaraja ya kupandia chuo kikuu, wanahitaji hizi fursa ziwepo. Zote hizi ni kero, na tunazijua, je ni lini tutazifanyia kazi? Kwa nini tunashindwa? Ninajiona kama nina majibu ya maswali yote haya na ninadhani naweza kuyafanyia kazi ipasavyo.

Leo hii nimeamua kuiweka nia yangu hadharani kabisa kuwa kwa ridhaa yangu na matakwa yangu binafsi, nafsi yangu inanituma na hapa basi natangaza rasmi nia yangu ya kuvuta fomu kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), pindi wakati utakapowadia. Naomba mungu aniongoze. Amina.

Dk. Hamisi Kigwangalla’s Contacts are:

0715636963
0754636963
0784636963

Email: hkigwangalla@gmail.com

Website: www.peercorpstrust.org

Dk. Hamisi Kigwangalla Kutangaza Rasmi Nia ya Kuwania Ubunge wa Jimbo la Nzega 2010

Tuesday, March 2, 2010
Mwanasiasa machachari na chipukizi, Dk. Hamisi A. Kigwangalla, ambaye ni mkazi na mzaliwa wa wilayani Nzega, Tabora anajipanga kutangaza rasmi nia yake ya kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia chama cha mapinduzi. 

Dk. Kigwangalla, ambaye anajiweka kama ni mtu mwenye kupenda maendeleo, anayeona mbali na mwenye nia ya dhati ya kuwaendeleza wanaNzega na watanzania wenzake walio maskini zaidi, alikuwa na haya ya kusema: "...mungu akinijaalia ninapanga kutangaza rasmi nia yangu ya kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia CCM kwenye uchaguzi ujao (yaani wa Mwaka 2010), hili linakuja sana baada ya kufuatwa na kuombwa na watu mbalimbali wa rika tofauti tofauti....nimejifikiria sana na ninadhani kama kila kitu kitaenda sawa naweza kufuata ushauri wa watu, kwa sasa hivi bado nashauriana na familia yangu, ndugu, jamaa na marafiki, wakiona nisonge mbele basi ninapanga kutangaza hadharani kupitia vyombo vya habari mnamo wiki ya kuanzia Machi 08, 2010."

Dk. Kigwangalla ni mwanaharakati, mkulima na mjasiriamali kijana aliyezaliwa wilayani Nzega miaka takriban 35 iliyopita na ni msomi wa digrii tatu ikiwemo ya kwanza ya udaktari wa tiba za binadamu (Doctor of Medicine), ya afya ya jamii (MPH) na ya utawala wa biashara (MBA). Kwa sasa anajishughulisha na kilimo na mambo ya harakati za kuleta maendeleo kwa kinamama, watoto na makundi mengine yaliyo katika hatari zaidi.

Tarehe 5-2-2010: Maadhimisho ya Kuzaliwa kwa CCM Nzega

Sherehe za kuadhimisha miaka 33 tangu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kizaliwe zilivutia na kufana sana pale wilayani Nzega ambapo mgeni rasmi siku hiyo alikuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tabora Mh. Hassan Wakasuvi. 

Sherehe hizo zilianza alfajiri ya siku hiyo ya tarehe 5/2/2010 (ambayo ndiyo siku ya kuzaliwa kwa CCM, chama tawala Tanzania) kwa Viongozi mbalimbali wa kimkoa wakiongozwa na Mwenyekiti Wakasuvi, Katibu wa CCM Mkoa Ndg. Iddi Ali Ame, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tabora Ndg. Julius, na wajumbe wengine wa Kamati ya Siasa Mkoa kushiriki maandamano ya mshikamano yaliyoanzia kwenye viwanja vya ofisi ya CCM wilaya na kuishia Kitangiri na baadaye ofisini ambapo mgeni rasmi alitoa hotuba fupi iliyolenga katika kuhamasisha mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM Nzega. 

Pia Viongozi wa Kiwilaya, wanachama, wakereketwa na wapenzi wa CCM Nzega walikuwepo. 

Kabla ya kuwasilisha hotuba yake, Ndg. Mwenyekiti Wakasuvi na viongozi wengine wa CCM Mkoa na Wilaya walishiriki kupanda miti ili kuboresha mazingira ya ofisi ya CCM wilaya Nzega na kuweka alama ya ukumbusho.

Sherehe za Kuadhimisha Kuzaliwa kwa CCM (5 Februari 2010) Zilivyofana Nzega



Mh. Asha Kabeke (kwenye kiti) wa Kundi la 'Hiari Stars' akikata mauno na Mh. Diwani mwenzake.

Mwenyekiti Wakasuvi (Kulia) akiwa na Mh Diwani Basilio (Katikati) na Kada wa Chama

Sherehe za Kuadhimisha Kuzaliwa kwa CCM (5 Februari 2010) Zilivyofana Nzega

Asubuhi saa kumi na mbili kamili viongozi wa chama na serikali; wanachama, wakereketwa na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Nzega walijidamka na kukusanyika kwenye viwanja vya ofisi ya CCM wilayani hapo, kwa malengo ya kushiriki kwenye matembezi ya hiari yaliyolenga kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama. Matembezi hayo yalifana sana na yalifanywa kuwa rahisi kwa kutumbuizwa na nyimbo za kuhamasisha zilizoletwa na wahamasishaji mahiri.

Picha hapa chini inawaonesha:- Kutoka Kushoto: Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Mzee Hassan Wakasuvi akiwa na Makada wa CCM Wilaya ya Nzega, Ndg. Babu Rajabu Ahmed (ambaye pia ni Katibu Tawi wa CCM, Tawi la Nzega Mjini Magharibi), Dk. Hamisi Kigwangalla na Ndg. Salum Juma (ambaye pia ni Katibu Tawi wa CCM, Tawi la Nzega Mjini Mashariki). Picha hii ilipigwa mara baada ya watembeaji hawa kurejea kwenye viwanja vinavyozunguka ofisi ya CCM wilaya ya Nzega, ambapo matembezi haya yalianzia.