Dkt. Kigwangalla Ahutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Kumaliza UKIMWI kufikia Mwaka 2030

Tuesday, June 21, 2016

Hotuba ya Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB), Mwenyekiti wa TAMISEMI Alipotangaza Nia Kugombea Urais 2015

Sunday, September 7, 2014

Hotuba Aliyoitoa Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB (Nzega), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, kwa Waandishi wa Habari Kutangaza Nia ya Kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwaka 2015 Kwenye Ukumbi wa Zanzibar, Hyatt Regency, The Kilimanjaro Hotel, Dar es salaam, Siku ya Tarehe 7 Septemba 2014.


Utangulizi


Ndugu viongozi mlioko hapa, wazazi wangu, wageni waalikwa, wanahabari, marafiki zangu, mke wangu na watoto wangu,

Nianze kwa kuwashukuru viongozi wa dini kwa dua za utangulizi.

Pia nitume salamu zangu za rambirambi kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Eng. Evarist Ndikilo na ndugu, jamaa na marafiki wa watu waliopoteza maisha kutokana na ajali mbaya ya gari iliyotokea juzi. Pia nitumie fursa hii kutuma salamu zangu za rambi rambi kwa Inspekta Mkuu wa Jeshi la polisi, IGP Ernest Mangu, ndugu wa marehemu na askari wote wa jeshi la polisi kutokana na uvamizi wa kituo cha polisi kule Bukombe. Na pia naomba nitumie fursa hii kumpa pole Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi, CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kupata ajali eneo la Misungwi, Mwanza.

Ndugu zangu mlioko hapa, ni heshima na furaha kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezimungu kwa kutujaalia uhai na kutukutanisha hapa siku ya leo. Pili niwashukuru nyote mliofika hapa kuja kunisikiliza. Niwashukuru zaidi waandaaji wa Mkutano huu kwa kujitoa na kwa namna ya kipekee niwashukuru wazazi wangu, mke wangu na wanangu Sheila, Hawa na HK Jr kwa uvumilivu na kwa kuendelea kunitia nguvu ya kusonga mbele.

Leo nitasema neno zito kidogo, kama nilivyoahidi siku chache zilizopita. Neno nitakalolisema hapa litabadilisha sura ya historia yangu milele. Ninawashukuru nyote kwa kuitikia wito wa kuja kuwa mashuhuda wa namna historia itakavyoendelea kuandikwa hapa.

Kinachotokea hapa leo hii kina maana kubwa sana kwa watu wenye historia inayofanana na mimi. Wale ambao wameyajua maisha ya shida na kukosa uhakika toka wakiwa tumboni mwa wazazi wao kutokana na hali za uchumi wao. Wale wenzangu na mie ambao kesho yao haina uhakika; wale ambao wengine hupenda kuwaita ‘wanyonge’, ambapo mimi nikijitazama nilikotoka husema, hapana, hawa si wanyonge bali ni ‘simba aliyelala.’

Shukrani Kwa Urithi Toka kwa Waasisi na Wazee Walionitangulia


Mimi ninayezungumza hapa nimeyajua maisha ya mtu mnyonge na maskini kwa kuyaishi na si kwa kusoma ama kusikia. Ninajua mtu akiongelea njaa anamaanisha nini, sihitaji kufundishwa, najua. Nasema haya maana naujua ugumu wa kumuelewesha mtu anayekula milo mitatu kwa siku, tena ya kujipakulia kuwa kuna wengine wanakula pilau sikukuu hadi sikukuu. Ni ngumu sana kumuelewesha mtu wa aina hiyo kuwa wapo watoto wanaogombania chakula kwenye sahani moja. Maana kila siku yeye huwashuhudia watu wa dunia anayoishi wakihangaika kutembea umbali mrefu ili wapunguze vitambi na wakae kwenye ‘shape’ na hajui kama kuna watu wanatembea umbali mrefu ili kutafuta chakula wasukume siku!

Ni katika nchi chache sana duniani, mtoto mwenye historia ya maisha kama yangu, aliyewahi kutembea mitaani akiuza karanga, Big G, maandazi na jerebi ili kusaidia wazazi kupata chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota ndoto ya kuwa Rais wa nchi yake. Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari.

Hii inamaanisha jambo moja kubwa, kwamba misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa Taifa letu haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na inafanya kazi. Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ama wa kiongozi, ndiyo uoneshe kipaji chako. Inadhihirisha kwamba, ukipigana ndani ya Tanzania unafanikiwa!

Hili peke yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kusonga mbele zaidi – nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa sawa bila kujali nani anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania itakayodumu kwenye misingi hii. Kwamba, ndani ya Tanzania, si lazima mtoto wa mama ntilie awe ‘baba-ntilie’ – anaweza kuwa mmiliki wa hoteli kubwa ya kitalii!

Kwa namna ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Taifa letu kwa kuzilinda tunu hizi, maana ninaamini kuwa hatuwezi kuizungumzia kesho bila kukumbuka shida na raha tulizopata jana.

Leo nimefika hapa kwa sababu chama changu kina mfumo mzuri ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa na wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi tumeukuta. Leo nimefika hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami nina haki ya kuwa Mbunge. Na leo nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo itakayotoa uongozi wa Taifa letu katika awamu ijayo.

Babu yangu mzaa baba aliishi Kijijini Goweko, eneo la Mlimani, na alikuwa mfugaji mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi maisha ya heshima kubwa pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa japokuwa Babu yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU na baadaye CCM katika ngazi ya Kata.

Babu yangu mzaa mama alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na alishiriki harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU. Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili heshima na kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya utawala dhalimu wa wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na hivyo alifanya juhudi kusomesha mabinti zake; mama yangu aliishia kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa ajili ya mabinti zangu, Sheila na Hawa, na kaka yao, HK Jr. Ninaamini kila mzazi wa kizazi changu ana ndoto inayofanana na yangu kwa watoto wake.

Ninaamini historia ya maisha yangu siku moja itaandikwa na itawasisimua na kuwapa matumaini makubwa vijana na watoto chini ya miaka 35 ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wote. Mmoja wa wajukuu zangu ataisoma na kusema ‘doesn’t it get better than this?’

Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano hai wa historia ya maisha ya watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo kwa kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi vilivyonitangulia. Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.

Mahusiano ya Watu na Serikali Yao


Kazi yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu – vijijini na kwenye majiji, imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu hawa anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.

Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa matabibu wenzangu pale hospitali ya Taifa Muhimbili, ama kwa wafanyabiashara na wachuuzi pale sokoni Kariakoo, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na wachache wasio waadilifu.

Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.

Nenda kule Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo siku zote. Wanachohitaji wao ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi, waelekezwe wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji, mwisho wa siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa wala kucheleweshewa malipo.

Watu hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote.   Lakini wanaamini kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya baadaye ya watoto na wajukuu zetu. Tutaiondoa Tanzania miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.

Na mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa kabisa kwamba, tunaweza kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua milango ya maisha bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila mtanzania kuishi kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule kuanzia leo. Tutaweza kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi akitumaini na kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye ataishi kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.

Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali yetu, haya ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.

Watanzania wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye uchumi wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi yetu kwa sasa na baadaye, tutafanikiwa.

Tamko Rasmi la Nia ya Kugombea Urais na Sababu


Ndugu zangu nyote mliopo hapa, natangaza rasmi, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.

Na nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na utayari wangu. Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa kina: mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto za kizazi chetu; uwepo wa fursa ya kugombea na kushinda uchaguzi ujao; uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, na kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia utekelezaji; uadilifu na uzalendo wangu; na zaidi nia yangu ya kuwa sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika nchi yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu ya mabadiliko ya namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa na namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia.

Ninatangaza nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania wanipime na kunitazama mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa kuwa nitapimwa na kuungwa mkono ama kutoungwa mkono, si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi yangu, si kwa umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye jamii, ama dini yangu, ama kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa rekodi yangu, sifa, utayari, dhamira na uwezo wangu, kama mtanzania.

Natangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano ili nipate fursa ya kuukimbiza uchumi wetu kutoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi. Mimi ni mwanamabadiliko, ninaamini nikipewa fursa, nitashirikiana na watanzania wenzangu na kwa pamoja tutaunyanyua uchumi wetu kutoka kiwango cha kukua cha tarakimu moja kwenda kile cha tarakimu mbili kwa miaka yote ya uongozi wangu. Ninaamini tutaweza kwa pamoja kuukuza mchango wa kilimo kwenye GDP kutoka asilimia 4.2 kwenda zaidi ya asilimia 6. Tukiyafanya haya naamini tutakuwa tumezalisha ajira nyingi zaidi kuliko leo.

Ninaamini katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye matamanio yetu. Kizazi chetu cha viongozi kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye ahadi inayotokana na ndoto za waasisi wa Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi wowote ule, maana naamini tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa na watu wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho: kupigana na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na umakini wa hali ya juu. 

Na ndugu watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa tuna kazi ya ziada ya kufanya mbele yetu. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye kuchukua hatua za kutenda.

Kutathmini na Kuwapima Watia Nia


Nyote mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la kututazama kwa ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote; tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa, ili wakati muafaka ukifika muwape taarifa sahihi watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa kuliongoza Taifa hili kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!

Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na kuamua kwa busara kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada ya kupima na kuchambua aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.

Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa na wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa na Katiba yetu, pia asili na historia yetu, anayeamini katika haki ya kuabudu lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana na dini zao.

Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma bora za afya, elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama wanavyopata mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na wakurugenzi wetu.

Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata haki hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.

Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kila mtanzania ana bima ya afya na ya maisha, na kwamba bima hiyo inampatia uhakika wa kupata huduma bora za afya popote na kwa wakati anapozihitaji bila kumbagua kwa hali yake. Kwamba, itakuwa mwisho sasa, ndani ya hospitali moja, kuwa na wodi nzuri wanazolazwa ‘wateule wachache waliochangia bima ya afya’ na kuwa na wodi za ‘ilimradi’ tu wanazolazwa wengine.

Kuwa, ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na kujitegemea kwenye masoko na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani, kujitegemea kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula, kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za hasara na faida za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu. Ili tulinde thamani ya fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu?

Kuwa, ni nani kati yetu anaichukia rushwa, anachukia wakwepa kodi wa makampuni makubwa ya kimataifa yanayovuna raslimali za nchi yetu na hayalipi hata kodi tu! Kwamba, ni nani atalinda raslimali za nchi yetu bila shaka. Kwamba, ni nani kati yetu atahakikisha tunapata hisa za kutosha kutokana na uchumi wa raslimali za madini, vito, mafuta na gesi? Kwamba, ni nani kati yetu atailinda ardhi ya watanzania na kuhakikisha haivamiwi na wasaka ardhi kutoka nje ya Taifa letu, kwamba atahakikisha ardhi inabaki kutumiwa kwa faida ya wakulima na wafanyakazi wa nchi yetu?

Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kupambana na changamoto za usafiri na usafirishaji, kuwa ataweza kuongeza tija na ufanisi kwenye bandari zetu, na ataweza kufufua usafiri wa reli, ndege na meli?

Kuwa, ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania walio wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto zake, zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la watanzania?

Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi. Mtu ambaye ukimtazama kwa nje ana mvuto na analeta matumaini kwa watanzania, ambaye ukimcheki hivi unasema ‘he is just a cool guy’, lakini kwa ndani anaumia, anaungua moyo wake kwa ajili ya Tanzania yetu.

E Pluribus Unum


Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!

Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa salama kama wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka. Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu pia, na haiishii hapo tu, matatizo hayo si yangu na huyo mwenzangu tu, ni yetu sote kama jamii.

Hivyo:

kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu.

Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, Arusha, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.

Mzee Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa msaada na yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa siku ili asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu yangu.

Mama John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja wengi mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Kariakoo; akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama yangu.

Kama kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mwanangu.

Kato na Kokugonza ni wanandoa wapya, wanaishi kijijini kule pembezoni ya Katerero, Koku amepata ujauzito na amefikia kujifungua, kwa hali yake na namna mtoto alivyokaa tumboni anapaswa akajifungulie hospitali ya wilaya ili ikibidi kufanyiwa operesheni, basi afanyiwe; ikitokea uchungu umeanza ghafla na akachelewa kufika hospitali ya wilaya sababu ya miundombinu mibovu na kukosa ambulance mapema, akapoteza damu nyingi hadi umauti ukamkuta yeye na mwanae, ni jambo lenye kuuma sana, si tu kwa Kato na wanafamilia wao, bali na mimi pia linaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mdogo wangu.

Bwana Kalumanzila ni mmachinga wa nguo za mitumba mitaani. Yeye huchukua nguo zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume, akiuza anachukua kifaida kidogo kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake. Akifukuzwa barabarani na akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na analazimika kumtumikia bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na madhila anayoyapata bwana Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mjomba wangu.

Fikra hizi zinatokana, kwa kiasi kikubwa, na funzo nililopewa na babu yangu wakati nikichagua kozi ya kusoma chuo kikuu, ambapo nilipata kitendawili cha kuchagua kati ya kwenda kusoma udaktari ama sheria; aliniambia kuwa, “ni bora ukachagua kusoma udaktari maana utapata baraka za Mungu kwa kujitoa kuwasaidia watu walio na shida…” na akaendelea kusema kuwa “…kwenye maisha yako ikitokea ukapata mali ama ukawa na nafasi kubwa ya kuamua juu ya mustakabali wa maisha ya wengine, usisahau kumshukuru Mungu kwa kuwatendea yaliyo mema wenzako na Mungu atazidisha Baraka zake kwako.” Leo miaka zaidi ya 15 baadaye naona maneno yake bado yanaishi moyoni mwangu. Maisha yangu yote nimeikumbatia falsafa hii. Nimeifanya kuwa dira ya utumishi wangu kwa wenzangu na kwa ulimwengu.

Falsafa hii imenifanya nishindwe kuvumilia unyonyaji, ukandamizaji, uzembe, wizi na ubadhirifu wa baadhi ya wenzetu walioshindwa kudumu kwenye njia ya kutoa haki, uadilifu, uwajibikaji na utumishi uliotukuka.

Tamati


Ndugu wanahabari, Tarehe 4, Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha Maendeleo ya Dunia (Center for Global Development) alisema: “…Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi wangu kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.  

Kuna watu wanadhani uwepo wa mfumo wa demokrasia imara, ama mfumo unaotoa uhuru na haki kwa watu wetu, ama uwepo wa mfumo wa soko huria, ama utandawazi ni muarobaini wa kudumisha amani yetu, mimi nasema, tunahitaji zaidi ya uhuru, zaidi ya demokrasia, zaidi ya mifumo ya utandawazi, ama ya soko huria ili tudumishe amani na mshikamano wetu – tunahitaji uhuru kwenye uchumi wetu. Tunahitaji uhuru kwenye mifuko ya kila mtanzania. Uhuru wa kuchagua anachotaka kula, kuvaa ama huduma kwa ajili yake na familia yake. Tunahitaji mabadiliko ya kifikra ili kuleta mapinduzi ya uchumi tunayoyatarajia. Tunahitaji kupigana kuhakikisha kila mtanzania anajitegemea kiuchumi. Hapo ndipo tutasema sasa tuna uhuru kamili.

Mungu awabariki sana. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.


MATUKIO-MICHUZI: Dk. Kigwangala aitaka TAMISEMI kuwashirikisha Wananchi kubuni Vyanzo vya Mapato

Wednesday, May 7, 2014
MATUKIO-MICHUZI: Dk. Kigwangala aitaka TAMISEMI kuwashirikisha Wananchi kubuni Vyanzo vya Mapato

MATUKIO-MICHUZI: Dk. Kigwangala aitaka TAMISEMI kuwashirikisha Wananchi kubuni Vyanzo vya Mapato

MATUKIO-MICHUZI: Dk. Kigwangala aitaka TAMISEMI kuwashirikisha Wananchi kubuni Vyanzo vya Mapato

Hawa Siasa Kigwangalla's Tennis Training

Sunday, March 9, 2014
Saturday, December 21, 2013


Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013.

Utangulizi
Ukiitazama Nzega ya leo si ile Nzega ya Miaka ya 90 ama ile ya miaka ya 70, alipozaliwa Mbunge wetu Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), imebadilika sana, imekuwa kwa kasi sana; idadi ya watu, magari na nyumba imeongezeka sana. Utoaji wa huduma zote muhimu umezidiwa kasi na ukuaji wa mji. Changamoto zilizopo leo ni nyingi na nzito sana. Kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, shule ni chache na zinatoa elimu isiyokidhi ubora unaohitajika, viwanda hakuna  ukilinganisha na miaka ya nyuma, migodi midogo midogo iliyokuwa asili ya Nzega imefungwa na serikali, mvua zimepungua kutokana na uharibifu wa mazingira hivyo uzalishaji wa mazao ya biashara na kilimo umeathiriwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, miundombinu ya barabara imeongezeka kwa wingi haswa maeneo ya vijijini na mijini japokuwa bado ni duni na haitoshi na pia huduma za kibenki ni duni na hazijawafikia wananchi walio wengi kule vijijini. 

Pamoja na mapungufu haya Nzega inafaidika kwa kuwa kwenye nafasi nzuri kijiografia, kwamba ni makutano ya barabara kuu ziendazo Kigoma, Kagera hadi Rwanda na Burundi na ile inayokatiza kwenda Mwanza hadi Musoma na Tabora hadi Mbeya. Kama zikiunganishwa kwa lami, Nzega inaweza kuwa kituo muhimu kwa biashara. Pia nafasi yake kijiografia imefanya Nzega iwe na mchanganyiko mzuri wa watu kimakabila kiasi kwamba mchanganyiko huu unatoa fursa ya kuleta uzoefu na ujuzi mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali ambao unapafanya Nzega pawe mahala palipochangamka (vibrant and dynamic). 

Mwaka 2010, kwenye uchaguzi Mkuu, Nzega ilifanya uamuzi sahihi wa kumchagua Mbunge mwanamapinduzi, mwanamabadiliko na mpiganaji mahiri na makini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) ambaye anajitahidi kupambana na changamoto hizi usiku na mchana pasi na kukata tamaa ama kuchoka. Mafanikio ya kazi yake yanaonekana na siyo ya kutafuta. Ifuatayo ni ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) hadi kufikia Desemba 2013.


1. Hali ya Jimbo

Hali ya jimbo ni shwari; amani, upendo na usalama umetamalaki japokuwa mpaka tunaandika taarifa hii kuna malalamiko ya watu wa kijiji cha Mwanshina, ambako kuligundulika uwepo wa dhahabu hivi siku za karibuni na kupelekea wananchi kujumuika pale kuanza shughuli za uchimbaji; bahati mbaya sana wamezuiliwa na askari wa kutuliza ghasia (FFU) waliopokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega. Mazungumzo yanaendelea kujua ni kwa nini serikali imewazuia wananchi hawa ili hatma ya mgodi huu ijulikane. Pili, kuna malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Ipala ambao wanadaiwa na serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega kuvamia eneo la msitu wa hifadhi. Ufuatiliaji wa uhalali wa katazo la Mkuu wa Wilaya ya Nzega lililoambatana na uvunjifu mkubwa wa haki za wananchi, ambapo wamedumu toka kabla ya uhuru, unaendelea.  

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega imeendelea kuhudhuria shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo harusi, misiba, mahafali za wanafunzi, harambee na pia kufanya ziara za kikazi kijiji kwa kijiji kupitia ‘Operesheni Wafuate Watu’. Pia ahadi za Mbunge ama wasaidizi wake kwenye maeneo mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa – hadi sasa ni zaidi ya asilimia 95 ya ahadi zote alizotoa mbunge zimetekelezwa ukiachilia chache sana ambazo ni za siku za karibuni. Kuna ligi kubwa ya kiwilaya inayofadhiliwa na Mbunge wa Nzega inaendelea katika hatua ya robo-fainali kwenye tarafa nne za Wilaya ya Nzega – mshindi wa kwanza atapata ‘Kombe la Kigwangalla’ na fedha taslim TZS 1,000,000, wa pili atapata TZS 500,000 na wa tatu TZS 300,000. Timu zote zilizoingia nane bora zitazawadiwa seti moja ya jezi kila timu.

Mbunge wa Nzega anaendelea kupigana kuhakikisha azimio la Baraza la Madiwani la kuanzisha Kampuni ya Benki Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation Ltd - NCCCL) linatekelezwa haraka. Tunatarajia mchakato huu utafanikiwa kutokana na uwepo wa takriban TZS 2.3 bilioni zilizopatikana kutoka kampuni ya Resolute Tanzania Ltd kama ushuru wa huduma (service levy) na ambazo zitatumika kama mtaji wa kuanzia wa benki (TZS bilioni 1) na zinazobaki kwa ajili ya kununulia mashine za kuchongea barabara na kuchimbia visima zitakazomilikiwa na kuendeshwa na kampuni hizi mbili tofauti ambazo zinatarajiwa kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya Halmashauri, wanaushirika na wananchi wengine watakaopenda kununua sehemu ya hisa za makampuni haya mawili.

2. Vipaumbele Vya Jimbo
 
2.1       Mapinduzi Kwenye Sekta ya Elimu Nzega:

(i.)        Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, mpaka sasa kwa kufanya jitihada binafsi na kwa kutumia pesa za mfuko wa jimbo (milioni 43) akishirikiana na Diwani, Mhe. Ramadhani Nchimani, Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ndala, Serikali ya Kijiji cha Kampala na wananchi kwa ujumla, ameanzisha ujenzi wa shule mpya ya ‘high school’ (kidato cha tano na cha sita) pale Kampala, Ndala (Shule hii imepewa jina la Chief Ngelengi High School); ujenzi unaendelea kwa kasi hivi sasa. Shule ya pili ya High School itakuwa ni ile ya Chief Ntinginya, ambapo Mbunge wa Nzega Dkt. Hamisi Kigwangalla, kufuatia makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nzega Mjini chini ya Diwani na Mwenyekiti wake Mhe. Kizwalo Dominic waliazimia kuanzisha ujenzi wa mabweni na madarasa ya ziada ili kuipandisha hadhi shule hii iwe ya kidato cha tani na cha sita. Shule ya tatu ya High School inamaliziwa kujengwa Kata ya Puge, Tarafa ya Puge kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge (ambayo imetoa sh milioni 13), Diwani Mhe. Alex Nyassani, Serikali ya Kijiji cha Upungu na wananchi kwa ujumla (ambao walianzisha majengo hayo); pia Halmashauri ya Wilaya tayari, kwa ushawishi wa Mbunge wa Nzega na Diwani wa Kata ya Puge, imetenga fedha taslimu sh milioni 28 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule hiyo. Shule ya Nne ya High School inamaliziwa kujengwa kule Kata ya Lusu (pale Hamza Azizi Ali Sekondari) na wawekezaji wa mgodi, Kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, kufuatia jitihada za kiufuatiliaji na ushawishi wa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) na Mhe. Said Mgalula (Diwani, Lusu) wakishirikiana na wananchi, kwamba ni lazima mgodi ujenge miradi ya maendeleo ya jamii kabla haujafungwa. Ni matarajio yetu kwamba shule hizi zitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi kabla ya mwaka 2014 kuisha. Tunawaomba wananchi wote kwa ujumla, wadau mbalimbali wa maendeleo na serikali tutimize wajibu wetu, tumuunge mkono Mbunge wetu tulete mapinduzi ya kielimu Nzega. 

(ii.)              Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la PeerCorps Trust Fund ameweza kuanzisha mpango wa kusomesha watoto yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni, mfuko huu unaoitwa Hamisi Kigwangalla Scholarship Fund ulianzishwa mwaka 2008 na umeendelea kusomesha watoto na kutoa misaada mbalimbali ya kielimu. Mpaka sasa zaidi ya watoto 576 wamefaidika na mpango huu. Na kila kata kuna wanafunzi 10 kutoka katika makundi haya wanalipiwa ada chini ya mpango huu. Japokuwa mfuko unakumbana na changamoto nyingi ikiwemo kupata maombi mengi zaidi ya uwezo wa mfuko na kuna baadhi ya kata mpaka sasa mfuko haujaweza kupata fedha za kulipa ada kwa baadhi ya wanafunzi, japokuwa Mhe. Mbunge anawataka walimu, wazazi/walezi na viongozi wa Kata hizo wawe wavumilivu na kwamba ada hizo zitalipwa kabla watoto hao hawajahitimu kwa kuwa majina yao tunayo na yaliishapitishwa kufaidika na mpango huu.

(iii.)             Mwezi Januari mwaka 2014 Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, atauanza mwaka kwa kuendelea kugawa vitabu 100 vya Kiada na 50 vya ziada kwenye shule zote za Sekondari za Kata za Jimbo la Nzega pamoja na Kompyuta kwenye shule 5 za sekondari kama ambavyo amekuwa akifanya toka achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo hili.

(iv.)            Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha tamasha la utamaduni wa watu wa Nzega litakalokuwa likifanyika kila mwaka mjini Nzega. Tamasha hilo ambalo linaitwa Mtukwao Festival (www.mtukwao.org) litakuwa ni kivutio cha watu na kuleta fursa ya biashara kwa wakazi wa Nzega, na sehemu ya kuitangaza Nzega na utamaduni wake kwa wageni, tayari limepata usajili wa serikali na maandalizi yanafanyika kulizindua mnamo Julai 2014 kwa mara ya kwanza, baada ya mipango ya kulizindua Julai 2013 kama ilivyotangazwa hapo awali kushindikana.

(v.)              Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha ujenzi wa chuo binafsi mjini Nzega eneo la Uchama kitakachokuwa kinatoa wahitimu kwenye fani za Uganga, Uuguzi na Ualimu kwa ngazi za Vyeti na Stashahada ili kuongeza nguvu kazi kwenye shule za sekondari za kata, zahanati na vituo vya afya. Malengo ni kusomesha bure walau wanafunzi watano - kwenye kila kozi, wasio na uwezo, mbali na wale wanaojilipia, kwa makubaliano ya kuhakikisha wanaajiriwa kwenye wilaya ya Nzega kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Hii itaongeza idadi ya watumishi kwenye huduma muhimu kwa wananchi na pia uwepo wa chuo utakuza fursa za kiuchumi na ukuaji wa taswira ya mji wa Nzega. Tunatarajia chuo hiki kitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi mwaka 2014 Mwezi Septemba.

2.2  Kuendesha Harakati za Kupigania Haki na Usawa kwa wanaNzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na wananchi wa Nzega, madiwani na watendaji wa halmashauri ameongoza mapambano ya kudai haki za Nzega dhidi ya wawekezaji wa Mgodi wa Golden Pride Project, kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, na kufanikiwa kupata mafanikio yafuatayo: mgodi umekubali na tayari umelipa sh bilioni 2.34 kama ushuru wa huduma (service levy) kwa halmashauri ya wilaya ya Nzega, bado kuna madai ya sh bilioni 4 za ushuru wa huduma yanayoendelea kufuatiliwa, ambazo ni malimbikizo ya ushuru huo toka mgodi uanzishwe takriban miaka 14 iliyopita; amefanikiwa kuishawishi serikali kuwa wananchi waliopoteza mali zao kutokana na uharibifu uliofanywa kupisha mgodi wana haki ya kifuta jasho na sasa serikali inaungana na Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kuwabana wawekezaji waanzishe mfuko wa kuwahifadhi wananchi hao; na jambo kubwa la tatu ni kwa kutumia nguvu ya umma kushawishi wawekezaji watekeleze ahadi za kujenga miradi ya maendeleo Nzega (Kituo cha Afya Lusu, Maabara kwenye sekondari 10 n.k.). Mbunge wa Nzega ataendelea kushawishi vikao vya halmashauri na kusimamia utekelezaji wa miradi itakayowagusa wanaNzega wengi zaidi, kama vile kuanzisha benki ya jamii ya watu wa Nzega ambayo itatoa mikopo kwenye SACCOS za kila kata, kununua mitambo yetu wenyewe ya kuchimbia visima kwenye kila kijiji, kujenga soko jipya na stendi mpya kubwa ili kukuza fursa za biashara ndogondogo kwa wananchi n.k. Mhe. Mbunge amekuwa akipigana bega kwa bega na wananchi wa Kijiji cha Mwabangu kuhakikisha wanapata haki ya kupatiwa leseni yao iliyopokwa kinyemela na wajanja wachache kwa faida yao ama fidia ya ardhi ya mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Isungangwanda.

2.3  Kuwezesha Wananchi Kushiriki Shughuli Mbalimbali za Kukuza Kipato Chao: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, amefanikiwa kuleta mapinduzi ya kijani kwenye kilimo cha zao la pamba na zao la alizeti kupitia uhamasishaji wa kampuni ya MSK Solutions Ltd ambayo inatoa mbegu bora, pembejeo, zana za kilimo, elimu ya kilimo bora na uwezeshaji wa wagani vijijini, soko la uhakika la mazao hayo na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao vijijini (Imekamilisha ujenzi wa maghala kule Ndekeli (Tarafa ya Puge), Igalula (Tarafa ya Mwakalundi), Nhabala (Tarafa ya Bukene) na imeanza ujenzi wa ma-godown mapya kule Nhobola (Tarafa ya Nyasa) na Usongohala (Tarafa ya Bukene). Mafanikio ni kuongezeka kwa wakulima wa pamba kutokea wakulima 355 mwaka 2008 hadi kufikia wakulima 24,000 wa pamba mwaka 2012 na kufanya idadi ya kilo za pamba zilizovunwa kufikia takriban milioni 6 kutoka kilo 20,000 mwaka 2008. Pia idadi ya wakulima wa alizeti imeongezeka kutoka wakulima 400 mwaka jana hadi kufikia 3500 mwaka 2013.

Makampuni ya wanunuzi wa pamba yameongezeka kutoka kampuni moja ya MSK na kuwa manne hivi sasa – hali inayoleta ushindani kwenye soko na hivyo kupandisha bei zaidi kwa faida ya mkulima. Japokuwa kampuni ya MSK Solutions Ltd imeamua kuacha kuhamasisha pamba na kujikita zaidi kwenye alizeti itaendelea kukumbukwa kwa kutia chachu uhuishaji wa kilimo cha zao hili kilichokuwa kimekufa.

Mipango inaendelea kuwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya kula kutokana na alizeti ya Nzega, tayari halmashauri ya Nzega imeazimia kutenga viwanja 10 kwenye eneo maalum la kujenga viwanda. Pia Mbunge wa Nzega amewezesha wananchi kujiunga katika vikundi vya ushirika wa SACCOS vipatavyo 9 na yupo kwenye harakati za kuvijengea uwezo vifanye kazi za kukuza uchumi kama vile kilimo, mifugo ya kuku kwa kuzalisha vifaranga na mayai, na shughuli za ufundi kwa vijana. Mbunge wa Nzega amegawa mashine mbili kwenye SACCOS ya vijana nay a wazee kwa ajili ya kuangulia vifaranga. Ili kuhakikisha chama kinakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo vijijini, Mbunge wa Nzega akishirikiana na mwenzake wa Bukene wamegawa mbegu za alizeti kwenye kila kata. Pia Mbunge wa Nzega amegawa pikipiki 10 kwenye kata 10 ili kuweka urahisi zaidi wa kufikisha huduma za ushauri wa maendeleo kwa wakulima vijijini.

2.4  Ujenzi wa Miundombinu Nzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameweza kushawishi vikao mbalimbali vya maamuzi na kuhakikisha azimio la kujenga barabara za lami Nzega Mjini linafanikiwa, hivi sasa tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kutekeleza hilo kwenye mwaka wa fedha wa 2013/14; pia kufunga mataa ya kuangaza mji mzima wa Nzega. Mbunge wa Nzega pia kupitia mfuko wa Jimbo amejenga daraja korofi na lililosahaulika kwa muda mrefu la Butandula, na sasa anatafuta namna ya kuhakikisha pia daraja lingine la Nhobola nalo linajengwa, tayari ametenga sh milioni 8 za mfuko wa jimbo kutekeleza hilo.

Mradi wa barabara ya Nzega – Tabora kwa kiwango cha lami – Mbunge wa Nzega kwa kutumia nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Tabora, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali inaleta fedha za kukamilisha mradi huu ndani ya muda uliopangwa na pia kusimamia kuhakikisha barabara hiyo na nyingine za mkoa wa Tabora, zinajengwa kwa viwango vya ubora unaostahiki, na wananchi wanapata ajira na kulipwa fidia ya mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi huu.

Pia Mbunge amehakikisha barabara korofi kama za kutoka Mbagwa – Nkiniziwa, Busondo – Ndekeli, Busondo – Mwakashanhala zinaingia kwenye bajeti ya ujenzi mwaka huu wa fedha 2013/14 na kuhakikisha zinajengwa, pia barabara nyingine muhimu kama za Muhugi – Mizibaziba – Ndekeli – Ndala zinaingizwa kwenye bajeti, lengo likiwa ni kuhakikisha Nzega inakuwa na mtandao mzuri wa lami mahala pote. Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) amefanikiwa kuhakikisha mradi wa kupeleka umeme Ndala kutoka Nzega unatekelezwa kwa viwango vya ubora unaofaa, na sasa anahangaika kuhakikisha pia maeneo ya Mbogwe, Wela, Miguwa, na yale ya Usagali, Kaloleni hadi Mirambo Itobo nayo yanapata mradi wa Umeme. Tayari maombi yake yameingizwa kwenye orodha ya miradi ya Umeme Vijijini (REA Phase II) na hivyo maandalizi ya awali ya upembuzi yakinifu yataanza muda wowote kuanzia sasa. Sambamba na jitihada hizi, Mbunge amefanikiwa kuishauri na hatimaye kuishawishi halmashauri ya Nzega kuanzisha kampuni ya ujenzi (NCCCL) na kuinunulia mitambo ya kuchongea barabara, mpango ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.

2.5  Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nzega: Baada ya kutoridhishwa na namna miradi ya maji ya benki ya dunia na ile ya serikali inavyosuasua, Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameshauri na hatimaye kuishawishi Halmashauri wanunue mitambo ya kuchimba visima na kuiweka chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi Nzega (NCCCL) ili kuondoa yale matatizo kwamba mkandarasi amelipwa achimbe kisima kimoja akikosa maji basi na pesa ya serikali ndiyo imeishaliwa. Pesa za kununulia mitambo hiyo zitatokana na mapato yaliyopatikana kutokana na ushuru wa huduma uliolipwa na kampuni ya Resolute. Tukiwa na mitambo yetu tutahakikisha tunachimba kisima na maji yanapatikana kwenye kila kijiji bila shida ndipo twende kijiji kingine. Pia Mhe. Mbunge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Tabora unaanza kutekelezwa – na kwa sasa hatua ya utafiti wa awali ilishamalizika na tunatarajia upembuzi yakinifu utafanyika mwaka huu na pengine mwakani kuanza kutekelezwa, ukizingatia hii ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Jakaya Kikwete. 

2.6  Upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa Umma: Mhe. Mbunge, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameamua kuanzia mwaka 2014 ataweka ratiba maalum ya kutumia taaluma yake ya udaktari kutibu wagonjwa kwenye vituo mbali mbali vya afya Nzega. Pia ameandaa mkakati kabambe wa kuleta madaktari bingwa wanaoruka (flying doctors) kwa ajili ya kuweka kambi ya tiba maalum mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya wananchi wa Nzega. Kwa kushirikiana na madiwani wenzake wa halmashauri ya Nzega wamefanikiwa kuhakikisha vituo pamoja na nyumba za walimu zilizoanza kujengwa na wananchi vinamaliziwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi – tayari bajeti imetengwa kumalizia vituo vyote mwaka 2013/14, na anaendelea kuhamasisha vijiji vingine ambavyo havijaanza kutekeleza mpango huu vianze mara moja ili tubaki tukitafuta namna ya kupambana na chamngamoto nyingine za watumishi, vifaa na madawa.

N.B: Kuna mambo mengi yanayofanyika Nzega kwa ushawishi wa Mbunge na Madiwani, yakitekelezwa na serikali kutokana na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mwaka 2010 – 2015, lakini si yote yaliyoripotiwa hapa. 

Taarifa hii imetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega, pia inapatikana hapa www.hamisikigwangalla.com na kigwangalla.blogspot.com 

Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb.)
Leo Siku ya Jumamosi, Desemba 21, 2013.