Pichani Kigwangalla Katika Pozi...

Thursday, March 8, 2012

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari: Dkt. Hamisi Kigwangalla Akanusha Kuutaka Uwaziri


OFISI YA MBUNGE, JIMBO LA NZEGA

Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (MB)
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tunapenda kuutarifu umma kwamba Mhe. Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesikitishwa sana kupata taarifa kutoka baadhi ya vyombo vya habari kuwa anatajwa kuchochea mgomo wa madaktari. Hata siku moja hajawahi kuwa mchochezi wa mgomo huu na yeye binafsi siku zote amekuwa mstari wa mbele kusema ukweli na kuweka hadharani msimamo wake na wala siyo kuchochea kwa kificho chini kwa chini.
Pia kuna gazeti moja la kila wiki limeandika jana stori (kwenye ukurasa wake wa mbele) kuwa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla ‘anatajwa kuchochea mgomo huo kwa malengo ya kuutaka uwaziri.’ Vyombo vingi vya habari vikivutiwa na kichwa hiki cha habari vimekuwa vikimpigia simu Mhe. Mbunge kumtaka atoe ufafanuzi. Mhe. Mbunge amesikitishwa sana na taarifa zilizoandikwa kwenye gazeti hili na tayari Mwanasheria wake ameanza kujipanga kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaka gazeti hili limsafishe kwenye jamii kwa kuchapisha habari ya kumsafisha ama lipelekwe mahakamani.
Kwa taarifa hii tunakanusha ushiriki wa aina yoyote ile unaotajwa kumhusisha  Mbunge wa Nzega kwenye uchochezi ama wa namna yoyote ile inayofikirika zaidi ya msimamo ambao Mhe. Mbunge Dkt. Kigwangalla amewahi kuuweka wazi siku za nyuma kwenye mikutano ya wazi ya madaktari au kwenye vyombo vya habari. Pia ifahamike kuwa kwa kuweka wazi msimamo wake kwamba madaktari wana madai ya msingi na hivyo wasikilizwe (ambayo kwa sasa serikali ilishakiri na kuyakubali madai yao na kutamka hadharani kuwa inayafanyia kazi) haimaanishi kuwa ni uchochezi bali ni matumizi ya haki za msingi za binadamu kama zilivyoainishwa kwenye Kati ba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenye mikataba mbali mbali ya kimataifa ya haki za binadam.
Na pia tunapenda kuwataarifu wanahabari kuwa Dkt. Hamisi Kigwangalla hajahudhuria mkutano wowote ule wa madaktari uliopelekea madaktari kuazimia kugoma tena na hivyo kumhusisha na ushawishi ama uchochezi ni kupotosha umma na kuvunja sheria.  Na zaidi kufikiria kuwa madaktari nchi nzima wanaweza kugoma kwa kumsikiliza mtu mmoja tu ni kuwatukana na kuwadhalilisha kwa kuwaona hawana uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi yao, ilhali hawa ni watu makini, wenye elimu na ujuzi wa hali ya juu na wengi wao wanamshinda elimu, ujuzi na uzoefu kwa mbali sana Mhe. Mbunge Dkt. Kigwangalla. Hali kadhalika, Mhe. Dkt. Kigwangalla aliomba Ubunge na hakutarajia kuwa angepewa Uwaziri na ni wazo la kitoto kufikiria kwamba mtu mwenye busara zake na hadhi yake kama yeye angeweza kupanga mkakati wa kumn’goa Waziri yeyote Yule ili awekwe yeye, maana kwanza hana muamana na mamlaka ya uteuzi, ambayo kimsingi ndiyo yenye uamuzi wa kumteua nani na kumuondoa nani, na pia haiyumkiniki kuwa eti ‘uwe mstari wa mbele kuvumbua maovu na mapungufu ya kiutendaji ya mtu ambaye unataka atolewe kwenye nafasi ili wewe uwekwe hapo!’ Kwa namna yoyote ile kama Dkt. Kigwangalla angekuwa anaitaka nafasi ya Uwaziri asingeunga mkono madai ya madaktari. Na kwamba kama kuna mtu ana Taarifa zozote zile zinazoweza kuthibitisha kuwa amekuwa akipanga mikakati ya kutafuta Uwaziri basi aziweke wazi na Mhe. Mbunge atakuwa tayari kujivua nafasi zake zote za uongozi alizonazo.
Mhe. Mbunge anawashauri waandishi wa habari kuwa waandike taarifa ambazo wana uhakika nazo tu na wasikubali kutumiwa na makundi ya wana siasa wenye malengo ya kuchafua wenzao.

Mwisho, mara zote toka mgogoro huu baina ya madaktari na serikali uanze, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) amekuwa akishauri pande zote mbili zikutane, zijadiliane na kutafuta suluhu ya matatizo yaliyopo, na leo hii tena bado anasisitiza kuwa njia pekee sahihi na sawia ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu ni kuzungumza na kuelewana kwenye mambo ya msingi. Hii ndiyo njia pekee itakayoepusha adha kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya, ambao wao ni waathirika wasio na hatia.

Imetolewa Leo Tar 8/Machi/2012 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega.

Mrisho Gambo na Rais Paul Kagame! Bravo Komredi!

Thursday, February 9, 2012
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Africa Mashariki na Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Komredi Mrisho Gambo na viongozi wenzake wa Jumuiya hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja na Rais Paul Kagame wa Rwanda. Ni baada tu ya vikao vyao vya kazi za Jumuiya hiyo nchini Rwanda mwishoni mwa mwaka jana. Vijana ni hazina kubwa, tukidumisha ushirikiano, tukajenga urafiki na mahusiano mazuri, tutaweza kuwa chachu inayohitajika kutufikisha kwenye malengo ya Shirikisho la Africa Mashariki!

MSIMAMO WA MBUNGE WA NZEGA KUHUSU POSHO

Monday, December 12, 2011
Kufuatia kuwepo kwa mjadala mzito wa kitaifa kuhusu ongezeko la posho ya kikao (Sitting allowance) ya wabunge kama ilivyoongezwa siku za karibuni, ofisi ya Mbunge wa Nzega imelitafakari suala hili na kuona umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi wa jimbo la Nzega na watanzania kwa ujumla kuhusiana na msimamo wa Mhe. Mbunge. Tamko hili linazingatia maswali mengi kutoka kwa wapiga kura wa jimbo la Nzega na baadhi ya watanzania waliotaka kujua nini msimamo wa Dr. Hamisi Kigwangalla, MB (Nzega, CCM) kuhusu posho, hususan ongezeko hili la kutoka 70,000 hadi 200,000.

Mbunge wa Nzega ana msimamo ufuatao:

Kwamba, posho ama ujira wa mwia, ni malipo halali ya kazi ya Mbunge na kwamba ongezeko lolote litakalofuata kanuni na taratibu za haki na usawa kwa watu wote litakuwa halali.

Kwamba, Ongezeko hili kama lilivyotamkwa na Mhe. Spika Anna Makinda (MB), limekuja kutokana na ongezeko la ukali wa maisha katika mji wa Dodoma linaleta mashaka na utata mkubwa kuhusiana na uhalali wake, linaonesha usaliti wa wabunge kwa wananchi waliowachagua na linaiaibisha taasisi ya Bunge kama mtetezi wa wanyonge na mdhibiti na msimamizi mkuu wa serikali. Mbunge wa Nzega anaamini kwamba sababu hii inawakimbiza wabunge mbali zaidi na wananchi na kwamba ni kweli kuna mfumuko mkubwa wa bei lakini hauwagusi wabunge tu pekee yao, unamgusa kila mtanzania, na kama ofisi ya Rais inaona umuhimu wa kuboresha hali ya maisha ya wabunge, basi ingewapandishia mishahara yao, ingewaongezea mafuta ya gari kwa ajili ya kufanyia kazi zao, ingeboresha mfuko wa jimbo, ingeboresha ofisi zao n.k. Kwa hakika kabisa, kwa sababu zilizotolewa na Mhe. Spika, posho iliyopaswa kuongezwa siyo posho ya kikao bali ni posho ya kujikimu. Na hata kama Mhe. Spika alikuwa na nia ya kuongeza posho ya kikao, basi kwa vyovyote vile sababu isingekuwa hii ya ukali wa maisha mjini Dodoma, maana hauongezeki kwa wabunge peke yao tu!

Kwamba, kwa kuwa sababu za kuongezwa kwa posho ya kikao haziendani na malengo ya uwepo wa posho hiyo, basi wabunge wote waungane mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Kabwe, Mbunge wa Bumbuli Mhe. January Makamba na Mbunge wa Nzega Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Nzega) waikatae posho hii ili kuwatendea haki watanzania wanaohangaika kutafuta mkate wao wa kila siku. Kuna madaktari wanakesha usiku kucha na wanalipwa posho ya on call allowance ya TZS 10,000 tu, kumlipa Mbunge posho ya 200,000 haijengi mazingira ya usawa ya kuugawana umaskini wa nchi yetu.

Kwamba, ili kupunguza visingizio vya wabunge kudai maslahi makubwa zaidi kwa kuwa wanaombwa sana amisaada na wapiga kura wao, ofisi ya Bunge ianzishe kitengo cha kutoa elimu kwa umma kuhusu kazi na majukumu ya Mbunge ili kuwaelimisha wananchi kwamba kusaidia matatizo binafsi siyo kazi yao na hivyo wasihukumiwe kwa kutokutoa misaada bali kwa kuisimamia serikali ipasavyo.


Tamko hili limetolewa leo Tar 12/12/2011 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB).

Mapinduzi ya Kijani (Pamba) Yamefanikiwa Nzega!

Tuesday, November 8, 2011
Katika hali ya kutia moyo, wilaya ya Nzega imefanikiwa kufufua kilimo cha Pamba. Zao hili la biashara lililokuwa limepotea kabisa wilayani hapa sasa limerudi upya tena, japokuwa si kwa kufikia kiwango cha zamani lakini mwanga wa matumaini unaangaza kila kona. Wilaya ya Nzega iliacha kulima pamba takriban miaka 12 iliyopita kufuatia kuanguka kwa utaratibu mbovu wa ushirika uliokuwepo. Tatizo hili halikuikumba Nzega peke yake bali ukanda wote wa Western Cotton Growing Area (WCGA) (yaani mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kigoma, Singida, Kagera n.k). Ushirika ulikuwa ukinunua pamba kwa mkopo na kulipa wakulima pesa yao kwa awamu. Mwaka 1990 wakulima wote hawakulipwa pesa ya malipo yao ya awamu ya pili. Hii iliwakatisha sana tamaa na wengi wao waliacha kulima pamba msimu wa kilimo uliofuatia. Mwaka 1991, bei za pamba zilizidi kuanguka kwenye soko la dunia na hivyo kusababisha ushirika tena kushindwa kununua pamba ya wakulima vizuri ipasavyo, na mzunguuko huu ulipelekea wakulima wengi zaidi kususa kulima pamba misimu iliyofuatia. Mfumo wa masoko ulipoboreshwa kwa kuingia kwa soko huria hapo baadaye, sehemu nyingine zilirudia kilimo cha pamba lakini Nzega ilikoma kabisa na pamba ikabaki historia! Na huu ulikuwa mwanzo wa kushamiri wa kwa umaskini wilayani Nzega. Maana wakulima walilazimika kuuza chakula ili wapate hela badala ya kuuza mazao ya biashara.

Kampuni ya MSK Solutions Ltd ikishirikiana na Serikali wilaya ya Nzega na Kampuni ya Rural Livelihood Development Company (RLDC) wamejifunga mikanda na kwa pamoja wamefanikiwa kuleta mapinduzi ya ukweli ya kijani. Pamba imerudi tena Nzega, imerudi kwa kasi ya ajabu ambayo haikutegemewa. Kwa pamoja wadau hawa wamekuwa wakiendesha mradi wa Nzega Cotton Development Project (NZECODEP) ambao unafadhiliwa kwa pamoja na wadau wawili, MSK Solutions Ltd na RLDC.

Mradi huu umeweza kufanikiwa kwa sababu zifuatazo, kwanza umewahakikishia wakulima soko la uhakika na bei nzuri zaidi ya pamba yao. Pili, mradi unahakikisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo cha pamba karibu na wakulima na kwa bei nzuri zaidi. Tatu, wakulima wanahakikishiwa ushauri wa kitaalamu karibu zaidi kwa kuwa mradi unawawezesha posho kidogo mabwana shamba ili kuwatia morali zaidi wa kutoa huduma za ugani.

Katika uhamasishaji huu, ujumbe mahsusi unaowafikia wakulima ni pamoja na uhakika wa vitu vyote hivi na pia maelezo yanayotoa cost-benefit analysis ya kilimo cha pamba ukilinganisha na mazao mengine na kwamba pamba haikuja kufuta kilimo cha mazao mengine bali kuhakikisha mkulima anakuwa na zao la mbadala endapo ikitokea amekosa mavuno ya kutosha ya mazao ya chakula ama mengine ya biashara atakayokuwa amelima. Pia wakulima wanaeleimishwa kuwa pamba inastahimili ukame ukilinganisha na mahindi na mpunga na hivyo kama mkulima akikosa hayo mazao mengine yote na akapata pamba, atauza atapata hela na kwenda kununua chakula. Na kama akipata mazao mengine, basi atafanya mambo mengine kwa kutumia hela itokanayo na pamba.

Kutoka kilo 20,000 Mwaka wa Kwanza, hadi 350,000 na sasa Kilo 982,000! Mbali na kukuza kipato cha mkulima mmoja mmoja, pamba itakuwa ni chanzo kipya kikubwa cha mapato ya halmashauri ya wilaya ya Nzega kupitia ushuru wa mazao (district cess) na hivyo kufanikisha miradi mbali ya maendeleo kama mabarabara, shule, zahanati n.k. Pia faida nyingine ni pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha na hivyo kutia chachu sekta nyingine za maendeleo na huduma wilayani hapa. Pia kushamiri kutaleta viwanda wilayani hapa. Maendeleo haya ni endelevu na yanagusa watu wengi ukilinganisha na uwepo wa mgodi mkubwa wa uchimbali dhahabu ambapo ikiisha ndiyo basi tena.

Kikwazo kikubwa kinachoukumba mradi, pamoja na mambo mengine, ni propaganda za kisiasa zinazofanywa na wanasiasa kwa vile tu harakati za kufufua zao la pamba Nzega zinafanywa na kampuni ya MSK Solutions Ltd ambamo Mbunge wa Jimbo la Nzega ana hisa.


Makala hii imeandaliwa na Ndg. Kumotola L. Kumotola, Afisa Mahusiano, Uratibu na Itifaki - Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega akishirikiana na Ndg. Hassan Jaha, Mratibu wa Mradi wa NZECODEP, MSK Solutions Ltd, Nzega.

Volunteers at Work!

Volunteers at Work!

Monday, November 7, 2011