Dk. Hamisi Kigwangalla atangaza rasmi kwa waandishi wa habari nia ya kuwania ubunge Nzega

Wednesday, March 10, 2010
Tarehe 10 Machi 2010

Dk. Hamisi A. Kigwangalla (MD, MPH, MBA) ni kijana msomi mwenye umri wa miaka 35, mwenye digrii tatu na aliyebobea katika taaluma ya afya ya jamii na utawala wa biashara. Dk. Kigwangalla ni kijana wa kitanzania anayeamini kwenye fikra mbadala na za kisasa lakini anaamini katika misingi iliyowekwa na wazee waasisi wa TANU na ASP. Alihitimu masomo ya digrii ya udaktari wa tiba ya binadamu (yaani Doctor of Medicine, MD) kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam mnamo mwaka 2004. Pia ni muhitimu wa digrii mbili za uzamili; moja ambayo ni Masters in Public Health Sciences (major: Safety promotion) – kwa Kiswahili inatafsirika kama digrii ya uzamili katika sayansi ya afya ya jamii (amebobea kwenye kuhamasisha usalama), alihitimu mwaka 2007 kutoka chuo kikuu cha Karolinska Institutet, Stockholm, Sweden, na ya pili ni Masters in Business Administration (major: organization and leadership) – ambayo kwa Kiswahili inatafsirika kama digrii ya uzamili katika utawala wa biashara (amebobea kwenye mambo ya uongozi na miundo ya mashirika) aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Blekinge (Blekinge Institute of Technology), pia kilichopo Sweden, mjini Ronneby.

Dk. Kigwangalla anaamini katika kutoa mchango wake juu ya maendeleo ya jamii kuliko kusubiri atafanyiwa nini na Taifa lake. (kama alivyowahi kusema raisi wa zamani wa marekani Bw. Abraham Lincoln).

Dk. Kigwangalla ni mtu anayefanya kazi zake kwa umakini, spidi na maarifa, na kuzingatia misingi ya maendeleo na uwajibikaji. Ni mwanapinduzi anayeamini mapinduzi ya Uchumi wa Tanzania yako karibu, na kwamba tutaendelea tu kama tutabadilisha fikra zetu (change of mindset). Anaiona Tanzania kama ni nchi yenye fursa nyingi na kwamba ni nchi iliyokaa vizuri na tayari tayari kuyapokea mapinduzi ya kiuchumi (Tanzania ni miongoni mwa emerging economies in Africa). Anaamini kuna haja ya kuwapa nafasi watu ambao wanayaona maisha kwa macho tofauti, badala ya kuangalia matatizo tu wanaangalia fursa ziko wapi ndani ya hayo matatizo. Bila kubadilisha mtazamo wetu hatutoweza kusonga mbele, itakuwa ni sawa na kujaribu kukimbiza jahazi nchi kavu!

Yeye anasema “maadui wa Tanzania wanajulikana na njia za kupambana nao zinajulikana – maadui hawa wapo toka nchi hii ianze, sasa kama maadui tunawajua na silaha za kuwamaliza tunazo, tunangoja nini sasa?....” Hapa anaongelea Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Yeye anaona kuna ya haja ya viongozi mahiri na wenye nia thabiti ya kuwatumikia watu wajitokeze popote walipo na waje kuongeza nguvu kwa taifa letu ili tuweze kupambana na maadui hawa. Anasema, “tatizo kubwa ni kwamba watu wengi wanaogopa kuingia kwenye ‘mainstream politics’ kwa kuwa hawajiamini katika uwezo wao wa kukabili mikiki mikiki inayoendana na siasa, wengine wanafikiri siasa ina wenyewe, wengine wanasubiri wastaafu ndiyo waingie kwenye siasa (hivi utaweza kutawatumikia watu vizuri wakati ukiwa umechoka?). vijana wengi wasomi na wachapakazi wazuri kabisa wanasahau kwamba siasa na mfumo wa maisha yao ya kila siku na kwamba hadi majumbani mwao wanafanya siasa– wengine ni watu makini sana na wangeweza kuchangia mengi kwenye kuleta maendeleo ya taifa letu, ……tatizo kubwa ni kwamba watanzania ni wazuri sana wa kusema na kupanga lakini ni wavivu wa kutekeleza, hivyo tunahitaji viongozi watendaji kwenye kila sekta, popote walipo wafanye mabadiliko! Tuache kuongea na kupanga tu, sasa tuanze kuwa mabingwa wa utekelezaji!” “….pia viongozi wengi si wabunifu, wachovu wa kufikiri na hivyo hata utendaji na usimamizi wao wa sera nzuri zilizowekwa unakuwa mbovu”

Dk. Kigwangalla anasema kwa kuyaangalia yote haya na ametafakari kwa umakini na kujipima uwezo wake, ameonelea aanze kwa vitendo ili awe chachu ya mabadiliko kwa watu wa Nzega, ambako ndipo alipozaliwa. Anasema, “jamani Charity begins at home na ndo maana nimeamua kuwania ubunge wa Nzega ili nishiriki kikamilifu na kwa ukaribu zaidi pamoja na wana Nzega wenzangu katika kuzikabili changamoto za maendeleo katika jimbo la Nzega kwa spidi na kwa ubunifu wa hali ya juu…..maana mimi kila nikiiangalia Nzega sioni matatizo bali naona fursa tu za kuleta mabadiliko, nashindwa kuelewa kwa nini sasa watu wakose mahali pa kunyweshea mifugo yao wakati mungu ametujaalia mabonde na mito ya kumwaga kabisa? Siku moja nilipita kijiji cha Nata, ambacho kipo karibu kabisa na bonde la mto Manonga, nilishangaa na kusikitika sana kuwaona akinamama wakifuata maji mbali kabisa na miji yao, takriban kilomita tano au saba! Eti kijijini hakuna visima, kweli?” Nikafuatilia sana suala hili nikagundua kuwa tatizo haliishii hapo tu, wakazi wa vijiji vya sehemu moja huwa wanalazimika wakati wa kiangazi kupeleka mifugo yao kuwekeza kwenye vijiji vilivyo karibu na mto, kweli tumeshindwa hata kutega maji kwa ajili ya mifugo yetu?”

Japokuwa Nzega ina fursa nyingi, na ni mojawapo ya wilaya kongwe, kasi yake ya maendeleo haiendani na fursa zilizopo. Nzega ilikuwa ni wilaya ya mbele kimaendeleo tangu miaka ya 60, mzunguko wa hela ulikuwa mkubwa, miundo mbinu ilikuwa na hali nzuri zaidi ya sasa ukilinganisha na wilaya zingine, lakini kasi yake ya ukuaji hairidhishi na shughuli za uchumi na maendeleo zinazidi kuzorota siku hadi siku.

Dk. Kigwangalla anasema “kasi ya maendeleo ya Nzega hairidhishi na matatizo mengi ya msingi hayapatiwi ufumbuzi…kero zinazowakabili watu wa Nzega ni nyingi na zinahitaji mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kubuni miradi mbalimbali itakayoweza kuharakisha maendeleo ya Nzega. Wananchi wa Nzega wanahitaji kuwa na kiongozi mwenye kupenda maendeleo, mwenye fikra mbadala na mwenye uwezo wa kuanzisha msukumo mpya wa kasi ya maendeleo kulingana na kero zao na vipaumbele vya kisera na kimikakati vya kiwilaya na kitaifa.” “Kuna mambo mengi hayajakamilika na utekelezaji wake unalegalega – nyumba za walimu na baadhi ya vyumba vya madarasa kwenye mashule ya kata havijakamilika, waalimu hawatoshi kwenye shule zetu mpya; huduma duni za ugani kwa wakulima, hali ya miundo mbinu vijijini bado hairidhishi.”

Mke wangu siku moja aliniuliza swali, maana yeye huwa muoga sana na hapendi sana mikakati yangu ya kuingia kwenye siasa, “hivi kwa ni haswa unataka kugombea Ubunge? Si ufanye tu mambo yako?” Na mimi sikusita kumjibu kuwa: “Ninataka kugombea Ubunge kwa kuwa ni uwezo mkubwa wa kuwatumikia watu, nina wito na ni haki yangu ya msingi kikatiba”. Alivyo kin’gang’anizi akaendelea “kwa nini lazima wewe tu, si uwaache wengine wafanye?” Nikamwambia: “mimi naona kama mambo hayaendi inavyopaswa na ninajiona kama ninaweza kuyafanya kwa ubora zaidi, sasa kwa nini nisitoe mchango wangu kwa taifa? Nikamuuliza wewe ni daktari, umeshuhudia akinamama wangapi wakipoteza maisha kwa kukosa huduma, wengine wakizalia njiani bila msaada wowote wa huduma? Je haya mambo kama yakipata watu wenye nia ya kweli ya kubadili mambo hayatendeki?” akanyamaza. Kwisha kazi yake. “mimi nikiangalia mjane aliyeachwa na babu yangu mdogo pale Inagana, Magengati naona kama anahitaji msaada kidogo tu aweze kumudu kuendesha maisha yake. Ndugu zangu wanaolima vitunguu kule Milambo-Itobo hawahitaji vitu vikubwa sana, wanahitaji wapate mtu wa kuwatetea na kuwaongoza kidogo tu waweze kupata faida zaidi kwenye shughuli zao na waboreshe zaidi maisha yao. Ni watu kama hawa wanaonifanya nijisikie wito zaidi wa kwenda kushirikiana nao kuleta mabadiliko katika maisha yao na familia zao, naona kama wamewekwa pembezoni na hawana mtetezi!

Mzee wangu Mzee Masanilo ni mkulima stadi na mahiri sana, hahitaji vitu vikubwa wala vya kutisha, yeye anahitaji soko la uhakika tu la mazao yake ya pamba, alizeti na mpunga. Wadogo zangu, akina Fatu na Ibra wao wanahitaji uhakika wa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na au vyuo vya kati (vya kutoa Diploma na Vyeti) vya kuwapa ujuzi na maarifa, wanahitaji madaraja ya kupandia chuo kikuu, wanahitaji hizi fursa ziwepo. Zote hizi ni kero, na tunazijua, je ni lini tutazifanyia kazi? Kwa nini tunashindwa? Ninajiona kama nina majibu ya maswali yote haya na ninadhani naweza kuyafanyia kazi ipasavyo.

Leo hii nimeamua kuiweka nia yangu hadharani kabisa kuwa kwa ridhaa yangu na matakwa yangu binafsi, nafsi yangu inanituma na hapa basi natangaza rasmi nia yangu ya kuvuta fomu kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), pindi wakati utakapowadia. Naomba mungu aniongoze. Amina.

Dk. Hamisi Kigwangalla’s Contacts are:

0715636963
0754636963
0784636963

Email: hkigwangalla@gmail.com

Website: www.peercorpstrust.org