Mwanasiasa machachari na chipukizi, Dk. Hamisi A. Kigwangalla, ambaye ni mkazi na mzaliwa wa wilayani Nzega, Tabora anajipanga kutangaza rasmi nia yake ya kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia chama cha mapinduzi.
Dk. Kigwangalla, ambaye anajiweka kama ni mtu mwenye kupenda maendeleo, anayeona mbali na mwenye nia ya dhati ya kuwaendeleza wanaNzega na watanzania wenzake walio maskini zaidi, alikuwa na haya ya kusema: "...mungu akinijaalia ninapanga kutangaza rasmi nia yangu ya kuwania ubunge wa jimbo la Nzega kupitia CCM kwenye uchaguzi ujao (yaani wa Mwaka 2010), hili linakuja sana baada ya kufuatwa na kuombwa na watu mbalimbali wa rika tofauti tofauti....nimejifikiria sana na ninadhani kama kila kitu kitaenda sawa naweza kufuata ushauri wa watu, kwa sasa hivi bado nashauriana na familia yangu, ndugu, jamaa na marafiki, wakiona nisonge mbele basi ninapanga kutangaza hadharani kupitia vyombo vya habari mnamo wiki ya kuanzia Machi 08, 2010."
Dk. Kigwangalla ni mwanaharakati, mkulima na mjasiriamali kijana aliyezaliwa wilayani Nzega miaka takriban 35 iliyopita na ni msomi wa digrii tatu ikiwemo ya kwanza ya udaktari wa tiba za binadamu (Doctor of Medicine), ya afya ya jamii (MPH) na ya utawala wa biashara (MBA). Kwa sasa anajishughulisha na kilimo na mambo ya harakati za kuleta maendeleo kwa kinamama, watoto na makundi mengine yaliyo katika hatari zaidi.