Kuoa Uchagani kuna raha zake!

Friday, May 21, 2010
wikiendi iliyopita mke wangu Mama Sheila na Mimi tulitembelewa na wageni. Wageni hao, wakwe zangu na mashemeji walituletea supu (mbuzi wawili) ya mzazi (mama Sheila) kwa ajili ya kunywa na kuleta maziwa ya kutosha. Hii ni baada ya kufurahishwa na ujio wa Mtoto wetu wa pili tuliyempa jina la Hawwah Kigwangalla. Hawwah ni jina la mama mkwe wangu.

Dk. Hamisi Kigwangalla na Kilimo Kwanza Nzega: Kilimo cha Pamba Kinawezekana!

Jitihada za kufufua kilimo cha zao la biashara la pamba Nzega, Tabora zinaelekea kuzaa matunda baada ya mwanga wa mavuno mazuri kuonekana. Zifuatazo ni picha zilizopigwa na Mkurugenzi wa Mradi wa Kuendeleza Pamba Nzega - yaani Nzega Cotton Development Project (NZECODEP), Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa na wadau wengine wa wilayani Nzega wakati wa tathmini ya mradi inayoendelea kule wilayani Nzega. Mpaka sasa dalili zinaonyesha kuwa kilimo cha pamba kitaleta mapinduzi makubwa ya uchumi wa mkulima Nzega, baada ya mradi kuwawezesha wananzega kutegemea kupata wastani wa kilo 1200 kwa ekari moja; kiwango kikubwa kuliko wastani wa taifa wa kilogramu 400 tu kwa ekari. Hii ni kutokana na uhamasishaji mkubwa uliofanywa na wafanyakazi mahiri na waliojitoa wa kampuni ya MSK Solutions Ltd, ambaye ni mmiliki wa mradi huo. Mradi huu unahamasisha matumizi kidogo ya madawa ya kuua wadudu na matumizi ya samadi au mboji pekee (kwa ajili ya kutunza ardhi) badala ya mbolea za kisasa za chumvichumvi. Hii inaifanya pamba ya Nzega iwe na hadhi ya pamba hai (organic cotton). Matumizi madogo ya dawa yanawezeshwa na kutumika kwa mfumo wa zao mtego (Integrated Pest Management, IPM) na zao linalotumika Nzega ni alizeti, ambayo inawawezesha wakulima pia kuvuna na kujipatia mafuta kwa ajili ya kula na mashudu kwa ajili ya mifugo yao.

Mradi unaelekea katika ujenzi wa kiwanda cha kuchambua pamba (cotton ginnery) mjini Nzega, kilimo cha mkataba kwa mwaka wa kilimo wa 2010/2011 ambao ni mwaka wa pili wa mradi na pia kutanuka zaidi na kuunganisha wilaya jirani ya Uyui.

Hizi ni harakati za mashirika na watu binafsi kujitokeza kuunga mkono azimio la Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete la Kilimo Kwanza kwa vitendo. Na tayari mafanikio yameshaonekana. Ushirikiano huu utawaletea manufaa makubwa wakulima na taifa kwa ujumla. Wengine wengi zaidi tujitokeze. TUKISHIRIKIANA TUTAJENGA UCHUMI IMARA!