Saturday, December 21, 2013


Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013.

Utangulizi
Ukiitazama Nzega ya leo si ile Nzega ya Miaka ya 90 ama ile ya miaka ya 70, alipozaliwa Mbunge wetu Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), imebadilika sana, imekuwa kwa kasi sana; idadi ya watu, magari na nyumba imeongezeka sana. Utoaji wa huduma zote muhimu umezidiwa kasi na ukuaji wa mji. Changamoto zilizopo leo ni nyingi na nzito sana. Kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, shule ni chache na zinatoa elimu isiyokidhi ubora unaohitajika, viwanda hakuna  ukilinganisha na miaka ya nyuma, migodi midogo midogo iliyokuwa asili ya Nzega imefungwa na serikali, mvua zimepungua kutokana na uharibifu wa mazingira hivyo uzalishaji wa mazao ya biashara na kilimo umeathiriwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, miundombinu ya barabara imeongezeka kwa wingi haswa maeneo ya vijijini na mijini japokuwa bado ni duni na haitoshi na pia huduma za kibenki ni duni na hazijawafikia wananchi walio wengi kule vijijini. 

Pamoja na mapungufu haya Nzega inafaidika kwa kuwa kwenye nafasi nzuri kijiografia, kwamba ni makutano ya barabara kuu ziendazo Kigoma, Kagera hadi Rwanda na Burundi na ile inayokatiza kwenda Mwanza hadi Musoma na Tabora hadi Mbeya. Kama zikiunganishwa kwa lami, Nzega inaweza kuwa kituo muhimu kwa biashara. Pia nafasi yake kijiografia imefanya Nzega iwe na mchanganyiko mzuri wa watu kimakabila kiasi kwamba mchanganyiko huu unatoa fursa ya kuleta uzoefu na ujuzi mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali ambao unapafanya Nzega pawe mahala palipochangamka (vibrant and dynamic). 

Mwaka 2010, kwenye uchaguzi Mkuu, Nzega ilifanya uamuzi sahihi wa kumchagua Mbunge mwanamapinduzi, mwanamabadiliko na mpiganaji mahiri na makini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) ambaye anajitahidi kupambana na changamoto hizi usiku na mchana pasi na kukata tamaa ama kuchoka. Mafanikio ya kazi yake yanaonekana na siyo ya kutafuta. Ifuatayo ni ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) hadi kufikia Desemba 2013.


1. Hali ya Jimbo

Hali ya jimbo ni shwari; amani, upendo na usalama umetamalaki japokuwa mpaka tunaandika taarifa hii kuna malalamiko ya watu wa kijiji cha Mwanshina, ambako kuligundulika uwepo wa dhahabu hivi siku za karibuni na kupelekea wananchi kujumuika pale kuanza shughuli za uchimbaji; bahati mbaya sana wamezuiliwa na askari wa kutuliza ghasia (FFU) waliopokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega. Mazungumzo yanaendelea kujua ni kwa nini serikali imewazuia wananchi hawa ili hatma ya mgodi huu ijulikane. Pili, kuna malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Ipala ambao wanadaiwa na serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega kuvamia eneo la msitu wa hifadhi. Ufuatiliaji wa uhalali wa katazo la Mkuu wa Wilaya ya Nzega lililoambatana na uvunjifu mkubwa wa haki za wananchi, ambapo wamedumu toka kabla ya uhuru, unaendelea.  

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega imeendelea kuhudhuria shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo harusi, misiba, mahafali za wanafunzi, harambee na pia kufanya ziara za kikazi kijiji kwa kijiji kupitia ‘Operesheni Wafuate Watu’. Pia ahadi za Mbunge ama wasaidizi wake kwenye maeneo mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa – hadi sasa ni zaidi ya asilimia 95 ya ahadi zote alizotoa mbunge zimetekelezwa ukiachilia chache sana ambazo ni za siku za karibuni. Kuna ligi kubwa ya kiwilaya inayofadhiliwa na Mbunge wa Nzega inaendelea katika hatua ya robo-fainali kwenye tarafa nne za Wilaya ya Nzega – mshindi wa kwanza atapata ‘Kombe la Kigwangalla’ na fedha taslim TZS 1,000,000, wa pili atapata TZS 500,000 na wa tatu TZS 300,000. Timu zote zilizoingia nane bora zitazawadiwa seti moja ya jezi kila timu.

Mbunge wa Nzega anaendelea kupigana kuhakikisha azimio la Baraza la Madiwani la kuanzisha Kampuni ya Benki Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation Ltd - NCCCL) linatekelezwa haraka. Tunatarajia mchakato huu utafanikiwa kutokana na uwepo wa takriban TZS 2.3 bilioni zilizopatikana kutoka kampuni ya Resolute Tanzania Ltd kama ushuru wa huduma (service levy) na ambazo zitatumika kama mtaji wa kuanzia wa benki (TZS bilioni 1) na zinazobaki kwa ajili ya kununulia mashine za kuchongea barabara na kuchimbia visima zitakazomilikiwa na kuendeshwa na kampuni hizi mbili tofauti ambazo zinatarajiwa kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya Halmashauri, wanaushirika na wananchi wengine watakaopenda kununua sehemu ya hisa za makampuni haya mawili.

2. Vipaumbele Vya Jimbo
 
2.1       Mapinduzi Kwenye Sekta ya Elimu Nzega:

(i.)        Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, mpaka sasa kwa kufanya jitihada binafsi na kwa kutumia pesa za mfuko wa jimbo (milioni 43) akishirikiana na Diwani, Mhe. Ramadhani Nchimani, Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ndala, Serikali ya Kijiji cha Kampala na wananchi kwa ujumla, ameanzisha ujenzi wa shule mpya ya ‘high school’ (kidato cha tano na cha sita) pale Kampala, Ndala (Shule hii imepewa jina la Chief Ngelengi High School); ujenzi unaendelea kwa kasi hivi sasa. Shule ya pili ya High School itakuwa ni ile ya Chief Ntinginya, ambapo Mbunge wa Nzega Dkt. Hamisi Kigwangalla, kufuatia makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nzega Mjini chini ya Diwani na Mwenyekiti wake Mhe. Kizwalo Dominic waliazimia kuanzisha ujenzi wa mabweni na madarasa ya ziada ili kuipandisha hadhi shule hii iwe ya kidato cha tani na cha sita. Shule ya tatu ya High School inamaliziwa kujengwa Kata ya Puge, Tarafa ya Puge kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge (ambayo imetoa sh milioni 13), Diwani Mhe. Alex Nyassani, Serikali ya Kijiji cha Upungu na wananchi kwa ujumla (ambao walianzisha majengo hayo); pia Halmashauri ya Wilaya tayari, kwa ushawishi wa Mbunge wa Nzega na Diwani wa Kata ya Puge, imetenga fedha taslimu sh milioni 28 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule hiyo. Shule ya Nne ya High School inamaliziwa kujengwa kule Kata ya Lusu (pale Hamza Azizi Ali Sekondari) na wawekezaji wa mgodi, Kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, kufuatia jitihada za kiufuatiliaji na ushawishi wa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) na Mhe. Said Mgalula (Diwani, Lusu) wakishirikiana na wananchi, kwamba ni lazima mgodi ujenge miradi ya maendeleo ya jamii kabla haujafungwa. Ni matarajio yetu kwamba shule hizi zitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi kabla ya mwaka 2014 kuisha. Tunawaomba wananchi wote kwa ujumla, wadau mbalimbali wa maendeleo na serikali tutimize wajibu wetu, tumuunge mkono Mbunge wetu tulete mapinduzi ya kielimu Nzega. 

(ii.)              Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la PeerCorps Trust Fund ameweza kuanzisha mpango wa kusomesha watoto yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni, mfuko huu unaoitwa Hamisi Kigwangalla Scholarship Fund ulianzishwa mwaka 2008 na umeendelea kusomesha watoto na kutoa misaada mbalimbali ya kielimu. Mpaka sasa zaidi ya watoto 576 wamefaidika na mpango huu. Na kila kata kuna wanafunzi 10 kutoka katika makundi haya wanalipiwa ada chini ya mpango huu. Japokuwa mfuko unakumbana na changamoto nyingi ikiwemo kupata maombi mengi zaidi ya uwezo wa mfuko na kuna baadhi ya kata mpaka sasa mfuko haujaweza kupata fedha za kulipa ada kwa baadhi ya wanafunzi, japokuwa Mhe. Mbunge anawataka walimu, wazazi/walezi na viongozi wa Kata hizo wawe wavumilivu na kwamba ada hizo zitalipwa kabla watoto hao hawajahitimu kwa kuwa majina yao tunayo na yaliishapitishwa kufaidika na mpango huu.

(iii.)             Mwezi Januari mwaka 2014 Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, atauanza mwaka kwa kuendelea kugawa vitabu 100 vya Kiada na 50 vya ziada kwenye shule zote za Sekondari za Kata za Jimbo la Nzega pamoja na Kompyuta kwenye shule 5 za sekondari kama ambavyo amekuwa akifanya toka achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo hili.

(iv.)            Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha tamasha la utamaduni wa watu wa Nzega litakalokuwa likifanyika kila mwaka mjini Nzega. Tamasha hilo ambalo linaitwa Mtukwao Festival (www.mtukwao.org) litakuwa ni kivutio cha watu na kuleta fursa ya biashara kwa wakazi wa Nzega, na sehemu ya kuitangaza Nzega na utamaduni wake kwa wageni, tayari limepata usajili wa serikali na maandalizi yanafanyika kulizindua mnamo Julai 2014 kwa mara ya kwanza, baada ya mipango ya kulizindua Julai 2013 kama ilivyotangazwa hapo awali kushindikana.

(v.)              Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha ujenzi wa chuo binafsi mjini Nzega eneo la Uchama kitakachokuwa kinatoa wahitimu kwenye fani za Uganga, Uuguzi na Ualimu kwa ngazi za Vyeti na Stashahada ili kuongeza nguvu kazi kwenye shule za sekondari za kata, zahanati na vituo vya afya. Malengo ni kusomesha bure walau wanafunzi watano - kwenye kila kozi, wasio na uwezo, mbali na wale wanaojilipia, kwa makubaliano ya kuhakikisha wanaajiriwa kwenye wilaya ya Nzega kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Hii itaongeza idadi ya watumishi kwenye huduma muhimu kwa wananchi na pia uwepo wa chuo utakuza fursa za kiuchumi na ukuaji wa taswira ya mji wa Nzega. Tunatarajia chuo hiki kitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi mwaka 2014 Mwezi Septemba.

2.2  Kuendesha Harakati za Kupigania Haki na Usawa kwa wanaNzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na wananchi wa Nzega, madiwani na watendaji wa halmashauri ameongoza mapambano ya kudai haki za Nzega dhidi ya wawekezaji wa Mgodi wa Golden Pride Project, kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, na kufanikiwa kupata mafanikio yafuatayo: mgodi umekubali na tayari umelipa sh bilioni 2.34 kama ushuru wa huduma (service levy) kwa halmashauri ya wilaya ya Nzega, bado kuna madai ya sh bilioni 4 za ushuru wa huduma yanayoendelea kufuatiliwa, ambazo ni malimbikizo ya ushuru huo toka mgodi uanzishwe takriban miaka 14 iliyopita; amefanikiwa kuishawishi serikali kuwa wananchi waliopoteza mali zao kutokana na uharibifu uliofanywa kupisha mgodi wana haki ya kifuta jasho na sasa serikali inaungana na Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kuwabana wawekezaji waanzishe mfuko wa kuwahifadhi wananchi hao; na jambo kubwa la tatu ni kwa kutumia nguvu ya umma kushawishi wawekezaji watekeleze ahadi za kujenga miradi ya maendeleo Nzega (Kituo cha Afya Lusu, Maabara kwenye sekondari 10 n.k.). Mbunge wa Nzega ataendelea kushawishi vikao vya halmashauri na kusimamia utekelezaji wa miradi itakayowagusa wanaNzega wengi zaidi, kama vile kuanzisha benki ya jamii ya watu wa Nzega ambayo itatoa mikopo kwenye SACCOS za kila kata, kununua mitambo yetu wenyewe ya kuchimbia visima kwenye kila kijiji, kujenga soko jipya na stendi mpya kubwa ili kukuza fursa za biashara ndogondogo kwa wananchi n.k. Mhe. Mbunge amekuwa akipigana bega kwa bega na wananchi wa Kijiji cha Mwabangu kuhakikisha wanapata haki ya kupatiwa leseni yao iliyopokwa kinyemela na wajanja wachache kwa faida yao ama fidia ya ardhi ya mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Isungangwanda.

2.3  Kuwezesha Wananchi Kushiriki Shughuli Mbalimbali za Kukuza Kipato Chao: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, amefanikiwa kuleta mapinduzi ya kijani kwenye kilimo cha zao la pamba na zao la alizeti kupitia uhamasishaji wa kampuni ya MSK Solutions Ltd ambayo inatoa mbegu bora, pembejeo, zana za kilimo, elimu ya kilimo bora na uwezeshaji wa wagani vijijini, soko la uhakika la mazao hayo na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao vijijini (Imekamilisha ujenzi wa maghala kule Ndekeli (Tarafa ya Puge), Igalula (Tarafa ya Mwakalundi), Nhabala (Tarafa ya Bukene) na imeanza ujenzi wa ma-godown mapya kule Nhobola (Tarafa ya Nyasa) na Usongohala (Tarafa ya Bukene). Mafanikio ni kuongezeka kwa wakulima wa pamba kutokea wakulima 355 mwaka 2008 hadi kufikia wakulima 24,000 wa pamba mwaka 2012 na kufanya idadi ya kilo za pamba zilizovunwa kufikia takriban milioni 6 kutoka kilo 20,000 mwaka 2008. Pia idadi ya wakulima wa alizeti imeongezeka kutoka wakulima 400 mwaka jana hadi kufikia 3500 mwaka 2013.

Makampuni ya wanunuzi wa pamba yameongezeka kutoka kampuni moja ya MSK na kuwa manne hivi sasa – hali inayoleta ushindani kwenye soko na hivyo kupandisha bei zaidi kwa faida ya mkulima. Japokuwa kampuni ya MSK Solutions Ltd imeamua kuacha kuhamasisha pamba na kujikita zaidi kwenye alizeti itaendelea kukumbukwa kwa kutia chachu uhuishaji wa kilimo cha zao hili kilichokuwa kimekufa.

Mipango inaendelea kuwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya kula kutokana na alizeti ya Nzega, tayari halmashauri ya Nzega imeazimia kutenga viwanja 10 kwenye eneo maalum la kujenga viwanda. Pia Mbunge wa Nzega amewezesha wananchi kujiunga katika vikundi vya ushirika wa SACCOS vipatavyo 9 na yupo kwenye harakati za kuvijengea uwezo vifanye kazi za kukuza uchumi kama vile kilimo, mifugo ya kuku kwa kuzalisha vifaranga na mayai, na shughuli za ufundi kwa vijana. Mbunge wa Nzega amegawa mashine mbili kwenye SACCOS ya vijana nay a wazee kwa ajili ya kuangulia vifaranga. Ili kuhakikisha chama kinakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo vijijini, Mbunge wa Nzega akishirikiana na mwenzake wa Bukene wamegawa mbegu za alizeti kwenye kila kata. Pia Mbunge wa Nzega amegawa pikipiki 10 kwenye kata 10 ili kuweka urahisi zaidi wa kufikisha huduma za ushauri wa maendeleo kwa wakulima vijijini.

2.4  Ujenzi wa Miundombinu Nzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameweza kushawishi vikao mbalimbali vya maamuzi na kuhakikisha azimio la kujenga barabara za lami Nzega Mjini linafanikiwa, hivi sasa tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kutekeleza hilo kwenye mwaka wa fedha wa 2013/14; pia kufunga mataa ya kuangaza mji mzima wa Nzega. Mbunge wa Nzega pia kupitia mfuko wa Jimbo amejenga daraja korofi na lililosahaulika kwa muda mrefu la Butandula, na sasa anatafuta namna ya kuhakikisha pia daraja lingine la Nhobola nalo linajengwa, tayari ametenga sh milioni 8 za mfuko wa jimbo kutekeleza hilo.

Mradi wa barabara ya Nzega – Tabora kwa kiwango cha lami – Mbunge wa Nzega kwa kutumia nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Tabora, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali inaleta fedha za kukamilisha mradi huu ndani ya muda uliopangwa na pia kusimamia kuhakikisha barabara hiyo na nyingine za mkoa wa Tabora, zinajengwa kwa viwango vya ubora unaostahiki, na wananchi wanapata ajira na kulipwa fidia ya mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi huu.

Pia Mbunge amehakikisha barabara korofi kama za kutoka Mbagwa – Nkiniziwa, Busondo – Ndekeli, Busondo – Mwakashanhala zinaingia kwenye bajeti ya ujenzi mwaka huu wa fedha 2013/14 na kuhakikisha zinajengwa, pia barabara nyingine muhimu kama za Muhugi – Mizibaziba – Ndekeli – Ndala zinaingizwa kwenye bajeti, lengo likiwa ni kuhakikisha Nzega inakuwa na mtandao mzuri wa lami mahala pote. Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) amefanikiwa kuhakikisha mradi wa kupeleka umeme Ndala kutoka Nzega unatekelezwa kwa viwango vya ubora unaofaa, na sasa anahangaika kuhakikisha pia maeneo ya Mbogwe, Wela, Miguwa, na yale ya Usagali, Kaloleni hadi Mirambo Itobo nayo yanapata mradi wa Umeme. Tayari maombi yake yameingizwa kwenye orodha ya miradi ya Umeme Vijijini (REA Phase II) na hivyo maandalizi ya awali ya upembuzi yakinifu yataanza muda wowote kuanzia sasa. Sambamba na jitihada hizi, Mbunge amefanikiwa kuishauri na hatimaye kuishawishi halmashauri ya Nzega kuanzisha kampuni ya ujenzi (NCCCL) na kuinunulia mitambo ya kuchongea barabara, mpango ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.

2.5  Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nzega: Baada ya kutoridhishwa na namna miradi ya maji ya benki ya dunia na ile ya serikali inavyosuasua, Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameshauri na hatimaye kuishawishi Halmashauri wanunue mitambo ya kuchimba visima na kuiweka chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi Nzega (NCCCL) ili kuondoa yale matatizo kwamba mkandarasi amelipwa achimbe kisima kimoja akikosa maji basi na pesa ya serikali ndiyo imeishaliwa. Pesa za kununulia mitambo hiyo zitatokana na mapato yaliyopatikana kutokana na ushuru wa huduma uliolipwa na kampuni ya Resolute. Tukiwa na mitambo yetu tutahakikisha tunachimba kisima na maji yanapatikana kwenye kila kijiji bila shida ndipo twende kijiji kingine. Pia Mhe. Mbunge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Tabora unaanza kutekelezwa – na kwa sasa hatua ya utafiti wa awali ilishamalizika na tunatarajia upembuzi yakinifu utafanyika mwaka huu na pengine mwakani kuanza kutekelezwa, ukizingatia hii ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Jakaya Kikwete. 

2.6  Upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa Umma: Mhe. Mbunge, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameamua kuanzia mwaka 2014 ataweka ratiba maalum ya kutumia taaluma yake ya udaktari kutibu wagonjwa kwenye vituo mbali mbali vya afya Nzega. Pia ameandaa mkakati kabambe wa kuleta madaktari bingwa wanaoruka (flying doctors) kwa ajili ya kuweka kambi ya tiba maalum mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya wananchi wa Nzega. Kwa kushirikiana na madiwani wenzake wa halmashauri ya Nzega wamefanikiwa kuhakikisha vituo pamoja na nyumba za walimu zilizoanza kujengwa na wananchi vinamaliziwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi – tayari bajeti imetengwa kumalizia vituo vyote mwaka 2013/14, na anaendelea kuhamasisha vijiji vingine ambavyo havijaanza kutekeleza mpango huu vianze mara moja ili tubaki tukitafuta namna ya kupambana na chamngamoto nyingine za watumishi, vifaa na madawa.

N.B: Kuna mambo mengi yanayofanyika Nzega kwa ushawishi wa Mbunge na Madiwani, yakitekelezwa na serikali kutokana na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mwaka 2010 – 2015, lakini si yote yaliyoripotiwa hapa. 

Taarifa hii imetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega, pia inapatikana hapa www.hamisikigwangalla.com na kigwangalla.blogspot.com 

Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb.)
Leo Siku ya Jumamosi, Desemba 21, 2013. 

Friday, February 1, 2013

HOJA BINAFSI YA KULITAKA BUNGE LIPITISHE AZIMIO LA KUANZISHA MPANGO MAALUM WA KUKUZA AJIRA KWA VIJANA KWA KUANZISHA MFUKO WA MIKOPO YA VIJANA WANAOWEKEZA KWENYE KILIMO NA VIWANDA VYENYE UHUSIANO WA MOJA KWA MOJA NA KILIMO

Mhe. Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezimungu muumba wa viumbe vyote, aliyetujaalia pumzi na kutupa afya safi, nguvu na uwezo wa kufika hapa siku hii ya leo, na zaidi kuniwezesha mimi kupata fursa hii adhimu na adimu sana kuwasilisha hoja hii mbele ya Bunge lako tukufu.

Mhe. Spika, nakushukuru sana wewe binafsi, naibu wako, wenyeviti wa Bunge na makatibu kwa msaada wenu katika kuwezesha uwasilishaji murua wa hoja hii siku ya leo. Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Mhe. Jenista Mhagama (Mb.), Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM kwa ushauri na ushirikiano alionipa wakati nikiandaa hoja hii, pia bila kumsahau Mhe. Hussein Mzee (Mb.), Mtunza Hazina wa Kamati ya Wabunge wa CCM, na watumishi wote wa Ofisi yetu ya Kamati ya Wabunge wa CCM.

Mhe. Spika, naomba pia nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Nzega kwa kuendelea kuniunga mkono katika harakati zetu za kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii Nzega. Wananzega ni mashahidi na wafaidika wakubwa wa miradi ya kilimo cha pamba, alizeti, miembe ya kisasa ya SUA, na sasa tunaingia kwenye uzalishaji na ufugaji wa kuku, miradi ambayo ilibuniwa kwa ushirikiano baina ya wananchi wa Nzega na Mbunge wao, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ambaye ni Mwenyekiti Mwanzilishi wa Shirika la Maendeleo Nzega (yaani Nzega Development Foundation Ltd), kwa kutumia nadharia zinazofanana na mapendekezo ya kwenye hoja hii. Ujumbe wangu kwa wananchi wa Nzega ni kwamba, nawaomba msitetereke pamoja na jitihada za wapinzani wangu kisiasa kupotosha ukweli, jambo ambalo halijawahi kufanikiwa – ni imani yangu kwamba ‘nyie wenyewe mnaijua dawa yao.’

Mhe. Spika, kazi ya ubunge ni ngumu sana, ina changamoto nyingi. Kubwa kwa mbunge kijana kama mimi ni ‘muda’. Muda wa kusoma, muda wa kuzaa, muda wa kulea na muda wa kutekeleza majukumu ya kiwakilishi. Niwashukuru mke wangu Dr. Bayoum (na nimpe pole kwa uchungu anaoupata huko labour ward), na mabinti zangu Sheila na Hawa Kigwangalla kwa kuendelea kunivumilia kila siku ninapokuwa ‘bize’ kutekeleza majukumu yangu. Wote nawaomba wadumishe upendo na uelewa kwangu wakitambua kuwa ninawapenda na mara zote ninawakumbuka sana, ninawa-‘miss’ sana!

Mhe. Spika, ama baada ya shukrani naomba sasa nianze kuiwasilisha hoja yangu rasmi kama ifuatavyo: Kwamba, japokuwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita Tanzania imerekodi viwango vya juu sana vya kukua kwa uchumi, tuna mafanikio kidogo sana katika kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi; na pia ukuaji huu mkubwa wa uchumi umeshindwa kuzalisha ajira za kutosha kuendana na kasi ya kuongezeka kwa idadi ya vijana kwa sababu za mpito za kidemografia (demographic transition), na pia ukuaji huu wa uchumi umeshindwa kuendana na ukuaji wa idadi ya vijana wanaotafuta kazi za kuajiriwa na pia kujiajiri, pia ukuaji huu wa uchumi unaopigiwa mfano kila kona ya dunia hii bado umeshindwa kuendana na kukua kwa kasi ya wahitimu kutoka kwenye vyuo vya elimu ya juu, ya kati na hata vile vya ufundi na ujuzi mbalimbali, na pia ukuaji huu umeshindwa kuendana na kukua kwa lazima kwa kasi ya uhitaji wa kilimo cha umwagiliaji kutokana na kupungua kwa ujazo wa mvua zinazonyesha na hivyo kupelekea wakulima wadogo vijijini wanaotegemea mvua, kupata mazao pungufu ya matarajio na jitihada zao.

Mhe. Spika, Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7 kwa kipindi cha kuanzia 2001 – 2010, ulianguka kidogo mwaka 2009 ambapo ulishuka mpaka asilimia 6 (kwa sababu ya kuanguka kwa uchumi wa dunia), japokuwa uliruka juu tena na kurudi kwenye kiwango chake cha awali cha asilimia 7 mnamo mwaka 2010. Sekta zilizokua kwa kasi zaidi mwaka 2010 zilikuwa ni mawasiliano (asimilia 22.1), ikifuatiwa na ujenzi (asilimia 10.2), umeme na gesi (asilimia 10.2), fedha (asilimia 10.1) na uzalishaji viwandani (asilimia 7.9). Kwa ujumla kukua kwa pato la taifa kuliendeshwa zaidi na biashara (trading), huduma za marekebisho (repairs), kilimo, uzalishaji, biashara ya majengo (real estate business) na huduma za kibiashara (business services). Mfano katika kipindi cha kuanzia 2001 mpaka 2007, pato la taifa lilikuwa kwa kiwango cha wastani wa asilimia 7.1, umaskini ulipungua (kwa kipimo cha Head Count Index) kutoka 35.7 mpaka 33.6 tu. Hii inaonesha wazi kabisa kwamba ukuaji wa uchumi haujawa mpana na haujawalenga wananchi maskini.

Mhe. Spika, kwa mujibu wa takwimu za Integrated Labour Force Survey za Tanzania za mwaka 2006, kiwango cha ujumla cha ukosefu wa ajira kilikuwa ni asilimia 12.9; kwa vijana kiwango ni kikubwa zaidi ya hiki, ambapo ni asilimia 17 kwa Tanzania Bara na asilimia 20 kwa Zanzibar. Hii inaonesha kuwa nguvu kazi kubwa zaidi ya Taifa letu haitumiki ipasavyo (underutilized), inaachwa inachanganyikiwa. Hata hivyo, viwango hivi bado ni vya chini ukilinganisha na ongezeko kubwa la vijana wanaohitimu masomo kutokana na wimbi kubwa la ongezeko la vyuo vikuu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi sasa. Na pia hata wale ambao wanachukuliwa kama wameajiriwa kwenye sekta binafsi, na ama wamejiajiri kwenye biashara ndogo ndogo, ufundi, kilimo, mifugo na uvuvi, kumekuwa hakuna tija ya kazi wanayoifanya. Mhe. Spika, Inakadiriwa kwamba kila mwaka zaidi ya wahitimu 1,200,000 kutoka kwenye ngazi mbali mbali za taaluma wanaingia kwenye soko la ajira lakini soko hili lina uwezo wa kuhudumia wahitimu 200,000 tu!

Mhe. Spika, tunatakiwa tufike mahala tukae chini tujiulize, tutafakari, na hatimaye tuchukue hatua. Kwa takwimu hizi utaona kuwa, kunyanyua juu kiwango cha ukuaji wa uchumi na haswa kwenye sekta zinazoshirikisha watu wengi zaidi ni jambo lenye umuhimu wa kipekee, hivyo kuvutia na kuwezesha uwekezaji kwenye sekta ambazo zinaajiri watu maskini walio wengi ni jambo la lazima.

Mhe. Spika, Takriban Miezi 13 iliyopita, ndani ya siku moja, nilikutwa na wakati mgumu sana baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa vijana mbalimbali 6 waliohitimu masomo yao ya shahada mbalimbali wakinitaka niwasaidie kupata mahala ‘pa kujishikiza’, kwenye mashirika ya 'marafiki zangu'. Mtihani huu ulikuwa mgumu sana kwangu. Nilijiuliza, ‘Nitautatuaje?’ Imani yangu ni kwamba siko peke yangu katika hili. Waheshimiwa wabunge wenzangu ni wahanga wa maswali magumu kama haya kutoka kwa vijana majimboni kwetu. Matumaini ya vijana na ya watanzania (kwa ujumla) yamewekwa rehani kwenye vichwa na mioyo ya waheshimiwa wabunge.

Mhe. Spika, binafsi nilibaki nikijiuliza, ‘Hivi marafiki zangu kila siku wanatoa nafasi za ajira kwenye mashirika yao?’ Maswali haya yalinifanya nimfikirie upya kijana wa kitanzania. Nikapata muda wa kufikiri kwa mapana na kwa kina kidogo na kubaini kwa haraka tu kabisa, na bila shida hata kidogo; kwamba, kama Taifa tuna tatizo, tena tatizo kubwa kweli kweli: nilijiuliza sana, hivi ni kwa nini vijana hawa hawakunijia na mawazo ya namna ya kujiajiri badala yake wanataka mahali pa kujishikiza? Tunazalisha ajira ngapi kwa mwaka? Wanaohitimu na wanaotafuta ajira, kutoka kwenye utitiri wa vyuo vikuu, kwa ujumla wao wapo wangapi? Wanaobaki bila ajira na ni wenye nguvu, nia, ari na wasaa wa kufanya kazi ni wangapi? Na je kama taifa tunawatumiaje?

Mhe. Spika, leo hii kuna fursa za masoko kwenye nchi za SADC, EU, AGOA na Jumuiya ya Africa ya Mashariki. Leo hii ni vijana wangapi wa kitanzania, kwa mfano, wamepata ajira nchini Kenya ama na kinyume chake ni vijana wangapi wa Kenya wanavamia soko la ajira la Tanzania na wanapewa nafasi za kipaumbele kwenye mashirika mbalimbali binafsi? Ni kampuni ngapi za vijana wa kitanzania zinauza bidhaa zake nchini Kenya? Tunapofungua milango kwa kusaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa, maana yake tunawakaribisha wenzetu ndani ya soko letu, je sisi tunaingia kwenye masoko yao? Ni lazima tufanye jitihada za maksudi za kuwaandaa vijana wa kitanzania kuwa washiriki mahiri, kuwa washindani wenye nguvu kwenye masoko ya ajira na kwenye kunyakua fursa mbali mbali za kuuza bidhaa nchi za nje.

Mhe. Spika, tunaposema uchumi wetu umekua, tunatathmini kama kweli kukua huko kumetupa faida kiasi gani? Tunapata faida gani kutokana na kuongezeka kwa vyuo vikuu, taasisi za kuzalisha fikra (think tanks) na kukua kwa idadi ya wasomi wetu (critical mass)? Je tumejiandaa kiasi gani kukuza ajira kwa vijana wetu? Maswali haya na mengi mengineyo ni magumu na hayajibiki kirahisi hata kidogo!

Mhe. Spika, nikasema, labda tuanzishe mjadala mahsusi wa kitaifa, utakaolitazama suala la ajira kwa vijana wa kitanzania kwa mapana na marefu, na kulipatia ufumbuzi. Vijana wa zama hizi hawataki maneno, wanataka vitendo. Maneno na mipango mizuri iliyoandikwa haitowasaidia sana, wanahitaji fursa nzuri za ajira, za kujiajiri, za kuendesha maisha yao. Mipango mgando na butu kama ule wa kuwawezesha vijana kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana kule kwenye halmashauri zetu, ama ule wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) haijaleta mapinduzi yoyote yale mpaka sasa. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kusimama hapa na kuipigia jalamba mikakati kama ile maana vijana hawaielewi na wala hawajaona matunda yake. Tena vijana wa siku hizi, Mhe. Spika, hawako tayari kutumiwa na wanasiasa, wa chama chochote kile cha siasa kwa faida za kisiasa. Vijana wanataka kuona mabadiliko, wanataka kuona mapinduzi, si yale ya kisiasa yasiyo na tija, wanataka kuona mapinduzi ya kiuchumi, na wako tayari kushiriki katika harakati za kufikia mapinduzi hayo.

Mhe. Spika, nimefanya tafakuri tunduizi juu ya ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana na pia kukuza uchumi wa nchi yetu na nimebaini kwamba uwekezaji kwenye kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na kilimo ndiyo suluhu ya haraka na ya ukweli ya tatizo la ajira kwa vijana; kwa namna yoyote ile haimaanishi hata kidogo kuwa hoja hii ndiyo muarobaini wa tatizo hili, ambalo ni pana na linahitaji ufumbuzi mpana zaidi wa kila sekta na linahitaji ushiriki wa wadau wengi zaidi, na kwamba si lazima kuwa vijana wote watataka kuwekeza kwenye ‘industries’ nilizozitaja hapa, hii ni dira tu na ni mchango wangu mdogo kwenye kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kabla halijawa ‘janga la kitaifa.’

Mhe. Spika, vijana wenye nguvu, wasipotumika vizuri, watatumiwa vibaya na watu wajanja wajanja wenye uchu na tamaa ya madaraka. Na wao wenyewe wanaweza kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa, kama kwenye mitandao ya biashara haramu za madawa ya kulevya, mitandao ya madangulo ya ukahaba, na hatimaye kuangamia wao wenyewe na wenzao wengine wengi zaidi. Kama taifa tuna wajibu wa kuandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya kizazi cha mbele yetu. Swali lingine hapa linazalishwa, Je tunaandaa mazingira hayo?

Mhe. Spika, azimio hili likitekelezwa litawawezesha vijana wote, wasomi na wasio wasomi, bali wajasiriamali, wenye ari, mshawasha, nia, tabia, fikra, hekima, utayari, utashi sahihi, na pia nguvu za kuwa watengeneza ajira badala ya watafuta ajira (job creators instead of job seekers) wajiunge kwenye vikundi na wafanye kazi za kujiajiri kwanza wao wenyewe lakini pia watakuwa waajiri wa wenzao. Mbali na faida za kiuchumi zitakazopatikana, pia mpango huu utaamsha ari ya mabadiliko ya kifikra (mindset change); kwamba badala ya vijana kusoma huku wakitarajia ajira baada ya masomo, kama ilivyo ada, watakuwa wakisoma huku wakifikiria kujiajiri na kutajirika, badala ya kuishi na kukua wakitegemea serikali itawaletea maendeleo yao, vichwa vyao sasa vitafunguka wataweza kufungulia ‘potentials’ zao nyingine, wataanza kuota kufika mbali zaidi katika maisha yao. Na wale watakaofanikiwa watakuwa mfano bora zaidi kwa wenzao, na hapo tutajikuta tumejenga taifa la watu makini, wawajibikaji na wenye tamaa ya mafanikio (ambitious na responsible citizens). Ile dhana kwamba utajiri si stahiki yao, ni wa watu wachache tu wenye asili hiyo, kwa hakika itatoweka!

Mhe. Spika, Pamoja na kuwekeza kwenye kilimo, vijana wataweza kujenga na kuendesha viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na kilimo (backward linkage), pia wengine wataanzisha kampuni za masoko (marketing & trading), wengine za usafirishaji (logistics and handling of goods), pia wataanzisha viwanda wezeshi (associated industries) mfano vya ‘packaging materials’.  

Mhe. Spika, wakati wengine wakiendeleza mashamba na viwanda vyao, ajira zitajizalisha zaidi kwenye sekta nyingine kutokana na uwekezaji huu (multiplier effect): mfano, wakati wengine wanawekeza kwenye mashamba na kwenye viwanda vyao, wengine watakuwa wanawekeza kwenye kuanzisha makampuni ya kutoa ushauri kwa wakulima, wengine kwenye ugunduzi wa mbegu, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, wengine kwenye habari na mawasiliano (mf. Kuboresha kilimo na upatikanaji wa masoko na taarifa za bei kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano kama vile ujumbe mfupi wa maneno (sms), intaneti – wengine wakiwatengenezea wengine tovuti kwa ajili ya biashara zao.

Mhe. Spika, pamoja na kuongeza tija na ufanisi (productivity and efficiency), tutakuwa tumeongeza uzalishaji wa mazao na bidhaa zinazotokana na mazao, tutakuwa tumeleta uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima karibu zaidi na wakulima (market stability and sustainability) na hatutouza mazao ambayo hayajaongezwa thamani kutoka shambani. Matarajio yangu ni kwamba, tutakuwa tumetatua si tu tatizo la ajira kwa vijana bali pia kwa kiasi kikubwa la kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao yetu, kuhakikisha masoko ya uhakika kwa wakulima, na mwishowe kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei (inflation rate) ya vitu na zaidi kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje ya Tanzania, jambo ambalo litachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha akaunti yetu ya ‘balance of payments’.

Mhe. Spika, ukiuangalia mpango huu vizuri utagundua kwamba kutakuwa na vijana wasomi (watakaowezeshwa kuwekeza kwenye mashamba makubwa ya kibiashara na viwanda) na wale ambao hawajasoma (watakaowekeza kwenye kilimo cha mashamba ya saizi ya kati na hata yale madogo madogo, na pia viwanda vidogo vidogo), haya makundi yatabebana kwenye model hii, na hivyo kila kundi litatoa ajira kwa watu wengi zaidi.

Mhe. Spika, kama kila kitu kikienda sawa (ceteris paribus), kibaiolojia tunawategemea vijana wataishi kwa muda mrefu huko mbele zaidi ya wazee. Tukiwatumia vijana kwa kuona mbele kuna nini, wakiwekeza leo na wakifanikiwa kuendesha biashara zao kwa faida maana yake ni kwamba baada ya miaka 20, Tanzania itakuwa na watu wenye nguvu na wenye uchumi imara, na kwa kuwa sekta binafsi ni injini ya kukua kwa uchumi wa nchi, tutatoka kwenye kundi la nchi maskini zaidi duniani. Pia, ni rahisi sana kwa kijana kufanya jambo la kubahatisha ama kuthubutu (kubeba ‘risk’) na kufanya kazi kwa bidii kufikia ndoto zake bila wasiwasi, na zaidi kundi hili likipewa kipaumbele linaweza kuondoa utamaduni wa watanzania kutoka kwenye kufanya mambo kwa mazoea (yaani 'business as usual' na 'laissez-faire') na kuwa nchi ya watu wenye kufanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu na ‘passion’ ya ukweli. Mimi naliona hili ndiyo kundi pekee litakaloweza kuijenga Tanzania mpya, Tanzania ya miaka 20 ijayo. Sina nia ya kuonekana ni mbaguzi wa wazee, ama simaanishi kuwa wazee hawahitajiki, la hasha, napenda kusema tu kuwa mpango huu ni mahsusi kwa vijana tu.

Mhe. Spika, ni lazima tuwe na ndoto. Na pia ni lazima tujipange kuzifikia ndoto zetu. Hakuna ujanja mwingine. Hatuwezi kufanikiwa kwa kutumia mikakati ile ile iliyotufikisha hapa. Ni jambo moja kuwa na ndoto, na ni lingine kujipanga namna ya kuifikia. Ni jambo lisiloyumkinika kupanda bangi na kujiandaa kuvuna mchicha hatimaye! Tunahitaji kubadilika, tupande mbegu za kuuandaa uchumi wa Tanzania ya kesho. Tunahitaji mawazo mapya , njia mpya za utekelezaji, na hapo ndipo tutaona matokeo mapya!
Mhe. Spika,

Baada ya maelezo haya, hoja yenyewe sasa inawasilishwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 54 (1.), (2.) na (3.), kama ifuatavyo: -

KWA KUWA, idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania (zaidi ya asilimia sitini) ni vijana chini ya miaka 40
NA KWA KUWA, vijana hawa ni nguvu kazi ya kutegemewa katika nchi yetu na kama kila kitu kitabaki sawa (ceteris paribus), kibaiolojia vijana hawa watakuwepo nchini kwa miaka mingi ijayo ukilinganisha na wazee

NA KWA KUWA, vijana wanahangaika kutafuta ajira na kuna fursa nyingi za kutengeneza ajira nchini ambazo hazijafanyiwa kazi

NA KWA KUWA, vijana wengi nchini humu wamedhihirisha kuwa wana ari, nguvu, nia, elimu, ujuzi na vipaji vya kupigiwa mfano kwenye fani mbalimbali na wanakosa mitaji na mpango mahsusi na wa maksudi wa uwezeshi, wanahitaji uongozi (leadership, mentorship and guidance) ili kukamilisha ndoto zao

NA KWA KUWA, tuna malengo ya kuivusha nchi yetu kiuchumi kufikia 2025 (cf. dira ya maendeleo Tanzania 2025) kuelekea nchi zenye uchumi wa ngazi ya kati (MICs), wengi wa watakaokuwepo (kibailojia) watakuwa ni vijana, na wanatakiwa kuwezeshwa ili wawe mhimili wa mwenendo wa uchumi wa Tanzania ya kesho tunayoilenga, na pia wakiwezeshwa leo tunaamini ndiyo wataifikisha Tanzania huko tunapopataka kesho

NA KWA KUWA, ili kuzalisha ajira nyingi zaidi na kwa haraka, kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja (backward linkage) na kilimo ndiyo jibu la msingi la nia hiyo

NA KWA KUWA, ilani ya uchaguzi ya CCM (Uk. 88 - 95, Kifungu Cha 79 (i.), (ii.) na (iii.)), ambacho ni Chama kinachotawala nchi yetu, inatambua na kutoa maelekezo mazuri kabisa kwa serikali kuhusiana na hoja hii ya kukuza ajira kwa vijana, na pia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (cf. Uk. 92, kifungu cha 5.2.4), na MKUKUTA II vinatambua umuhimu wa kutekeleza haya. Pia Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye maelezo yake ya utangulizi mwanzo wa Mpango huo anasema na ninamnukuu hapa, kwamba “Employment creation, particularly for the youth, is also a critical cross-cutting target of this Plan.” [inatafsirika Kiswahili kama ‘kutengeneza ajira, hususan kwa vijana, ni lengo mtambuka la huu mpango’]. Kinachotakiwa sasa si kingine bali ni kufanya jitihada za utekelezaji tu maana barabara zote zinaelekea huko.

HIVYO BASI, bunge linaazimia kuitaka serikali yetu ifanye yafuatayo:
  1. KWAMBA, Ianzishe mpango maalum wa kukuza ajira kwa vijana kwa kuanzisha mfuko wa mikopo ya vijana wanaowekeza kwenye kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja (backward linkage) na kilimo. Mfuko huu hapo baadaye utaendelezwa na kuwa Benki ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (Tanzania Youth Development Bank).

  1. KWAMBA, Ianzishe mfuko maalum wa kutoa mikopo ya uwekezaji kwa vijana wa Tanzania, utakaoitwa ‘Tanzania Youth Enterprise Challenge Fund’ na iwekeze katika mfuko huu mtaji usiopungua bilioni za kitanzania mia mbili (mwaka wa kwanza) na bilioni mia moja kila mwaka wa fedha utakaofuata. Mfuko huu uwalenge vijana watakaowekeza kwenye sekta ambazo tutazichagua, sana sana tuweke kipaumbele kwenye sekta za kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja (backward linkage) na kilimo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi kwa vijana. Vijana hawa waingizwe kwenye mashindano ya kuandika maandiko ya miradi (project proposals/business plans), na ile itakayoshinda kwenye mchakato huu ndiyo pekee itakayochaguliwa. Mchakato huu katika hatua Fulani, kama itabidi iwe hivyo, uwashirikishe wananchi kwa njia ya kupigia kura miradi wanayoona inafaa na ushindi katika hatua hii iwe ni kigezo kimojawapo cha kuwapata watakaoshinda.
 NA KWAMBA, Mikopo itakayotolewa katika mchakato huu itakuwa ni yenye masharti nafuu, kama ifuatavyo:
·         Itakuwa na riba ndogo (asimilia 6 kushuka chini),
·         Itakuwa na kipindi kirefu cha kurudisha (payback period)  - cha takriban miaka 15-20,
·         Itakuwa na kipindi kirefu cha kutoanza kurudisha mkopo (grace period) – kati ya miaka miwili hadi mitatu
·         Isiwe na masharti ya dhamana/security za mali (maana vijana hawana assets zozote) bali iwe na ‘dhamana’ maalum kama cheti cha elimu/ujuzi kwenye fani husika, ardhi ya shamba lililorasimishwa kwa utaratibu unaokubalika, na iwe kwenye usimamizi wa kitengo maalum cha mfuko huo. Mpango huu uendane na kuweka utaratibu mzuri na rahisi wa kusajili mashamba na ardhi.

  1. KWAMBA, Itenge maeneo maalum ya kuwekeza (special economic zones) chini ya mpango huu. Ichague maeneo maalum kwa mazao na viwanda maalum kwenye wilaya mahsusi za nchi yetu. Vijana waelekezwe na kusimamiwa kuwekeza kwenye sekta zilizochaguliwa na wawezeshwe kupata mitaji hiyo. Uanzishwaji wa miradi hii uendane na kuwepo kwa sharti la kuwataka vijana (wawekezaji) kuhamasisha kilimo cha kisasa na kusaidia wakulima kwenye maeneo yanayowazunguka kwa njia ya mkataba maalum (contract farming) wa kukopesha pembejeo za kilimo, mbegu bora za mazao, zana za kilimo ama kuwalimia na kuwavunia kwa mashine, kutengeneza mifumo ya umwagiliaji – hii itasaidia kuongeza tija na ufanisi kwa wakulima.

  1. KWAMBA, serikali iamue kuchagua sekta zitakazohusika kwenye mpango huu maalum kwa ajili ya vijana. Baadhi ya sekta za kuangaliwa ni pamoja na kilimo kikubwa cha kibiashara cha umwagiliaji – kila mradi ni lazima uwe na mpango wa kuwafikia wakulima wadogo wanaozunguka shamba husika (satellite out-grower schemes), ujenzi wa viwanda kama vya kuchambua pamba (ginneries) na kusokota nyuzi (spinning); kukoboa na kusaga unga/chakula cha mifugo; kukamua na kusafisha mafuta ya kula, pia kutengeneza sabuni; kusindika juice n.k, utafanyika kwenye maeneo ya karibu na mashamba hayo. Kila eneo la mradi litengwe likiwa na uwezekano wa kufanya utanuzi kwenye sekta hiyo ili kukamilisha mnyororo wa thamani kwenye  eneo moja (value chain).
Mhe. Spika,
NAOMBA KUTOA HOJA.


Dr. Hamisi Kigwangalla (MB),
Jimbo la Nzega.