Katika hali ya kutia moyo, wilaya ya Nzega imefanikiwa kufufua kilimo cha Pamba. Zao hili la biashara lililokuwa limepotea kabisa wilayani hapa sasa limerudi upya tena, japokuwa si kwa kufikia kiwango cha zamani lakini mwanga wa matumaini unaangaza kila kona. Wilaya ya Nzega iliacha kulima pamba takriban miaka 12 iliyopita kufuatia kuanguka kwa utaratibu mbovu wa ushirika uliokuwepo. Tatizo hili halikuikumba Nzega peke yake bali ukanda wote wa Western Cotton Growing Area (WCGA) (yaani mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kigoma, Singida, Kagera n.k). Ushirika ulikuwa ukinunua pamba kwa mkopo na kulipa wakulima pesa yao kwa awamu. Mwaka 1990 wakulima wote hawakulipwa pesa ya malipo yao ya awamu ya pili. Hii iliwakatisha sana tamaa na wengi wao waliacha kulima pamba msimu wa kilimo uliofuatia. Mwaka 1991, bei za pamba zilizidi kuanguka kwenye soko la dunia na hivyo kusababisha ushirika tena kushindwa kununua pamba ya wakulima vizuri ipasavyo, na mzunguuko huu ulipelekea wakulima wengi zaidi kususa kulima pamba misimu iliyofuatia. Mfumo wa masoko ulipoboreshwa kwa kuingia kwa soko huria hapo baadaye, sehemu nyingine zilirudia kilimo cha pamba lakini Nzega ilikoma kabisa na pamba ikabaki historia! Na huu ulikuwa mwanzo wa kushamiri wa kwa umaskini wilayani Nzega. Maana wakulima walilazimika kuuza chakula ili wapate hela badala ya kuuza mazao ya biashara.
Kampuni ya MSK Solutions Ltd ikishirikiana na Serikali wilaya ya Nzega na Kampuni ya Rural Livelihood Development Company (RLDC) wamejifunga mikanda na kwa pamoja wamefanikiwa kuleta mapinduzi ya ukweli ya kijani. Pamba imerudi tena Nzega, imerudi kwa kasi ya ajabu ambayo haikutegemewa. Kwa pamoja wadau hawa wamekuwa wakiendesha mradi wa Nzega Cotton Development Project (NZECODEP) ambao unafadhiliwa kwa pamoja na wadau wawili, MSK Solutions Ltd na RLDC.
Mradi huu umeweza kufanikiwa kwa sababu zifuatazo, kwanza umewahakikishia wakulima soko la uhakika na bei nzuri zaidi ya pamba yao. Pili, mradi unahakikisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo cha pamba karibu na wakulima na kwa bei nzuri zaidi. Tatu, wakulima wanahakikishiwa ushauri wa kitaalamu karibu zaidi kwa kuwa mradi unawawezesha posho kidogo mabwana shamba ili kuwatia morali zaidi wa kutoa huduma za ugani.
Katika uhamasishaji huu, ujumbe mahsusi unaowafikia wakulima ni pamoja na uhakika wa vitu vyote hivi na pia maelezo yanayotoa cost-benefit analysis ya kilimo cha pamba ukilinganisha na mazao mengine na kwamba pamba haikuja kufuta kilimo cha mazao mengine bali kuhakikisha mkulima anakuwa na zao la mbadala endapo ikitokea amekosa mavuno ya kutosha ya mazao ya chakula ama mengine ya biashara atakayokuwa amelima. Pia wakulima wanaeleimishwa kuwa pamba inastahimili ukame ukilinganisha na mahindi na mpunga na hivyo kama mkulima akikosa hayo mazao mengine yote na akapata pamba, atauza atapata hela na kwenda kununua chakula. Na kama akipata mazao mengine, basi atafanya mambo mengine kwa kutumia hela itokanayo na pamba.
Kutoka kilo 20,000 Mwaka wa Kwanza, hadi 350,000 na sasa Kilo 982,000! Mbali na kukuza kipato cha mkulima mmoja mmoja, pamba itakuwa ni chanzo kipya kikubwa cha mapato ya halmashauri ya wilaya ya Nzega kupitia ushuru wa mazao (district cess) na hivyo kufanikisha miradi mbali ya maendeleo kama mabarabara, shule, zahanati n.k. Pia faida nyingine ni pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha na hivyo kutia chachu sekta nyingine za maendeleo na huduma wilayani hapa. Pia kushamiri kutaleta viwanda wilayani hapa. Maendeleo haya ni endelevu na yanagusa watu wengi ukilinganisha na uwepo wa mgodi mkubwa wa uchimbali dhahabu ambapo ikiisha ndiyo basi tena.
Kikwazo kikubwa kinachoukumba mradi, pamoja na mambo mengine, ni propaganda za kisiasa zinazofanywa na wanasiasa kwa vile tu harakati za kufufua zao la pamba Nzega zinafanywa na kampuni ya MSK Solutions Ltd ambamo Mbunge wa Jimbo la Nzega ana hisa.
Makala hii imeandaliwa na Ndg. Kumotola L. Kumotola, Afisa Mahusiano, Uratibu na Itifaki - Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega akishirikiana na Ndg. Hassan Jaha, Mratibu wa Mradi wa NZECODEP, MSK Solutions Ltd, Nzega.
Subscribe to:
Posts (Atom)