Are we Realistically Trying to Solve the Electricity Problem in Our Country?

Tuesday, June 7, 2011
Mpaka leo hii, tuna mitambo ya jumla ya MW 336 inayowashwa kwa kutumia gesi asilia, yaani kuna ile inayomilikiwa na kuendeshwa na Songas (MW 191), ile ya serikali ya Ubungo (MW 100) na ile ya Tegeta (MW 45). Hii mitambo tu ukiongeza na ile ya makampuni kama matatu hivi yanayotumia gesi asilia kuendeshea mitambo yao, yameisha-exhaust supply ya gesi. Hata ile ya Dowans ikiwashwa leo, bado haitoweza kuwaka to full capacity (ya 112 MW), badala yake itazalisha MW 75 tu, kwa sababu ya poor supply ya gesi.

Leo hii kuna miradi ya Ubungo - MW 100, Kinyerezi MW 260 na Somanga Fungo MW 240, jumla yake ni MW 600. Je, serikali iko tayari kuwekeza kwenye bomba jipya litakalosaidia kutatua tatizo hili la upatikanaji wa gesi, ambalo ni very expensive?

Leo hii serikali inalalamikia gharama za uendeshaji wa mitambo ya IPTL, inayotumia Heavy Fuel Oil (HFO) kuwa ziko juu sana, sasa kwa nini tena inajenga power plant ya Mwanza (MW 60) kwa mitambo itakayotumia HFO ilhali wanaiona IPTL inavyosumbua kwa gharama?

Saa nyingine unashindwa kuelewa ni jinsi gani wasomi wetu wanafanya maamuzi mazito kama haya! Sijui wanakuwa wanatumia vigezo gani?

Hivi kwa nini serikali isianzishe mradi wa Umeme na wakajikita zaidi kwenye MW chache tu zilizo ndani ya uwezo wetu? Kama walivyofanya kwenye barabara kwa nini wasifanye hivyo pia kwenye umeme???

TATIZO LA UMEME NCHINI!

Mhe. Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla (MB), atauliza:-

(a) Tangu serikali ya awamu ya pili hadi leo, serikali imetumia jumla ya shilingi ngapi kuzalisha umeme, na bado tatizo lipo?

(b) Je, tatizo la umeme nchini litaisha lini?

(c) Kwa nini serikali inaongea mipango mingi ya kutatua tatizo la umeme bila kutekeleza na kwa nini suala la upatikanaji umeme nchini ni la dharura kila siku?

Waziri wa nishati na madini atajibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mhe. Spika, uwekezaji wa serikali katika miradi ya kuzalisha umeme tangu kipindi cha serikali ya awamu ya pili hadi leo unafikia jumla ya Dola za Marekani milioni 798.

(b) Mhe. Spika, tatizo la uhaba wa umeme litaisha baada ya kutekeleza kwa ukamilifu na kwa wakati mpango wa kipindi kifupi cha 2011 - 2015 kama ilivyofafanuliwa kwenye mpango kabambe wa uendelezaji wa sekta ya umeme wa mwaka 2009. Miradi itakayotekelezwa kipindi hicho itaongeza jumla ya MW 1830 kwenye mfumo wa gridi ya Taifa kwa gharama inayokadiriwa ya Dola za marekani milioni 3,700.

(c) Mhe. Spika, serikali imeazimia kutekeleza kwa wakati miradi ya kuzalisha na kusafirisha umeme kulingana na Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa sekta ya Umeme, hususan, katika kipindi cha 2011 - 2018. Miradi iliyopangwa kujengwa itaongeza MW 600 kwa kutumia maporomoko ya nguvu za maji, MW 870 kwa kutumia gesi asili, MW 1200 kwa kutumia makaa ya mawe na MW 100 kwa kutumia nguvu ya upepo. Serikali inategemea miradi hii itakamilika kwa kushirikisha uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuwa gharama za miradi hii yote ni kubwa.

Mhe. Spika, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza mikakati ya kutafuta fedha za kugharamia miradi ya kipaumbele niliyoitaja hapo juu.

Maswali Mawili ya Nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Kigwangalla:

(1) Kama toka awamu ya pili mpaka leo hii serikali ilitumia Dola za Marekani milioni 798 na bado hali ya upatikanaji umeme nchini ni duni kiasi hiki, serikali hii leo itapata wapi Dola za Marekani milioni 3,700?

(2) Mpaka leo miundombinu ya kusafirisha gesi kutoka Mnazi bay na Songosongo kwa ajili kuzalishia umeme kwenye mitambo iliyopo Dar es salaam ni duni na imechakaa, na uwekezaji kwenye bomba la kusafirishia gesi ni gharama kubwa, mnatuhakikishiaje dhamira ya serikali ya kulitatua tatizo la umeme kwa haraka kwamba ni ya ukweli au tutegemee kuendelea kufaidi mgao kila siku?