Friday, February 1, 2013

HOJA BINAFSI YA KULITAKA BUNGE LIPITISHE AZIMIO LA KUANZISHA MPANGO MAALUM WA KUKUZA AJIRA KWA VIJANA KWA KUANZISHA MFUKO WA MIKOPO YA VIJANA WANAOWEKEZA KWENYE KILIMO NA VIWANDA VYENYE UHUSIANO WA MOJA KWA MOJA NA KILIMO

Mhe. Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezimungu muumba wa viumbe vyote, aliyetujaalia pumzi na kutupa afya safi, nguvu na uwezo wa kufika hapa siku hii ya leo, na zaidi kuniwezesha mimi kupata fursa hii adhimu na adimu sana kuwasilisha hoja hii mbele ya Bunge lako tukufu.

Mhe. Spika, nakushukuru sana wewe binafsi, naibu wako, wenyeviti wa Bunge na makatibu kwa msaada wenu katika kuwezesha uwasilishaji murua wa hoja hii siku ya leo. Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Mhe. Jenista Mhagama (Mb.), Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM kwa ushauri na ushirikiano alionipa wakati nikiandaa hoja hii, pia bila kumsahau Mhe. Hussein Mzee (Mb.), Mtunza Hazina wa Kamati ya Wabunge wa CCM, na watumishi wote wa Ofisi yetu ya Kamati ya Wabunge wa CCM.

Mhe. Spika, naomba pia nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Nzega kwa kuendelea kuniunga mkono katika harakati zetu za kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii Nzega. Wananzega ni mashahidi na wafaidika wakubwa wa miradi ya kilimo cha pamba, alizeti, miembe ya kisasa ya SUA, na sasa tunaingia kwenye uzalishaji na ufugaji wa kuku, miradi ambayo ilibuniwa kwa ushirikiano baina ya wananchi wa Nzega na Mbunge wao, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ambaye ni Mwenyekiti Mwanzilishi wa Shirika la Maendeleo Nzega (yaani Nzega Development Foundation Ltd), kwa kutumia nadharia zinazofanana na mapendekezo ya kwenye hoja hii. Ujumbe wangu kwa wananchi wa Nzega ni kwamba, nawaomba msitetereke pamoja na jitihada za wapinzani wangu kisiasa kupotosha ukweli, jambo ambalo halijawahi kufanikiwa – ni imani yangu kwamba ‘nyie wenyewe mnaijua dawa yao.’

Mhe. Spika, kazi ya ubunge ni ngumu sana, ina changamoto nyingi. Kubwa kwa mbunge kijana kama mimi ni ‘muda’. Muda wa kusoma, muda wa kuzaa, muda wa kulea na muda wa kutekeleza majukumu ya kiwakilishi. Niwashukuru mke wangu Dr. Bayoum (na nimpe pole kwa uchungu anaoupata huko labour ward), na mabinti zangu Sheila na Hawa Kigwangalla kwa kuendelea kunivumilia kila siku ninapokuwa ‘bize’ kutekeleza majukumu yangu. Wote nawaomba wadumishe upendo na uelewa kwangu wakitambua kuwa ninawapenda na mara zote ninawakumbuka sana, ninawa-‘miss’ sana!

Mhe. Spika, ama baada ya shukrani naomba sasa nianze kuiwasilisha hoja yangu rasmi kama ifuatavyo: Kwamba, japokuwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita Tanzania imerekodi viwango vya juu sana vya kukua kwa uchumi, tuna mafanikio kidogo sana katika kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi; na pia ukuaji huu mkubwa wa uchumi umeshindwa kuzalisha ajira za kutosha kuendana na kasi ya kuongezeka kwa idadi ya vijana kwa sababu za mpito za kidemografia (demographic transition), na pia ukuaji huu wa uchumi umeshindwa kuendana na ukuaji wa idadi ya vijana wanaotafuta kazi za kuajiriwa na pia kujiajiri, pia ukuaji huu wa uchumi unaopigiwa mfano kila kona ya dunia hii bado umeshindwa kuendana na kukua kwa kasi ya wahitimu kutoka kwenye vyuo vya elimu ya juu, ya kati na hata vile vya ufundi na ujuzi mbalimbali, na pia ukuaji huu umeshindwa kuendana na kukua kwa lazima kwa kasi ya uhitaji wa kilimo cha umwagiliaji kutokana na kupungua kwa ujazo wa mvua zinazonyesha na hivyo kupelekea wakulima wadogo vijijini wanaotegemea mvua, kupata mazao pungufu ya matarajio na jitihada zao.

Mhe. Spika, Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7 kwa kipindi cha kuanzia 2001 – 2010, ulianguka kidogo mwaka 2009 ambapo ulishuka mpaka asilimia 6 (kwa sababu ya kuanguka kwa uchumi wa dunia), japokuwa uliruka juu tena na kurudi kwenye kiwango chake cha awali cha asilimia 7 mnamo mwaka 2010. Sekta zilizokua kwa kasi zaidi mwaka 2010 zilikuwa ni mawasiliano (asimilia 22.1), ikifuatiwa na ujenzi (asilimia 10.2), umeme na gesi (asilimia 10.2), fedha (asilimia 10.1) na uzalishaji viwandani (asilimia 7.9). Kwa ujumla kukua kwa pato la taifa kuliendeshwa zaidi na biashara (trading), huduma za marekebisho (repairs), kilimo, uzalishaji, biashara ya majengo (real estate business) na huduma za kibiashara (business services). Mfano katika kipindi cha kuanzia 2001 mpaka 2007, pato la taifa lilikuwa kwa kiwango cha wastani wa asilimia 7.1, umaskini ulipungua (kwa kipimo cha Head Count Index) kutoka 35.7 mpaka 33.6 tu. Hii inaonesha wazi kabisa kwamba ukuaji wa uchumi haujawa mpana na haujawalenga wananchi maskini.

Mhe. Spika, kwa mujibu wa takwimu za Integrated Labour Force Survey za Tanzania za mwaka 2006, kiwango cha ujumla cha ukosefu wa ajira kilikuwa ni asilimia 12.9; kwa vijana kiwango ni kikubwa zaidi ya hiki, ambapo ni asilimia 17 kwa Tanzania Bara na asilimia 20 kwa Zanzibar. Hii inaonesha kuwa nguvu kazi kubwa zaidi ya Taifa letu haitumiki ipasavyo (underutilized), inaachwa inachanganyikiwa. Hata hivyo, viwango hivi bado ni vya chini ukilinganisha na ongezeko kubwa la vijana wanaohitimu masomo kutokana na wimbi kubwa la ongezeko la vyuo vikuu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi sasa. Na pia hata wale ambao wanachukuliwa kama wameajiriwa kwenye sekta binafsi, na ama wamejiajiri kwenye biashara ndogo ndogo, ufundi, kilimo, mifugo na uvuvi, kumekuwa hakuna tija ya kazi wanayoifanya. Mhe. Spika, Inakadiriwa kwamba kila mwaka zaidi ya wahitimu 1,200,000 kutoka kwenye ngazi mbali mbali za taaluma wanaingia kwenye soko la ajira lakini soko hili lina uwezo wa kuhudumia wahitimu 200,000 tu!

Mhe. Spika, tunatakiwa tufike mahala tukae chini tujiulize, tutafakari, na hatimaye tuchukue hatua. Kwa takwimu hizi utaona kuwa, kunyanyua juu kiwango cha ukuaji wa uchumi na haswa kwenye sekta zinazoshirikisha watu wengi zaidi ni jambo lenye umuhimu wa kipekee, hivyo kuvutia na kuwezesha uwekezaji kwenye sekta ambazo zinaajiri watu maskini walio wengi ni jambo la lazima.

Mhe. Spika, Takriban Miezi 13 iliyopita, ndani ya siku moja, nilikutwa na wakati mgumu sana baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa vijana mbalimbali 6 waliohitimu masomo yao ya shahada mbalimbali wakinitaka niwasaidie kupata mahala ‘pa kujishikiza’, kwenye mashirika ya 'marafiki zangu'. Mtihani huu ulikuwa mgumu sana kwangu. Nilijiuliza, ‘Nitautatuaje?’ Imani yangu ni kwamba siko peke yangu katika hili. Waheshimiwa wabunge wenzangu ni wahanga wa maswali magumu kama haya kutoka kwa vijana majimboni kwetu. Matumaini ya vijana na ya watanzania (kwa ujumla) yamewekwa rehani kwenye vichwa na mioyo ya waheshimiwa wabunge.

Mhe. Spika, binafsi nilibaki nikijiuliza, ‘Hivi marafiki zangu kila siku wanatoa nafasi za ajira kwenye mashirika yao?’ Maswali haya yalinifanya nimfikirie upya kijana wa kitanzania. Nikapata muda wa kufikiri kwa mapana na kwa kina kidogo na kubaini kwa haraka tu kabisa, na bila shida hata kidogo; kwamba, kama Taifa tuna tatizo, tena tatizo kubwa kweli kweli: nilijiuliza sana, hivi ni kwa nini vijana hawa hawakunijia na mawazo ya namna ya kujiajiri badala yake wanataka mahali pa kujishikiza? Tunazalisha ajira ngapi kwa mwaka? Wanaohitimu na wanaotafuta ajira, kutoka kwenye utitiri wa vyuo vikuu, kwa ujumla wao wapo wangapi? Wanaobaki bila ajira na ni wenye nguvu, nia, ari na wasaa wa kufanya kazi ni wangapi? Na je kama taifa tunawatumiaje?

Mhe. Spika, leo hii kuna fursa za masoko kwenye nchi za SADC, EU, AGOA na Jumuiya ya Africa ya Mashariki. Leo hii ni vijana wangapi wa kitanzania, kwa mfano, wamepata ajira nchini Kenya ama na kinyume chake ni vijana wangapi wa Kenya wanavamia soko la ajira la Tanzania na wanapewa nafasi za kipaumbele kwenye mashirika mbalimbali binafsi? Ni kampuni ngapi za vijana wa kitanzania zinauza bidhaa zake nchini Kenya? Tunapofungua milango kwa kusaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa, maana yake tunawakaribisha wenzetu ndani ya soko letu, je sisi tunaingia kwenye masoko yao? Ni lazima tufanye jitihada za maksudi za kuwaandaa vijana wa kitanzania kuwa washiriki mahiri, kuwa washindani wenye nguvu kwenye masoko ya ajira na kwenye kunyakua fursa mbali mbali za kuuza bidhaa nchi za nje.

Mhe. Spika, tunaposema uchumi wetu umekua, tunatathmini kama kweli kukua huko kumetupa faida kiasi gani? Tunapata faida gani kutokana na kuongezeka kwa vyuo vikuu, taasisi za kuzalisha fikra (think tanks) na kukua kwa idadi ya wasomi wetu (critical mass)? Je tumejiandaa kiasi gani kukuza ajira kwa vijana wetu? Maswali haya na mengi mengineyo ni magumu na hayajibiki kirahisi hata kidogo!

Mhe. Spika, nikasema, labda tuanzishe mjadala mahsusi wa kitaifa, utakaolitazama suala la ajira kwa vijana wa kitanzania kwa mapana na marefu, na kulipatia ufumbuzi. Vijana wa zama hizi hawataki maneno, wanataka vitendo. Maneno na mipango mizuri iliyoandikwa haitowasaidia sana, wanahitaji fursa nzuri za ajira, za kujiajiri, za kuendesha maisha yao. Mipango mgando na butu kama ule wa kuwawezesha vijana kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana kule kwenye halmashauri zetu, ama ule wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) haijaleta mapinduzi yoyote yale mpaka sasa. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kusimama hapa na kuipigia jalamba mikakati kama ile maana vijana hawaielewi na wala hawajaona matunda yake. Tena vijana wa siku hizi, Mhe. Spika, hawako tayari kutumiwa na wanasiasa, wa chama chochote kile cha siasa kwa faida za kisiasa. Vijana wanataka kuona mabadiliko, wanataka kuona mapinduzi, si yale ya kisiasa yasiyo na tija, wanataka kuona mapinduzi ya kiuchumi, na wako tayari kushiriki katika harakati za kufikia mapinduzi hayo.

Mhe. Spika, nimefanya tafakuri tunduizi juu ya ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana na pia kukuza uchumi wa nchi yetu na nimebaini kwamba uwekezaji kwenye kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na kilimo ndiyo suluhu ya haraka na ya ukweli ya tatizo la ajira kwa vijana; kwa namna yoyote ile haimaanishi hata kidogo kuwa hoja hii ndiyo muarobaini wa tatizo hili, ambalo ni pana na linahitaji ufumbuzi mpana zaidi wa kila sekta na linahitaji ushiriki wa wadau wengi zaidi, na kwamba si lazima kuwa vijana wote watataka kuwekeza kwenye ‘industries’ nilizozitaja hapa, hii ni dira tu na ni mchango wangu mdogo kwenye kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kabla halijawa ‘janga la kitaifa.’

Mhe. Spika, vijana wenye nguvu, wasipotumika vizuri, watatumiwa vibaya na watu wajanja wajanja wenye uchu na tamaa ya madaraka. Na wao wenyewe wanaweza kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa, kama kwenye mitandao ya biashara haramu za madawa ya kulevya, mitandao ya madangulo ya ukahaba, na hatimaye kuangamia wao wenyewe na wenzao wengine wengi zaidi. Kama taifa tuna wajibu wa kuandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya kizazi cha mbele yetu. Swali lingine hapa linazalishwa, Je tunaandaa mazingira hayo?

Mhe. Spika, azimio hili likitekelezwa litawawezesha vijana wote, wasomi na wasio wasomi, bali wajasiriamali, wenye ari, mshawasha, nia, tabia, fikra, hekima, utayari, utashi sahihi, na pia nguvu za kuwa watengeneza ajira badala ya watafuta ajira (job creators instead of job seekers) wajiunge kwenye vikundi na wafanye kazi za kujiajiri kwanza wao wenyewe lakini pia watakuwa waajiri wa wenzao. Mbali na faida za kiuchumi zitakazopatikana, pia mpango huu utaamsha ari ya mabadiliko ya kifikra (mindset change); kwamba badala ya vijana kusoma huku wakitarajia ajira baada ya masomo, kama ilivyo ada, watakuwa wakisoma huku wakifikiria kujiajiri na kutajirika, badala ya kuishi na kukua wakitegemea serikali itawaletea maendeleo yao, vichwa vyao sasa vitafunguka wataweza kufungulia ‘potentials’ zao nyingine, wataanza kuota kufika mbali zaidi katika maisha yao. Na wale watakaofanikiwa watakuwa mfano bora zaidi kwa wenzao, na hapo tutajikuta tumejenga taifa la watu makini, wawajibikaji na wenye tamaa ya mafanikio (ambitious na responsible citizens). Ile dhana kwamba utajiri si stahiki yao, ni wa watu wachache tu wenye asili hiyo, kwa hakika itatoweka!

Mhe. Spika, Pamoja na kuwekeza kwenye kilimo, vijana wataweza kujenga na kuendesha viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na kilimo (backward linkage), pia wengine wataanzisha kampuni za masoko (marketing & trading), wengine za usafirishaji (logistics and handling of goods), pia wataanzisha viwanda wezeshi (associated industries) mfano vya ‘packaging materials’.  

Mhe. Spika, wakati wengine wakiendeleza mashamba na viwanda vyao, ajira zitajizalisha zaidi kwenye sekta nyingine kutokana na uwekezaji huu (multiplier effect): mfano, wakati wengine wanawekeza kwenye mashamba na kwenye viwanda vyao, wengine watakuwa wanawekeza kwenye kuanzisha makampuni ya kutoa ushauri kwa wakulima, wengine kwenye ugunduzi wa mbegu, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, wengine kwenye habari na mawasiliano (mf. Kuboresha kilimo na upatikanaji wa masoko na taarifa za bei kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano kama vile ujumbe mfupi wa maneno (sms), intaneti – wengine wakiwatengenezea wengine tovuti kwa ajili ya biashara zao.

Mhe. Spika, pamoja na kuongeza tija na ufanisi (productivity and efficiency), tutakuwa tumeongeza uzalishaji wa mazao na bidhaa zinazotokana na mazao, tutakuwa tumeleta uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima karibu zaidi na wakulima (market stability and sustainability) na hatutouza mazao ambayo hayajaongezwa thamani kutoka shambani. Matarajio yangu ni kwamba, tutakuwa tumetatua si tu tatizo la ajira kwa vijana bali pia kwa kiasi kikubwa la kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao yetu, kuhakikisha masoko ya uhakika kwa wakulima, na mwishowe kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei (inflation rate) ya vitu na zaidi kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje ya Tanzania, jambo ambalo litachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha akaunti yetu ya ‘balance of payments’.

Mhe. Spika, ukiuangalia mpango huu vizuri utagundua kwamba kutakuwa na vijana wasomi (watakaowezeshwa kuwekeza kwenye mashamba makubwa ya kibiashara na viwanda) na wale ambao hawajasoma (watakaowekeza kwenye kilimo cha mashamba ya saizi ya kati na hata yale madogo madogo, na pia viwanda vidogo vidogo), haya makundi yatabebana kwenye model hii, na hivyo kila kundi litatoa ajira kwa watu wengi zaidi.

Mhe. Spika, kama kila kitu kikienda sawa (ceteris paribus), kibaiolojia tunawategemea vijana wataishi kwa muda mrefu huko mbele zaidi ya wazee. Tukiwatumia vijana kwa kuona mbele kuna nini, wakiwekeza leo na wakifanikiwa kuendesha biashara zao kwa faida maana yake ni kwamba baada ya miaka 20, Tanzania itakuwa na watu wenye nguvu na wenye uchumi imara, na kwa kuwa sekta binafsi ni injini ya kukua kwa uchumi wa nchi, tutatoka kwenye kundi la nchi maskini zaidi duniani. Pia, ni rahisi sana kwa kijana kufanya jambo la kubahatisha ama kuthubutu (kubeba ‘risk’) na kufanya kazi kwa bidii kufikia ndoto zake bila wasiwasi, na zaidi kundi hili likipewa kipaumbele linaweza kuondoa utamaduni wa watanzania kutoka kwenye kufanya mambo kwa mazoea (yaani 'business as usual' na 'laissez-faire') na kuwa nchi ya watu wenye kufanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu na ‘passion’ ya ukweli. Mimi naliona hili ndiyo kundi pekee litakaloweza kuijenga Tanzania mpya, Tanzania ya miaka 20 ijayo. Sina nia ya kuonekana ni mbaguzi wa wazee, ama simaanishi kuwa wazee hawahitajiki, la hasha, napenda kusema tu kuwa mpango huu ni mahsusi kwa vijana tu.

Mhe. Spika, ni lazima tuwe na ndoto. Na pia ni lazima tujipange kuzifikia ndoto zetu. Hakuna ujanja mwingine. Hatuwezi kufanikiwa kwa kutumia mikakati ile ile iliyotufikisha hapa. Ni jambo moja kuwa na ndoto, na ni lingine kujipanga namna ya kuifikia. Ni jambo lisiloyumkinika kupanda bangi na kujiandaa kuvuna mchicha hatimaye! Tunahitaji kubadilika, tupande mbegu za kuuandaa uchumi wa Tanzania ya kesho. Tunahitaji mawazo mapya , njia mpya za utekelezaji, na hapo ndipo tutaona matokeo mapya!
Mhe. Spika,

Baada ya maelezo haya, hoja yenyewe sasa inawasilishwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 54 (1.), (2.) na (3.), kama ifuatavyo: -

KWA KUWA, idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania (zaidi ya asilimia sitini) ni vijana chini ya miaka 40
NA KWA KUWA, vijana hawa ni nguvu kazi ya kutegemewa katika nchi yetu na kama kila kitu kitabaki sawa (ceteris paribus), kibaiolojia vijana hawa watakuwepo nchini kwa miaka mingi ijayo ukilinganisha na wazee

NA KWA KUWA, vijana wanahangaika kutafuta ajira na kuna fursa nyingi za kutengeneza ajira nchini ambazo hazijafanyiwa kazi

NA KWA KUWA, vijana wengi nchini humu wamedhihirisha kuwa wana ari, nguvu, nia, elimu, ujuzi na vipaji vya kupigiwa mfano kwenye fani mbalimbali na wanakosa mitaji na mpango mahsusi na wa maksudi wa uwezeshi, wanahitaji uongozi (leadership, mentorship and guidance) ili kukamilisha ndoto zao

NA KWA KUWA, tuna malengo ya kuivusha nchi yetu kiuchumi kufikia 2025 (cf. dira ya maendeleo Tanzania 2025) kuelekea nchi zenye uchumi wa ngazi ya kati (MICs), wengi wa watakaokuwepo (kibailojia) watakuwa ni vijana, na wanatakiwa kuwezeshwa ili wawe mhimili wa mwenendo wa uchumi wa Tanzania ya kesho tunayoilenga, na pia wakiwezeshwa leo tunaamini ndiyo wataifikisha Tanzania huko tunapopataka kesho

NA KWA KUWA, ili kuzalisha ajira nyingi zaidi na kwa haraka, kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja (backward linkage) na kilimo ndiyo jibu la msingi la nia hiyo

NA KWA KUWA, ilani ya uchaguzi ya CCM (Uk. 88 - 95, Kifungu Cha 79 (i.), (ii.) na (iii.)), ambacho ni Chama kinachotawala nchi yetu, inatambua na kutoa maelekezo mazuri kabisa kwa serikali kuhusiana na hoja hii ya kukuza ajira kwa vijana, na pia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (cf. Uk. 92, kifungu cha 5.2.4), na MKUKUTA II vinatambua umuhimu wa kutekeleza haya. Pia Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye maelezo yake ya utangulizi mwanzo wa Mpango huo anasema na ninamnukuu hapa, kwamba “Employment creation, particularly for the youth, is also a critical cross-cutting target of this Plan.” [inatafsirika Kiswahili kama ‘kutengeneza ajira, hususan kwa vijana, ni lengo mtambuka la huu mpango’]. Kinachotakiwa sasa si kingine bali ni kufanya jitihada za utekelezaji tu maana barabara zote zinaelekea huko.

HIVYO BASI, bunge linaazimia kuitaka serikali yetu ifanye yafuatayo:
  1. KWAMBA, Ianzishe mpango maalum wa kukuza ajira kwa vijana kwa kuanzisha mfuko wa mikopo ya vijana wanaowekeza kwenye kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja (backward linkage) na kilimo. Mfuko huu hapo baadaye utaendelezwa na kuwa Benki ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (Tanzania Youth Development Bank).

  1. KWAMBA, Ianzishe mfuko maalum wa kutoa mikopo ya uwekezaji kwa vijana wa Tanzania, utakaoitwa ‘Tanzania Youth Enterprise Challenge Fund’ na iwekeze katika mfuko huu mtaji usiopungua bilioni za kitanzania mia mbili (mwaka wa kwanza) na bilioni mia moja kila mwaka wa fedha utakaofuata. Mfuko huu uwalenge vijana watakaowekeza kwenye sekta ambazo tutazichagua, sana sana tuweke kipaumbele kwenye sekta za kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja (backward linkage) na kilimo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi kwa vijana. Vijana hawa waingizwe kwenye mashindano ya kuandika maandiko ya miradi (project proposals/business plans), na ile itakayoshinda kwenye mchakato huu ndiyo pekee itakayochaguliwa. Mchakato huu katika hatua Fulani, kama itabidi iwe hivyo, uwashirikishe wananchi kwa njia ya kupigia kura miradi wanayoona inafaa na ushindi katika hatua hii iwe ni kigezo kimojawapo cha kuwapata watakaoshinda.
 NA KWAMBA, Mikopo itakayotolewa katika mchakato huu itakuwa ni yenye masharti nafuu, kama ifuatavyo:
·         Itakuwa na riba ndogo (asimilia 6 kushuka chini),
·         Itakuwa na kipindi kirefu cha kurudisha (payback period)  - cha takriban miaka 15-20,
·         Itakuwa na kipindi kirefu cha kutoanza kurudisha mkopo (grace period) – kati ya miaka miwili hadi mitatu
·         Isiwe na masharti ya dhamana/security za mali (maana vijana hawana assets zozote) bali iwe na ‘dhamana’ maalum kama cheti cha elimu/ujuzi kwenye fani husika, ardhi ya shamba lililorasimishwa kwa utaratibu unaokubalika, na iwe kwenye usimamizi wa kitengo maalum cha mfuko huo. Mpango huu uendane na kuweka utaratibu mzuri na rahisi wa kusajili mashamba na ardhi.

  1. KWAMBA, Itenge maeneo maalum ya kuwekeza (special economic zones) chini ya mpango huu. Ichague maeneo maalum kwa mazao na viwanda maalum kwenye wilaya mahsusi za nchi yetu. Vijana waelekezwe na kusimamiwa kuwekeza kwenye sekta zilizochaguliwa na wawezeshwe kupata mitaji hiyo. Uanzishwaji wa miradi hii uendane na kuwepo kwa sharti la kuwataka vijana (wawekezaji) kuhamasisha kilimo cha kisasa na kusaidia wakulima kwenye maeneo yanayowazunguka kwa njia ya mkataba maalum (contract farming) wa kukopesha pembejeo za kilimo, mbegu bora za mazao, zana za kilimo ama kuwalimia na kuwavunia kwa mashine, kutengeneza mifumo ya umwagiliaji – hii itasaidia kuongeza tija na ufanisi kwa wakulima.

  1. KWAMBA, serikali iamue kuchagua sekta zitakazohusika kwenye mpango huu maalum kwa ajili ya vijana. Baadhi ya sekta za kuangaliwa ni pamoja na kilimo kikubwa cha kibiashara cha umwagiliaji – kila mradi ni lazima uwe na mpango wa kuwafikia wakulima wadogo wanaozunguka shamba husika (satellite out-grower schemes), ujenzi wa viwanda kama vya kuchambua pamba (ginneries) na kusokota nyuzi (spinning); kukoboa na kusaga unga/chakula cha mifugo; kukamua na kusafisha mafuta ya kula, pia kutengeneza sabuni; kusindika juice n.k, utafanyika kwenye maeneo ya karibu na mashamba hayo. Kila eneo la mradi litengwe likiwa na uwezekano wa kufanya utanuzi kwenye sekta hiyo ili kukamilisha mnyororo wa thamani kwenye  eneo moja (value chain).
Mhe. Spika,
NAOMBA KUTOA HOJA.


Dr. Hamisi Kigwangalla (MB),
Jimbo la Nzega.