MSIMAMO WA MBUNGE WA NZEGA KUHUSU POSHO

Monday, December 12, 2011
Kufuatia kuwepo kwa mjadala mzito wa kitaifa kuhusu ongezeko la posho ya kikao (Sitting allowance) ya wabunge kama ilivyoongezwa siku za karibuni, ofisi ya Mbunge wa Nzega imelitafakari suala hili na kuona umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi wa jimbo la Nzega na watanzania kwa ujumla kuhusiana na msimamo wa Mhe. Mbunge. Tamko hili linazingatia maswali mengi kutoka kwa wapiga kura wa jimbo la Nzega na baadhi ya watanzania waliotaka kujua nini msimamo wa Dr. Hamisi Kigwangalla, MB (Nzega, CCM) kuhusu posho, hususan ongezeko hili la kutoka 70,000 hadi 200,000.

Mbunge wa Nzega ana msimamo ufuatao:

Kwamba, posho ama ujira wa mwia, ni malipo halali ya kazi ya Mbunge na kwamba ongezeko lolote litakalofuata kanuni na taratibu za haki na usawa kwa watu wote litakuwa halali.

Kwamba, Ongezeko hili kama lilivyotamkwa na Mhe. Spika Anna Makinda (MB), limekuja kutokana na ongezeko la ukali wa maisha katika mji wa Dodoma linaleta mashaka na utata mkubwa kuhusiana na uhalali wake, linaonesha usaliti wa wabunge kwa wananchi waliowachagua na linaiaibisha taasisi ya Bunge kama mtetezi wa wanyonge na mdhibiti na msimamizi mkuu wa serikali. Mbunge wa Nzega anaamini kwamba sababu hii inawakimbiza wabunge mbali zaidi na wananchi na kwamba ni kweli kuna mfumuko mkubwa wa bei lakini hauwagusi wabunge tu pekee yao, unamgusa kila mtanzania, na kama ofisi ya Rais inaona umuhimu wa kuboresha hali ya maisha ya wabunge, basi ingewapandishia mishahara yao, ingewaongezea mafuta ya gari kwa ajili ya kufanyia kazi zao, ingeboresha mfuko wa jimbo, ingeboresha ofisi zao n.k. Kwa hakika kabisa, kwa sababu zilizotolewa na Mhe. Spika, posho iliyopaswa kuongezwa siyo posho ya kikao bali ni posho ya kujikimu. Na hata kama Mhe. Spika alikuwa na nia ya kuongeza posho ya kikao, basi kwa vyovyote vile sababu isingekuwa hii ya ukali wa maisha mjini Dodoma, maana hauongezeki kwa wabunge peke yao tu!

Kwamba, kwa kuwa sababu za kuongezwa kwa posho ya kikao haziendani na malengo ya uwepo wa posho hiyo, basi wabunge wote waungane mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Kabwe, Mbunge wa Bumbuli Mhe. January Makamba na Mbunge wa Nzega Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Nzega) waikatae posho hii ili kuwatendea haki watanzania wanaohangaika kutafuta mkate wao wa kila siku. Kuna madaktari wanakesha usiku kucha na wanalipwa posho ya on call allowance ya TZS 10,000 tu, kumlipa Mbunge posho ya 200,000 haijengi mazingira ya usawa ya kuugawana umaskini wa nchi yetu.

Kwamba, ili kupunguza visingizio vya wabunge kudai maslahi makubwa zaidi kwa kuwa wanaombwa sana amisaada na wapiga kura wao, ofisi ya Bunge ianzishe kitengo cha kutoa elimu kwa umma kuhusu kazi na majukumu ya Mbunge ili kuwaelimisha wananchi kwamba kusaidia matatizo binafsi siyo kazi yao na hivyo wasihukumiwe kwa kutokutoa misaada bali kwa kuisimamia serikali ipasavyo.


Tamko hili limetolewa leo Tar 12/12/2011 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB).