Dk Kigwangala awakaba Resolute
Mwananchi, Jumatano Desemba 1, 2010
Na Mustapha Kapalata, Nzega
MBUNGE wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangala, amesema mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Nzega Golden Pride Mine Ltd, hauna manufaa na wananchi wa jimbo hilo.
Kauli ya mbunge huyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kuanza kutumikia wananchi, akianzia ziara yake kwenye mgodi huo.
Dk Kigwangala alifanya ziara ya kushtukiza mgodini hapo jana na kukutana na Meneja Mwendeshaji, Les Taylor, akimtaka kueleza jinsi wananchi wanavyonufaika na mgodi huo.
Hatua ya Mbunge inatokana na kero kubwa ya maji inayowakumba wananchi wa Nzega. Hivi sasa plastiki la lita 20 za ujazo linanunuliwa kwa sh 1,500.
Mbunge huyo alisema mgodi huo hauna msaada kwa wananchi wa jimbo hilo kwani, uongozi wa mgodi huo hautoi huduma muhimu kama maji kwa wananchi, ilhali wanaendelea kukausha vyanzo vya maji.
Dk Kigwangala alisema uhusiano wa wawekezaji hao na wananchi wanaozunguka eneo hilo, ni sawa na chui na paka, hawaelewani kutokana na utawala wa mgodi huo unaodharau raia kwenye nchi yao.
Alisema mikataba iliyofungwa enzi hizo siyo yakinifu ambayo itanufaisha wananchi wa Nzega na watanzania na kwamba, inalenga kunufaisha watu binafsi.
Kuhusu mrahaba unaolipwa kwa halmashauri wa sh 200 milioni kwa mwaka, Dk Kigwangala alisema kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na rasilimali wanayovuna.
"Kwa kweli kama mbunge, mikataba hii ni ya kihuni , siridhishwi nayo hata kidogo, kiwango wanachotoa ni bora wangechimba bure. Hawana msaada kwa watu wa taifa hili, wanachokifanya ni kuongeza umaskini, naheshimu sana mikataba lakini huu siridhiki nao," alisema Dk Kigwangala.
Alisema muda wa uchimbaji kwa mgodi huo unakaribia kumalizika na wananchi wataachiwa mashimo, yenye madhara makubwa kwa afya zao, huku akimtaka meneja huyo kurekebisha haraka uhusiano wao na wananchi.
Kwa upande wake, Taylor alimshutumu mbunge huyo kwa kufanya ziara isiyo rasmi na kwamba, alitakiwa kutoa taarifa kama mbunge kuingia mgodini.
Taylor alisema malalamiko ya wananchi kuhusu uhusiano siyo kazi ya mgodi, bali serikali ambayo inatakiwa kutimiza ahadi zake.
Alisema kampuni inatoa msaada pindi inapoguswa na tatizo, siyo lazima na halihusiani na mkataba wao.
Awali, Dk Kigwangala alitembelea vyanzo vya maji na Meneja wa maji wilaya ya Nzega, Samuel Buyigi, akimweleza kutokuwepo kwa uhusiano mzuri na mgodi huo ambao unakausha vyanzo vya maji.
Buyigi alisema mgodi huo unachukua maji kutoka vyanzo vya maji na kwamba, vingine vimeanza kukauka, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi.
Subscribe to:
Posts (Atom)