OFISI YA MBUNGE, JIMBO LA NZEGA
Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (MB)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tunapenda kuutarifu umma kwamba Mhe. Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesikitishwa sana kupata taarifa kutoka baadhi ya vyombo vya habari kuwa anatajwa kuchochea mgomo wa madaktari. Hata siku moja hajawahi kuwa mchochezi wa mgomo huu na yeye binafsi siku zote amekuwa mstari wa mbele kusema ukweli na kuweka hadharani msimamo wake na wala siyo kuchochea kwa kificho chini kwa chini.
Pia kuna gazeti moja la kila wiki limeandika jana stori (kwenye ukurasa wake wa mbele) kuwa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla ‘anatajwa kuchochea mgomo huo kwa malengo ya kuutaka uwaziri.’ Vyombo vingi vya habari vikivutiwa na kichwa hiki cha habari vimekuwa vikimpigia simu Mhe. Mbunge kumtaka atoe ufafanuzi. Mhe. Mbunge amesikitishwa sana na taarifa zilizoandikwa kwenye gazeti hili na tayari Mwanasheria wake ameanza kujipanga kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaka gazeti hili limsafishe kwenye jamii kwa kuchapisha habari ya kumsafisha ama lipelekwe mahakamani.
Kwa taarifa hii tunakanusha ushiriki wa aina yoyote ile unaotajwa kumhusisha Mbunge wa Nzega kwenye uchochezi ama wa namna yoyote ile inayofikirika zaidi ya msimamo ambao Mhe. Mbunge Dkt. Kigwangalla amewahi kuuweka wazi siku za nyuma kwenye mikutano ya wazi ya madaktari au kwenye vyombo vya habari. Pia ifahamike kuwa kwa kuweka wazi msimamo wake kwamba madaktari wana madai ya msingi na hivyo wasikilizwe (ambayo kwa sasa serikali ilishakiri na kuyakubali madai yao na kutamka hadharani kuwa inayafanyia kazi) haimaanishi kuwa ni uchochezi bali ni matumizi ya haki za msingi za binadamu kama zilivyoainishwa kwenye Kati ba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenye mikataba mbali mbali ya kimataifa ya haki za binadam.
Na pia tunapenda kuwataarifu wanahabari kuwa Dkt. Hamisi Kigwangalla hajahudhuria mkutano wowote ule wa madaktari uliopelekea madaktari kuazimia kugoma tena na hivyo kumhusisha na ushawishi ama uchochezi ni kupotosha umma na kuvunja sheria. Na zaidi kufikiria kuwa madaktari nchi nzima wanaweza kugoma kwa kumsikiliza mtu mmoja tu ni kuwatukana na kuwadhalilisha kwa kuwaona hawana uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi yao, ilhali hawa ni watu makini, wenye elimu na ujuzi wa hali ya juu na wengi wao wanamshinda elimu, ujuzi na uzoefu kwa mbali sana Mhe. Mbunge Dkt. Kigwangalla. Hali kadhalika, Mhe. Dkt. Kigwangalla aliomba Ubunge na hakutarajia kuwa angepewa Uwaziri na ni wazo la kitoto kufikiria kwamba mtu mwenye busara zake na hadhi yake kama yeye angeweza kupanga mkakati wa kumn’goa Waziri yeyote Yule ili awekwe yeye, maana kwanza hana muamana na mamlaka ya uteuzi, ambayo kimsingi ndiyo yenye uamuzi wa kumteua nani na kumuondoa nani, na pia haiyumkiniki kuwa eti ‘uwe mstari wa mbele kuvumbua maovu na mapungufu ya kiutendaji ya mtu ambaye unataka atolewe kwenye nafasi ili wewe uwekwe hapo!’ Kwa namna yoyote ile kama Dkt. Kigwangalla angekuwa anaitaka nafasi ya Uwaziri asingeunga mkono madai ya madaktari. Na kwamba kama kuna mtu ana Taarifa zozote zile zinazoweza kuthibitisha kuwa amekuwa akipanga mikakati ya kutafuta Uwaziri basi aziweke wazi na Mhe. Mbunge atakuwa tayari kujivua nafasi zake zote za uongozi alizonazo.
Mhe. Mbunge anawashauri waandishi wa habari kuwa waandike taarifa ambazo wana uhakika nazo tu na wasikubali kutumiwa na makundi ya wana siasa wenye malengo ya kuchafua wenzao.Mwisho, mara zote toka mgogoro huu baina ya madaktari na serikali uanze, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) amekuwa akishauri pande zote mbili zikutane, zijadiliane na kutafuta suluhu ya matatizo yaliyopo, na leo hii tena bado anasisitiza kuwa njia pekee sahihi na sawia ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu ni kuzungumza na kuelewana kwenye mambo ya msingi. Hii ndiyo njia pekee itakayoepusha adha kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya, ambao wao ni waathirika wasio na hatia.
Imetolewa Leo Tar 8/Machi/2012 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega.
No comments:
Post a Comment