Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? Taarifa ya
Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013.
Utangulizi
Ukiitazama Nzega
ya leo si ile Nzega ya Miaka ya 90 ama ile ya miaka ya 70, alipozaliwa Mbunge
wetu Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), imebadilika sana, imekuwa kwa kasi sana;
idadi ya watu, magari na nyumba imeongezeka sana. Utoaji wa huduma zote muhimu umezidiwa
kasi na ukuaji wa mji. Changamoto zilizopo leo ni nyingi na nzito sana. Kuna shida
kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, shule ni chache na zinatoa elimu
isiyokidhi ubora unaohitajika, viwanda hakuna
ukilinganisha na miaka ya nyuma, migodi midogo midogo iliyokuwa asili ya
Nzega imefungwa na serikali, mvua zimepungua kutokana na uharibifu wa mazingira
hivyo uzalishaji wa mazao ya biashara na kilimo umeathiriwa sana ukilinganisha na
miaka ya nyuma, miundombinu ya barabara imeongezeka kwa wingi haswa maeneo ya
vijijini na mijini japokuwa bado ni duni na haitoshi na pia huduma za kibenki
ni duni na hazijawafikia wananchi walio wengi kule vijijini.
Pamoja na
mapungufu haya Nzega inafaidika kwa kuwa kwenye nafasi nzuri kijiografia,
kwamba ni makutano ya barabara kuu ziendazo Kigoma, Kagera hadi Rwanda na
Burundi na ile inayokatiza kwenda Mwanza hadi Musoma na Tabora hadi Mbeya. Kama
zikiunganishwa kwa lami, Nzega inaweza kuwa kituo muhimu kwa biashara. Pia nafasi
yake kijiografia imefanya Nzega iwe na mchanganyiko mzuri wa watu kimakabila
kiasi kwamba mchanganyiko huu unatoa fursa ya kuleta uzoefu na ujuzi mbalimbali
kutoka sehemu mbalimbali ambao unapafanya Nzega pawe mahala palipochangamka (vibrant
and dynamic).
Mwaka 2010,
kwenye uchaguzi Mkuu, Nzega ilifanya uamuzi sahihi wa kumchagua Mbunge mwanamapinduzi,
mwanamabadiliko na mpiganaji mahiri na makini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.)
ambaye anajitahidi kupambana na changamoto hizi usiku na mchana pasi na kukata
tamaa ama kuchoka. Mafanikio ya kazi yake yanaonekana na siyo ya kutafuta.
Ifuatayo ni ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla (Mb.) hadi kufikia Desemba 2013.
1. Hali ya Jimbo
Hali ya jimbo ni
shwari; amani, upendo na usalama umetamalaki japokuwa mpaka tunaandika taarifa
hii kuna malalamiko ya watu wa kijiji cha Mwanshina, ambako kuligundulika uwepo
wa dhahabu hivi siku za karibuni na kupelekea wananchi kujumuika pale kuanza
shughuli za uchimbaji; bahati mbaya sana wamezuiliwa na askari wa kutuliza
ghasia (FFU) waliopokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega.
Mazungumzo yanaendelea kujua ni kwa nini serikali imewazuia wananchi hawa ili hatma
ya mgodi huu ijulikane. Pili, kuna malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Ipala
ambao wanadaiwa na serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega kuvamia
eneo la msitu wa hifadhi. Ufuatiliaji wa uhalali wa katazo la Mkuu wa Wilaya ya
Nzega lililoambatana na uvunjifu mkubwa wa haki za wananchi, ambapo wamedumu
toka kabla ya uhuru, unaendelea.
Ofisi ya Mbunge
wa Jimbo la Nzega imeendelea kuhudhuria shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo
harusi, misiba, mahafali za wanafunzi, harambee na pia kufanya ziara za kikazi
kijiji kwa kijiji kupitia ‘Operesheni Wafuate Watu’. Pia ahadi za Mbunge ama
wasaidizi wake kwenye maeneo mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa – hadi sasa ni
zaidi ya asilimia 95 ya ahadi zote alizotoa mbunge zimetekelezwa ukiachilia
chache sana ambazo ni za siku za karibuni. Kuna ligi kubwa ya kiwilaya
inayofadhiliwa na Mbunge wa Nzega inaendelea katika hatua ya robo-fainali
kwenye tarafa nne za Wilaya ya Nzega – mshindi wa kwanza atapata ‘Kombe la Kigwangalla’ na fedha taslim TZS
1,000,000, wa pili atapata TZS 500,000 na wa tatu TZS 300,000. Timu zote
zilizoingia nane bora zitazawadiwa seti moja ya jezi kila timu.
Mbunge wa Nzega
anaendelea kupigana kuhakikisha azimio la Baraza la Madiwani la kuanzisha
Kampuni ya Benki Jamii ya Nzega (Nzega
Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation
Ltd - NCCCL) linatekelezwa haraka. Tunatarajia mchakato huu utafanikiwa
kutokana na uwepo wa takriban TZS 2.3 bilioni zilizopatikana kutoka kampuni ya
Resolute Tanzania Ltd kama ushuru wa huduma (service levy) na ambazo zitatumika
kama mtaji wa kuanzia wa benki (TZS bilioni 1) na zinazobaki kwa ajili ya
kununulia mashine za kuchongea barabara na kuchimbia visima zitakazomilikiwa na
kuendeshwa na kampuni hizi mbili tofauti ambazo zinatarajiwa kuanzishwa kwa
ushirikiano baina ya Halmashauri, wanaushirika na wananchi wengine watakaopenda
kununua sehemu ya hisa za makampuni haya mawili.
2. Vipaumbele Vya Jimbo
2.1
Mapinduzi
Kwenye Sekta ya Elimu Nzega:
(i.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, mpaka sasa kwa kufanya jitihada binafsi na
kwa kutumia pesa za mfuko wa jimbo (milioni 43) akishirikiana na Diwani, Mhe.
Ramadhani Nchimani, Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ndala, Serikali ya Kijiji
cha Kampala na wananchi kwa ujumla, ameanzisha ujenzi wa shule mpya ya ‘high school’ (kidato cha tano
na cha sita) pale Kampala, Ndala (Shule hii imepewa jina la Chief Ngelengi High School); ujenzi
unaendelea kwa kasi hivi sasa. Shule ya
pili ya High School itakuwa ni ile ya Chief
Ntinginya, ambapo Mbunge wa Nzega Dkt. Hamisi Kigwangalla, kufuatia
makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nzega Mjini chini ya Diwani na
Mwenyekiti wake Mhe. Kizwalo Dominic waliazimia kuanzisha ujenzi wa mabweni na
madarasa ya ziada ili kuipandisha hadhi shule hii iwe ya kidato cha tani na cha
sita. Shule ya tatu ya High School inamaliziwa
kujengwa Kata ya Puge, Tarafa ya Puge kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge
(ambayo imetoa sh milioni 13), Diwani Mhe. Alex Nyassani, Serikali ya Kijiji
cha Upungu na wananchi kwa ujumla (ambao walianzisha majengo hayo); pia
Halmashauri ya Wilaya tayari, kwa ushawishi wa Mbunge wa Nzega na Diwani wa
Kata ya Puge, imetenga fedha taslimu sh milioni 28 kwa ajili ya kumalizia
ujenzi wa shule hiyo. Shule ya Nne ya
High School inamaliziwa kujengwa kule Kata ya Lusu (pale Hamza Azizi Ali
Sekondari) na wawekezaji wa mgodi, Kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, kufuatia
jitihada za kiufuatiliaji na ushawishi wa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) na
Mhe. Said Mgalula (Diwani, Lusu) wakishirikiana na wananchi, kwamba ni lazima
mgodi ujenge miradi ya maendeleo ya jamii kabla haujafungwa. Ni matarajio yetu
kwamba shule hizi zitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi kabla ya mwaka 2014
kuisha. Tunawaomba wananchi wote kwa ujumla, wadau mbalimbali wa maendeleo na
serikali tutimize wajibu wetu, tumuunge mkono Mbunge wetu tulete mapinduzi ya
kielimu Nzega.
(ii.)
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na shirika lisilo la
kiserikali la PeerCorps Trust Fund ameweza kuanzisha mpango wa kusomesha watoto
yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni, mfuko huu unaoitwa Hamisi Kigwangalla Scholarship Fund
ulianzishwa mwaka 2008 na umeendelea kusomesha watoto na kutoa misaada
mbalimbali ya kielimu. Mpaka sasa zaidi ya watoto 576 wamefaidika na mpango
huu. Na kila kata kuna wanafunzi 10 kutoka katika makundi haya wanalipiwa ada
chini ya mpango huu. Japokuwa mfuko unakumbana na changamoto nyingi ikiwemo
kupata maombi mengi zaidi ya uwezo wa mfuko na kuna baadhi ya kata mpaka sasa
mfuko haujaweza kupata fedha za kulipa ada kwa baadhi ya wanafunzi, japokuwa
Mhe. Mbunge anawataka walimu, wazazi/walezi na viongozi wa Kata hizo wawe
wavumilivu na kwamba ada hizo zitalipwa kabla watoto hao hawajahitimu kwa kuwa
majina yao tunayo na yaliishapitishwa kufaidika na mpango huu.
(iii.)
Mwezi Januari mwaka 2014 Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, atauanza
mwaka kwa kuendelea kugawa vitabu 100 vya Kiada na 50 vya ziada kwenye shule
zote za Sekondari za Kata za Jimbo la Nzega pamoja na Kompyuta kwenye shule 5
za sekondari kama ambavyo amekuwa akifanya toka achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo
hili.
(iv.)
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha tamasha la utamaduni wa watu wa
Nzega litakalokuwa likifanyika kila mwaka mjini Nzega. Tamasha hilo ambalo
linaitwa Mtukwao Festival (www.mtukwao.org) litakuwa ni kivutio cha watu
na kuleta fursa ya biashara kwa wakazi wa Nzega, na sehemu ya kuitangaza Nzega
na utamaduni wake kwa wageni, tayari limepata usajili wa serikali na maandalizi
yanafanyika kulizindua mnamo Julai 2014 kwa mara ya kwanza, baada ya mipango ya
kulizindua Julai 2013 kama ilivyotangazwa hapo awali kushindikana.
(v.)
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha ujenzi wa chuo binafsi mjini
Nzega eneo la Uchama kitakachokuwa kinatoa wahitimu kwenye fani za Uganga,
Uuguzi na Ualimu kwa ngazi za Vyeti na Stashahada ili kuongeza nguvu kazi
kwenye shule za sekondari za kata, zahanati na vituo vya afya. Malengo ni
kusomesha bure walau wanafunzi watano - kwenye kila kozi, wasio na uwezo, mbali
na wale wanaojilipia, kwa makubaliano ya kuhakikisha wanaajiriwa kwenye wilaya
ya Nzega kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Hii itaongeza idadi ya
watumishi kwenye huduma muhimu kwa wananchi na pia uwepo wa chuo utakuza fursa
za kiuchumi na ukuaji wa taswira ya mji wa Nzega. Tunatarajia chuo hiki kitakamilika
na kuanza kudahili wanafunzi mwaka 2014 Mwezi Septemba.
2.2 Kuendesha Harakati za Kupigania Haki na Usawa kwa wanaNzega:
Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi
Kigwangalla, akishirikiana na wananchi wa Nzega, madiwani na watendaji wa
halmashauri ameongoza mapambano ya kudai haki za Nzega dhidi ya wawekezaji wa
Mgodi wa Golden Pride Project, kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, na kufanikiwa
kupata mafanikio yafuatayo: mgodi umekubali na tayari umelipa sh bilioni 2.34 kama ushuru wa huduma
(service levy) kwa halmashauri ya wilaya ya Nzega, bado kuna madai ya sh
bilioni 4 za ushuru wa huduma yanayoendelea kufuatiliwa, ambazo ni malimbikizo
ya ushuru huo toka mgodi uanzishwe takriban miaka 14 iliyopita; amefanikiwa
kuishawishi serikali kuwa wananchi waliopoteza mali zao kutokana na uharibifu
uliofanywa kupisha mgodi wana haki ya kifuta jasho na sasa serikali inaungana
na Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kuwabana wawekezaji waanzishe mfuko wa
kuwahifadhi wananchi hao; na jambo kubwa la tatu ni kwa kutumia nguvu ya umma
kushawishi wawekezaji watekeleze ahadi za kujenga miradi ya maendeleo Nzega
(Kituo cha Afya Lusu, Maabara kwenye sekondari 10 n.k.). Mbunge wa Nzega
ataendelea kushawishi vikao vya halmashauri na kusimamia utekelezaji wa miradi
itakayowagusa wanaNzega wengi zaidi, kama vile kuanzisha benki ya jamii ya watu
wa Nzega ambayo itatoa mikopo kwenye SACCOS za kila kata, kununua mitambo yetu
wenyewe ya kuchimbia visima kwenye kila kijiji, kujenga soko jipya na stendi
mpya kubwa ili kukuza fursa za biashara ndogondogo kwa wananchi n.k. Mhe.
Mbunge amekuwa akipigana bega kwa bega na wananchi wa Kijiji cha Mwabangu
kuhakikisha wanapata haki ya kupatiwa leseni yao iliyopokwa kinyemela na
wajanja wachache kwa faida yao ama fidia ya ardhi ya mgodi wa wachimbaji wadogo
wadogo wa Isungangwanda.
2.3 Kuwezesha Wananchi Kushiriki Shughuli Mbalimbali za Kukuza Kipato
Chao: Mbunge wa Nzega, Mhe.
Dkt. Hamisi Kigwangalla, amefanikiwa kuleta mapinduzi ya kijani kwenye
kilimo cha zao la pamba na zao la alizeti kupitia uhamasishaji wa kampuni ya
MSK Solutions Ltd ambayo inatoa mbegu bora, pembejeo, zana za kilimo, elimu ya
kilimo bora na uwezeshaji wa wagani vijijini, soko la uhakika la mazao hayo na
ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao vijijini (Imekamilisha ujenzi wa maghala
kule Ndekeli (Tarafa ya Puge), Igalula (Tarafa ya Mwakalundi), Nhabala (Tarafa
ya Bukene) na imeanza ujenzi wa ma-godown mapya kule Nhobola (Tarafa ya Nyasa)
na Usongohala (Tarafa ya Bukene). Mafanikio ni kuongezeka kwa wakulima wa pamba
kutokea wakulima 355 mwaka 2008 hadi kufikia wakulima 24,000 wa pamba mwaka
2012 na kufanya idadi ya kilo za pamba zilizovunwa kufikia takriban milioni 6
kutoka kilo 20,000 mwaka 2008. Pia idadi ya wakulima wa alizeti imeongezeka
kutoka wakulima 400 mwaka jana hadi kufikia 3500 mwaka 2013.
Makampuni ya wanunuzi wa pamba
yameongezeka kutoka kampuni moja ya MSK na kuwa manne hivi sasa – hali
inayoleta ushindani kwenye soko na hivyo kupandisha bei zaidi kwa faida ya
mkulima. Japokuwa kampuni ya MSK Solutions Ltd imeamua kuacha kuhamasisha pamba
na kujikita zaidi kwenye alizeti itaendelea kukumbukwa kwa kutia chachu
uhuishaji wa kilimo cha zao hili kilichokuwa kimekufa.
Mipango inaendelea kuwashawishi
wawekezaji wajenge viwanda vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya kula kutokana
na alizeti ya Nzega, tayari halmashauri ya Nzega imeazimia kutenga viwanja 10
kwenye eneo maalum la kujenga viwanda. Pia Mbunge wa Nzega amewezesha wananchi
kujiunga katika vikundi vya ushirika wa SACCOS vipatavyo 9 na yupo kwenye
harakati za kuvijengea uwezo vifanye kazi za kukuza uchumi kama vile kilimo,
mifugo ya kuku kwa kuzalisha vifaranga na mayai, na shughuli za ufundi kwa
vijana. Mbunge wa Nzega amegawa mashine mbili kwenye SACCOS ya vijana nay a wazee
kwa ajili ya kuangulia vifaranga. Ili kuhakikisha chama kinakuwa mstari wa
mbele katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo vijijini, Mbunge wa
Nzega akishirikiana na mwenzake wa Bukene wamegawa mbegu za alizeti kwenye kila
kata. Pia Mbunge wa Nzega amegawa pikipiki 10 kwenye kata 10 ili kuweka urahisi
zaidi wa kufikisha huduma za ushauri wa maendeleo kwa wakulima vijijini.
2.4 Ujenzi wa Miundombinu Nzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameweza
kushawishi vikao mbalimbali vya maamuzi na kuhakikisha azimio la kujenga
barabara za lami Nzega Mjini linafanikiwa, hivi sasa tayari bajeti imetengwa
kwa ajili ya kutekeleza hilo kwenye mwaka wa fedha wa 2013/14; pia kufunga
mataa ya kuangaza mji mzima wa Nzega. Mbunge wa Nzega pia kupitia mfuko wa
Jimbo amejenga daraja korofi na lililosahaulika kwa muda mrefu la Butandula, na
sasa anatafuta namna ya kuhakikisha pia daraja lingine la Nhobola nalo
linajengwa, tayari ametenga sh milioni 8
za mfuko wa jimbo kutekeleza hilo.
Mradi wa barabara ya Nzega – Tabora
kwa kiwango cha lami – Mbunge wa Nzega kwa kutumia nafasi yake kama Makamu
Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Tabora, amekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha serikali inaleta fedha za kukamilisha mradi huu ndani ya muda
uliopangwa na pia kusimamia kuhakikisha barabara hiyo na nyingine za mkoa wa
Tabora, zinajengwa kwa viwango vya ubora unaostahiki, na wananchi wanapata
ajira na kulipwa fidia ya mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi huu.
Pia Mbunge amehakikisha barabara
korofi kama za kutoka Mbagwa – Nkiniziwa, Busondo – Ndekeli, Busondo –
Mwakashanhala zinaingia kwenye bajeti ya ujenzi mwaka huu wa fedha 2013/14 na kuhakikisha
zinajengwa, pia barabara nyingine muhimu kama za Muhugi – Mizibaziba – Ndekeli
– Ndala zinaingizwa kwenye bajeti, lengo likiwa ni kuhakikisha Nzega inakuwa na
mtandao mzuri wa lami mahala pote. Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.)
amefanikiwa kuhakikisha mradi wa kupeleka umeme Ndala kutoka Nzega unatekelezwa
kwa viwango vya ubora unaofaa, na sasa anahangaika kuhakikisha pia maeneo ya
Mbogwe, Wela, Miguwa, na yale ya Usagali, Kaloleni hadi Mirambo Itobo nayo
yanapata mradi wa Umeme. Tayari maombi yake yameingizwa kwenye orodha ya miradi
ya Umeme Vijijini (REA Phase II) na hivyo maandalizi ya awali ya upembuzi
yakinifu yataanza muda wowote kuanzia sasa. Sambamba na jitihada hizi, Mbunge
amefanikiwa kuishauri na hatimaye kuishawishi halmashauri ya Nzega kuanzisha
kampuni ya ujenzi (NCCCL) na kuinunulia mitambo ya kuchongea barabara, mpango
ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.
2.5 Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nzega: Baada ya
kutoridhishwa na namna miradi ya maji ya benki ya dunia na ile ya serikali
inavyosuasua, Mbunge wa Nzega, Dkt.
Hamisi Kigwangalla, ameshauri na hatimaye kuishawishi Halmashauri wanunue
mitambo ya kuchimba visima na kuiweka chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi
Nzega (NCCCL) ili kuondoa yale matatizo kwamba mkandarasi amelipwa achimbe
kisima kimoja akikosa maji basi na pesa ya serikali ndiyo imeishaliwa. Pesa za
kununulia mitambo hiyo zitatokana na mapato yaliyopatikana kutokana na ushuru
wa huduma uliolipwa na kampuni ya Resolute. Tukiwa na mitambo yetu
tutahakikisha tunachimba kisima na maji yanapatikana kwenye kila kijiji bila
shida ndipo twende kijiji kingine. Pia Mhe. Mbunge amekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Tabora unaanza
kutekelezwa – na kwa sasa hatua ya utafiti wa awali ilishamalizika na
tunatarajia upembuzi yakinifu utafanyika mwaka huu na pengine mwakani kuanza
kutekelezwa, ukizingatia hii ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Jakaya Kikwete.
2.6 Upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa Umma: Mhe.
Mbunge, Dkt. Hamisi Kigwangalla,
ameamua kuanzia mwaka 2014 ataweka ratiba maalum ya kutumia taaluma yake ya
udaktari kutibu wagonjwa kwenye vituo mbali mbali vya afya Nzega. Pia ameandaa
mkakati kabambe wa kuleta madaktari bingwa wanaoruka (flying doctors) kwa ajili
ya kuweka kambi ya tiba maalum mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya wananchi wa
Nzega. Kwa kushirikiana na madiwani wenzake wa halmashauri ya Nzega
wamefanikiwa kuhakikisha vituo pamoja na nyumba za walimu zilizoanza kujengwa
na wananchi vinamaliziwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi –
tayari bajeti imetengwa kumalizia vituo vyote mwaka 2013/14, na anaendelea
kuhamasisha vijiji vingine ambavyo havijaanza kutekeleza mpango huu vianze mara
moja ili tubaki tukitafuta namna ya kupambana na chamngamoto nyingine za
watumishi, vifaa na madawa.
N.B: Kuna mambo
mengi yanayofanyika Nzega kwa ushawishi wa Mbunge na Madiwani, yakitekelezwa na
serikali kutokana na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mwaka 2010 – 2015,
lakini si yote yaliyoripotiwa hapa.
Taarifa hii
imetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega, pia inapatikana hapa www.hamisikigwangalla.com na
kigwangalla.blogspot.com
Mhe.
Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb.)
Leo Siku ya
Jumamosi, Desemba 21, 2013.
No comments:
Post a Comment