Hotuba Aliyoitoa Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB (Nzega), Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya TAMISEMI, kwa Waandishi wa Habari Kutangaza Nia ya Kugombea Urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwaka 2015 Kwenye Ukumbi wa Zanzibar, Hyatt
Regency, The Kilimanjaro Hotel, Dar es salaam, Siku ya Tarehe 7 Septemba 2014.
Utangulizi
Ndugu
viongozi mlioko hapa, wazazi wangu, wageni waalikwa, wanahabari, marafiki
zangu, mke wangu na watoto wangu,
Nianze kwa kuwashukuru
viongozi wa dini kwa dua za utangulizi.
Pia nitume salamu
zangu za rambirambi kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Eng. Evarist Ndikilo na
ndugu, jamaa na marafiki wa watu waliopoteza maisha kutokana na ajali mbaya ya
gari iliyotokea juzi. Pia nitumie fursa hii kutuma salamu zangu za rambi rambi
kwa Inspekta Mkuu wa Jeshi la polisi, IGP Ernest Mangu, ndugu wa marehemu na
askari wote wa jeshi la polisi kutokana na uvamizi wa kituo cha polisi kule
Bukombe. Na pia naomba nitumie fursa hii kumpa pole Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi, CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
kwa kupata ajali eneo la Misungwi, Mwanza.
Ndugu zangu
mlioko hapa, ni heshima na furaha kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Awali ya
yote nimshukuru Mwenyezimungu kwa kutujaalia uhai na kutukutanisha hapa siku ya
leo. Pili niwashukuru nyote mliofika hapa kuja kunisikiliza. Niwashukuru zaidi
waandaaji wa Mkutano huu kwa kujitoa na kwa namna ya kipekee niwashukuru wazazi
wangu, mke wangu na wanangu Sheila, Hawa na HK Jr kwa uvumilivu na kwa
kuendelea kunitia nguvu ya kusonga mbele.
Leo nitasema neno zito
kidogo, kama nilivyoahidi siku chache zilizopita. Neno nitakalolisema hapa
litabadilisha sura ya historia yangu milele. Ninawashukuru nyote kwa kuitikia
wito wa kuja kuwa mashuhuda wa namna historia itakavyoendelea kuandikwa hapa.
Kinachotokea hapa leo hii
kina maana kubwa sana kwa watu wenye historia inayofanana na mimi. Wale ambao
wameyajua maisha ya shida na kukosa uhakika toka wakiwa tumboni mwa wazazi wao
kutokana na hali za uchumi wao. Wale wenzangu na mie ambao kesho yao haina
uhakika; wale ambao wengine hupenda kuwaita ‘wanyonge’, ambapo mimi
nikijitazama nilikotoka husema, hapana, hawa si wanyonge bali ni ‘simba
aliyelala.’
Shukrani
Kwa Urithi Toka kwa Waasisi na Wazee Walionitangulia
Mimi ninayezungumza hapa
nimeyajua maisha ya mtu mnyonge na maskini kwa kuyaishi na si kwa kusoma ama
kusikia. Ninajua mtu akiongelea njaa anamaanisha nini, sihitaji kufundishwa,
najua. Nasema haya maana naujua ugumu wa kumuelewesha mtu anayekula milo mitatu
kwa siku, tena ya kujipakulia kuwa kuna wengine wanakula pilau sikukuu hadi
sikukuu. Ni ngumu sana kumuelewesha mtu wa aina hiyo kuwa wapo watoto
wanaogombania chakula kwenye sahani moja. Maana kila siku yeye huwashuhudia
watu wa dunia anayoishi wakihangaika
kutembea umbali mrefu ili wapunguze vitambi na wakae kwenye ‘shape’ na hajui
kama kuna watu wanatembea umbali mrefu ili kutafuta chakula wasukume siku!
Ni katika nchi chache sana
duniani, mtoto mwenye historia ya maisha kama yangu, aliyewahi kutembea mitaani
akiuza karanga, Big G, maandazi na jerebi ili kusaidia wazazi kupata chochote
kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota ndoto ya kuwa Rais wa nchi yake.
Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari.
Hii inamaanisha jambo moja
kubwa, kwamba misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa Taifa
letu haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na inafanya kazi.
Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ama wa kiongozi, ndiyo uoneshe kipaji
chako. Inadhihirisha kwamba, ukipigana ndani ya Tanzania unafanikiwa!
Hili peke yake linanipa
sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kusonga mbele zaidi – nataka niwe mfano hai
wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa sawa bila kujali nani anatokea familia
ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni lazima atokee kiongozi wa
kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania itakayodumu kwenye misingi hii.
Kwamba, ndani ya Tanzania, si lazima mtoto wa mama ntilie awe ‘baba-ntilie’ –
anaweza kuwa mmiliki wa hoteli kubwa ya kitalii!
Kwa namna ya kipekee
nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Taifa letu kwa
kuzilinda tunu hizi, maana ninaamini kuwa hatuwezi kuizungumzia kesho bila
kukumbuka shida na raha tulizopata jana.
Leo nimefika hapa kwa
sababu chama changu kina mfumo mzuri ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa
na wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi tumeukuta. Leo nimefika hapa kwa sababu
Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu
walitumia misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami
nina haki ya kuwa Mbunge. Na leo nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo
hiyo itakayotoa uongozi wa Taifa letu katika awamu ijayo.
Babu yangu mzaa baba
aliishi Kijijini Goweko, eneo la Mlimani, na alikuwa mfugaji mkubwa wa ng’ombe
na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi maisha ya heshima kubwa pale
kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa japokuwa Babu yangu aliwahi kushika
nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU na baadaye CCM katika ngazi ya
Kata.
Babu yangu mzaa mama alikuwa
mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora School miaka miwili
mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini
ya serikali ya wakoloni, na alishiriki harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa
chama cha TAA na baadaye TANU. Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba
kila mtu anastahili heshima na kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na
kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya utawala
dhalimu wa wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na hivyo
alifanya juhudi kusomesha mabinti zake; mama yangu aliishia kwenye ualimu kabla
ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania ya mabinti zake itahitaji
wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa ajili ya mabinti zangu, Sheila na
Hawa, na kaka yao, HK Jr. Ninaamini kila mzazi wa kizazi changu ana ndoto
inayofanana na yangu kwa watoto wake.
Ninaamini historia ya
maisha yangu siku moja itaandikwa na itawasisimua na kuwapa matumaini makubwa
vijana na watoto chini ya miaka 35 ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya watanzania
wote. Mmoja wa wajukuu zangu ataisoma na kusema ‘doesn’t it get better than
this?’
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano
hai wa historia ya maisha ya watanzania
wengi. Na kwamba, nina deni la
kulipa kwa vizazi vijavyo kwa kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na
vizazi vilivyonitangulia. Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo
vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.
Mahusiano
ya Watu na Serikali Yao
Kazi yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu
– vijijini na kwenye majiji,
imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa maskini, wazee kwa vijana –
hakuna hata mmoja kati ya watu hawa anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake
zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na wana nia
ya kufanya hivyo.
Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa
kule Pugu Road viwandani, kwa matabibu wenzangu pale hospitali ya Taifa
Muhimbili, ama kwa wafanyabiashara na wachuuzi pale sokoni Kariakoo, wote
watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na wachache wasio waadilifu.
Watanzania wanataka kupata
huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda kule Nanyumbu, ama
Tandahimba, ama kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali
itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali haitowafanyia kila
kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na wamekuwa
wakifanya hivyo siku zote. Wanachohitaji wao ni kujengewa mazingira wezeshi
kushiriki shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe namna ya kuongeza
uzalishaji kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi,
waelekezwe wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji,
mwisho wa siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa
wala kucheleweshewa malipo.
Watu hawatarajii serikali
itabeba mizigo yao yote. Lakini wanaamini kabisa,
kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha
serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi wetu, tutaweza, kwa
kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya baadaye ya watoto na
wajukuu zetu. Tutaiondoa Tanzania miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na
mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa kabisa kwamba, tunaweza
kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua milango ya maisha bora
zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila mtanzania kuishi kwa
matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule kuanzia leo. Tutaweza
kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi akitumaini na kuamini
kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye ataishi kwa heshima,
raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini,
kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa
vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali yetu, haya
ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.
Watanzania
wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, mabadiliko
makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye uchumi wetu. Wanaamini tukichagua
kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi yetu kwa sasa na baadaye,
tutafanikiwa.
Tamko
Rasmi la Nia ya Kugombea Urais na Sababu
Ndugu
zangu nyote mliopo hapa, natangaza rasmi, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na
nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama
kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na utayari wangu. Na
ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa kina: mahitaji ya
sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto za kizazi chetu; uwepo wa fursa ya kugombea
na kushinda uchaguzi ujao; uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari, kufanya
maamuzi sahihi, na kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia utekelezaji;
uadilifu na uzalendo wangu; na zaidi nia yangu ya kuwa sehemu ya watanzania
wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika nchi yetu – mapinduzi ambayo
yatatia chachu ya mabadiliko ya namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa
na namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia.
Ninatangaza
nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania wanipime na kunitazama mwenendo
na uwezo wangu, nikiamini kabisa kuwa nitapimwa na kuungwa mkono ama kutoungwa
mkono, si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi yangu, si kwa umri wangu, na
wala si kwa daraja langu kwenye jamii, ama dini yangu, ama kabila langu.
Ninaamini nitapimwa kwa rekodi yangu, sifa, utayari, dhamira na uwezo wangu,
kama mtanzania.
Natangaza
nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano ili nipate fursa ya kuukimbiza
uchumi wetu kutoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi. Mimi ni mwanamabadiliko,
ninaamini nikipewa fursa, nitashirikiana na watanzania wenzangu na kwa pamoja
tutaunyanyua uchumi wetu kutoka kiwango cha kukua cha tarakimu moja kwenda kile
cha tarakimu mbili kwa miaka yote ya uongozi wangu. Ninaamini tutaweza kwa
pamoja kuukuza mchango wa kilimo kwenye GDP kutoka asilimia 4.2 kwenda zaidi ya
asilimia 6. Tukiyafanya haya naamini tutakuwa tumezalisha ajira nyingi zaidi kuliko
leo.
Ninaamini
katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi waliotutangulia
wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye matamanio yetu. Kizazi chetu
cha viongozi kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye ahadi
inayotokana na ndoto za waasisi wa Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba
jukumu hilo bila woga wala wasiwasi wowote ule, maana naamini tusipojitokeza
watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa na watu wasiostahili. Nina suluhu ya
changamoto kubwa za leo na kesho: kupigana na njaa na kuhakikisha usalama wa
chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko
ya tabia nchi ni miongoni mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia
kazi kwa haraka na umakini wa hali ya juu.
Na ndugu watanzania
wenzangu, amini nawaambia, kuwa tuna kazi ya ziada ya kufanya mbele yetu. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza
tukiamua; uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu
makubwa kwenye kuchukua hatua za kutenda.
Kutathmini
na Kuwapima Watia Nia
Nyote mliopo hapa na
wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la kututazama kwa ukaribu sana,
kututathmini na kutupima sote; tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za
matumaini, wanaotajwa tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa, ili wakati muafaka
ukifika muwape taarifa sahihi watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa
kuliongoza Taifa hili kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa,
ni nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake bali
kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na kuamua kwa
busara kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada ya kupima na kuchambua
aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.
Kuwa,
ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa na wajibu wa watu
wote, kama unavyolindwa na Katiba yetu, pia asili na historia yetu, anayeamini
katika haki ya kuabudu lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa
watanzania kutokana na dini zao.
Kuwa,
ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma bora za afya, elimu,
maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama wanavyopata mahakimu na
majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na wakurugenzi wetu.
Kuwa,
ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata haki hizi bila
kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.
Kuwa,
ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kila mtanzania ana bima ya afya na ya
maisha, na kwamba bima hiyo inampatia uhakika wa kupata huduma bora za afya
popote na kwa wakati anapozihitaji bila kumbagua kwa hali yake. Kwamba, itakuwa
mwisho sasa, ndani ya hospitali moja, kuwa na wodi nzuri wanazolazwa ‘wateule
wachache waliochangia bima ya afya’ na kuwa na wodi za ‘ilimradi’ tu
wanazolazwa wengine.
Kuwa,
ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na kujitegemea kwenye masoko na
malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani, kujitegemea kwenye masoko
ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula, kwenye chakula cha uhakika kwa ajili
ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi,
masoko na biashara za hasara na faida za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya
mipaka yetu. Ili tulinde thamani ya fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi
wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu?
Kuwa,
ni nani kati yetu anaichukia rushwa, anachukia wakwepa kodi wa makampuni
makubwa ya kimataifa yanayovuna raslimali za nchi yetu na hayalipi hata kodi
tu! Kwamba, ni nani atalinda raslimali za nchi yetu bila shaka. Kwamba, ni nani
kati yetu atahakikisha tunapata hisa za kutosha kutokana na uchumi wa raslimali
za madini, vito, mafuta na gesi? Kwamba, ni nani kati yetu atailinda ardhi ya
watanzania na kuhakikisha haivamiwi na wasaka ardhi kutoka nje ya Taifa letu,
kwamba atahakikisha ardhi inabaki kutumiwa kwa faida ya wakulima na wafanyakazi
wa nchi yetu?
Kuwa,
ni nani kati yetu ataweza kupambana na changamoto za usafiri na usafirishaji,
kuwa ataweza kuongeza tija na ufanisi kwenye bandari zetu, na ataweza kufufua
usafiri wa reli, ndege na meli?
Kuwa,
ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania walio wengi,
historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto zake, zinaakisi
‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la watanzania?
Wakati
ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa
sahihi, wachague mtu sahihi. Mtu ambaye ukimtazama kwa nje ana mvuto na analeta
matumaini kwa watanzania, ambaye ukimcheki hivi unasema ‘he is just a cool
guy’, lakini kwa ndani anaumia, anaungua moyo wake kwa ajili ya Tanzania yetu.
E
Pluribus Unum
Mimi
naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina
ya wengi, mmoja!
Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya uwingi
wetu. Siwezi kuwa salama kama wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama
wengine wanateseka. Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni
ya kwangu pia, na haiishii hapo tu, matatizo hayo si yangu na huyo mwenzangu tu,
ni yetu sote kama jamii.
Hivyo:
kitisho
cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu
na familia yangu.
Kucheleweshewa
haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, Arusha, ni
kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.
Mzee
Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa msaada na yeye
hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa siku ili asukume siku,
inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu yangu.
Mama
John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja wengi mtaani
kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Kariakoo; akifukuzwa, akapigwa virungu,
akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na mgambo
wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya biashara mahala pasiporuhusiwa,
inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama yangu.
Kama
kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini, hiyo inaniuma na
kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mwanangu.
Kato
na Kokugonza ni wanandoa wapya, wanaishi kijijini kule pembezoni ya Katerero,
Koku amepata ujauzito na amefikia kujifungua, kwa hali yake na namna mtoto
alivyokaa tumboni anapaswa akajifungulie hospitali ya wilaya ili ikibidi
kufanyiwa operesheni, basi afanyiwe; ikitokea uchungu umeanza ghafla na
akachelewa kufika hospitali ya wilaya sababu ya miundombinu mibovu na kukosa
ambulance mapema, akapoteza damu nyingi hadi umauti ukamkuta yeye na mwanae, ni
jambo lenye kuuma sana, si tu kwa Kato na wanafamilia wao, bali na mimi pia
linaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mdogo wangu.
Bwana
Kalumanzila ni mmachinga wa nguo za mitumba mitaani. Yeye huchukua nguo zake
kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume, akiuza anachukua
kifaida kidogo kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa ya mwenye mali Karume
jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata inamfanya aishi yeye na mkewe
na watoto wake. Akifukuzwa barabarani na akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya
kufanya na analazimika kumtumikia bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali
iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na madhila anayoyapata bwana Kalumanzila
zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mjomba wangu.
Fikra
hizi zinatokana, kwa kiasi kikubwa, na funzo nililopewa na babu yangu wakati
nikichagua kozi ya kusoma chuo kikuu, ambapo nilipata kitendawili cha kuchagua
kati ya kwenda kusoma udaktari ama sheria; aliniambia kuwa, “ni bora ukachagua
kusoma udaktari maana utapata baraka za Mungu kwa kujitoa kuwasaidia watu walio
na shida…” na akaendelea kusema kuwa “…kwenye maisha yako ikitokea ukapata mali
ama ukawa na nafasi kubwa ya kuamua juu ya mustakabali wa maisha ya wengine,
usisahau kumshukuru Mungu kwa kuwatendea yaliyo mema wenzako na Mungu atazidisha
Baraka zake kwako.” Leo miaka zaidi ya 15 baadaye naona maneno yake bado
yanaishi moyoni mwangu. Maisha yangu yote nimeikumbatia falsafa hii. Nimeifanya
kuwa dira ya utumishi wangu kwa wenzangu na kwa ulimwengu.
Falsafa
hii imenifanya nishindwe kuvumilia unyonyaji, ukandamizaji, uzembe, wizi na
ubadhirifu wa baadhi ya wenzetu walioshindwa kudumu kwenye njia ya kutoa haki,
uadilifu, uwajibikaji na utumishi uliotukuka.
Tamati
Ndugu
wanahabari, Tarehe 4, Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha Maendeleo
ya Dunia (Center for Global Development) alisema: “…Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania
kuongoza nchi masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi
yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka
mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…”
Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuongoza
nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi
wangu kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Kuna watu wanadhani uwepo
wa mfumo wa demokrasia imara, ama mfumo unaotoa uhuru na haki kwa watu wetu,
ama uwepo wa mfumo wa soko huria, ama utandawazi ni muarobaini wa kudumisha
amani yetu, mimi nasema, tunahitaji zaidi ya uhuru, zaidi ya demokrasia, zaidi
ya mifumo ya utandawazi, ama ya soko huria ili tudumishe amani na mshikamano
wetu – tunahitaji uhuru kwenye uchumi wetu. Tunahitaji uhuru kwenye mifuko ya
kila mtanzania. Uhuru wa kuchagua anachotaka kula, kuvaa ama huduma kwa ajili
yake na familia yake. Tunahitaji mabadiliko ya kifikra ili kuleta mapinduzi ya
uchumi tunayoyatarajia. Tunahitaji kupigana kuhakikisha kila mtanzania anajitegemea
kiuchumi. Hapo ndipo tutasema sasa tuna uhuru kamili.
Mungu
awabariki sana. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.
No comments:
Post a Comment