TATIZO LA UMEME NCHINI!

Tuesday, June 7, 2011
Mhe. Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla (MB), atauliza:-

(a) Tangu serikali ya awamu ya pili hadi leo, serikali imetumia jumla ya shilingi ngapi kuzalisha umeme, na bado tatizo lipo?

(b) Je, tatizo la umeme nchini litaisha lini?

(c) Kwa nini serikali inaongea mipango mingi ya kutatua tatizo la umeme bila kutekeleza na kwa nini suala la upatikanaji umeme nchini ni la dharura kila siku?

Waziri wa nishati na madini atajibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mhe. Spika, uwekezaji wa serikali katika miradi ya kuzalisha umeme tangu kipindi cha serikali ya awamu ya pili hadi leo unafikia jumla ya Dola za Marekani milioni 798.

(b) Mhe. Spika, tatizo la uhaba wa umeme litaisha baada ya kutekeleza kwa ukamilifu na kwa wakati mpango wa kipindi kifupi cha 2011 - 2015 kama ilivyofafanuliwa kwenye mpango kabambe wa uendelezaji wa sekta ya umeme wa mwaka 2009. Miradi itakayotekelezwa kipindi hicho itaongeza jumla ya MW 1830 kwenye mfumo wa gridi ya Taifa kwa gharama inayokadiriwa ya Dola za marekani milioni 3,700.

(c) Mhe. Spika, serikali imeazimia kutekeleza kwa wakati miradi ya kuzalisha na kusafirisha umeme kulingana na Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa sekta ya Umeme, hususan, katika kipindi cha 2011 - 2018. Miradi iliyopangwa kujengwa itaongeza MW 600 kwa kutumia maporomoko ya nguvu za maji, MW 870 kwa kutumia gesi asili, MW 1200 kwa kutumia makaa ya mawe na MW 100 kwa kutumia nguvu ya upepo. Serikali inategemea miradi hii itakamilika kwa kushirikisha uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuwa gharama za miradi hii yote ni kubwa.

Mhe. Spika, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza mikakati ya kutafuta fedha za kugharamia miradi ya kipaumbele niliyoitaja hapo juu.

Maswali Mawili ya Nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Kigwangalla:

(1) Kama toka awamu ya pili mpaka leo hii serikali ilitumia Dola za Marekani milioni 798 na bado hali ya upatikanaji umeme nchini ni duni kiasi hiki, serikali hii leo itapata wapi Dola za Marekani milioni 3,700?

(2) Mpaka leo miundombinu ya kusafirisha gesi kutoka Mnazi bay na Songosongo kwa ajili kuzalishia umeme kwenye mitambo iliyopo Dar es salaam ni duni na imechakaa, na uwekezaji kwenye bomba la kusafirishia gesi ni gharama kubwa, mnatuhakikishiaje dhamira ya serikali ya kulitatua tatizo la umeme kwa haraka kwamba ni ya ukweli au tutegemee kuendelea kufaidi mgao kila siku?

No comments:

Post a Comment